Tanzania yafikisha laini milioni 80.7 za simu

October 24, 2024 3:33 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Dar es Salaam imeshika nafasi ya kwanza kwa kuwa na laini milioni 14.8.
  • Mikoa ya Kusini Pemba na Unguja yashika mkia.

Dar es Salaam.  Huenda kasi ya maendeleo nchini Tanzania ikaongezeka, mara baada ya sekta ya mawasiliano kuendelea kushuhudia ukuaji chanya katika maeneo mbalimbali ikiwemo matumizi ya huduma za simu.

Mawasiliano ni nyanja muhimu katika kukuza maendeleo hasa katika mapinduzi ya nne ya uchumi wa kidijitali ambapo mawasiliano ndio kiungo muhimu.

Takwimu za mawasiliano za robo ya tatu ya mwaka 2024 zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha matumizi ya huduma za simu yameongezeka kwa asilimia tano.

Takwimu hizo zimebainisha kuwa mpaka Septemba 2024, usajili wa laini za simu umeongezeka hadi kufikia laini milioni 80.7 kutoka laini milioni 76.6 iliyorekodiwa katika robo ya mwaka iliyoishia Juni 2024.

Ongezeko hilo linajumlisha laini za simu za mkononi na za mezani ambazo zimetumika kwenye huduma ya mawasiliano angalau mara moja katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

laini hizo ni zile zinazotumika kwa mawasiliano ya binadamu (Person to Person – P2P) na zinazotumika kwa mawasiliano ya mashine (Machine to Machine – M2M).

Mtandao uliongoza kwa kusajili line nyingi zaidi kwa mujibu wa ripoti ya TCRA. Picha/Telecom Review.

Vodacom kinara wa laini nyingi

Hata hivyo, Mtandao wa Vodacom ndio unaoongoza kwa asilimia 56.2  kusajili laini nyingi zaidi za M2M kuliko mitandao mingine kati ya laini zote zilizosajiliwa.

 Airtel inashika nafasi ya pili kwa asilimia 32.7, ikifuatiwa na Halotel kwa  asilimia 5.9,Tigo asilimia 4.8 na TTCL ikiwa na asilimia 0.4 kwa kila mtoa huduma wa M2M.

Wakati kila mtoa huduma kwa M2M akisajili laini hizo takwimu za watoa huduma za P2P zinaonesha Vodacom ina asilimia 30.3, Tigo asilimia 29.4, Airtel asilimia 24.5, halotel asilimia 13.8 huku TTCL wakiwa na asilimia 2.0.

Dar es Salaam kinara kwa usajili wa laini Tanzania

Takwimu za TCRA zinabainisha kuwa mkoa wa Dar es Salaam imeshika nafasi ya kwanza kwa kuwa na laini milioni 14.8 zilizosajiliwa katika kipindi cha robo ya mwaka unaoishia Septemba 2024.

Laini hizo ziizosajiliwa Dar es Salaam ni asilimia 58.7 ya laini zote zilizosajiliwa nchini katika kipindi hicho, mara tano zaidi ya laini zilizosajiliwa katika mkoa wa Katavi uliosajili laini chache zaidi.

Jiji la Mwanza limeshika nafasi ya pili kwa kuwa na laini milioni 5.3 zilizosajiliwa ikifuatiwa na jiji la Arusha lililoshika nafasi ya tatu kwa kuwa na laini milioni 4.9, Mbeya nafasi ya nne ikiwa na laini milioni 4.6 na Dodoma ikiwa nafasi ya tano kwa kuwa na laini milioni 4.3.

Mikoa mingine ni Morogoro uliosajili laini milioni 4.1,Tabora laini milioni 3.9, Kilimanjaro laini milioni 3.1,Tanga laini milioni 2.9 na Geita laini milioni 2.6.

Mbali na mikoa hiyo, mikoa ya Tanzania visiwani ikiongozwa Kaskazini Unguja imesajili laini 73,743, Kusini Unguja yenye laini 110,970, na Kusini Pemba laini 124,472.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks