Ruto amteua Prof. Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais Kenya

October 18, 2024 12:00 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya Bunge la Seneti kupiga kura ya kumuondoa madarakani Rigathi Gachagua.

Dar es Salaam. Rais wa Kenya William Ruto amemteua Prof. Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais mpya nchini humo kujaza nafasi ya Rigathi Gachagua ambaye Bunge la Seneti lilimpigia kura ya kumuondoa mamlakani kufuatia shutuma 11 anazokabiliana nazo ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka na utakatishaji fedha.

Jina la Kindiki limesomwa bungeni na Spika wa Bunge la Kenya Moses Wetangula leo Oktoba 18, 2024 katika kikao kilichokuwa kinaendelea.

“Nimepokea ujumbe kutoka kwa Rais kuhusu uteuzi wa Prof Kithure Kindiki kujaza nafasi katika ofisi ya Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” ametangaza Wetangula huku akishangiliwa na wabunge.

Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya pindi Rais anapowasilisha uteuzi kwenye Bunge, wabunge watapiga kura ya kulikubali au kukataa kuliidhinisha jina hilo.

Prof. Kindiki, ambaye kwa sasa anahudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, atahitaji idhini kutoka kwa Bunge la Kitaifa kabla ya kushika nafasi ya Naibu Rais aambapo lazima Bunge lipigie kura uteuzi ndani ya siku 60 baada ya kupokea jina hilo.

Uteuzi wa Kindikiunakuja kufuatia Bunge la Seneti  jana Oktoba 17, 2024  kumuondoa ofisini Rigathi Gachagua kwa mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake na Bunge la Kitaifa.

Oktoba 8, 2024 wabunge 281 katika Bunge la Kitaifa walipiga kura ya ndio kumuondoa madarakani Gachagua kutokana na mashtaka 11 aliyotuhumiwa nayo ikiwemo kuihujumu serikali, kuhusika katika ufisadi, ukaidi na  kuendesha siasa za migawanyiko ya kikabila 

Hatua hiyo ni baada ya Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse kuwasilisha hoja ya kumuondoa Gachagua madarakani kutokana na sababu 11 alizoainisha Septemba 26, 2024 na kisha hoja hiyo kuungwa mkono na wabunge 291, ikiwa ni zaidi ya idadi ya chini ya wabunge 117 inayotakikana kuruhusu mjadala huo.

Sababu nyingine zilizotajwa na Mutuse kumuondoa Gachagua ni pamoja na kujikusanyia utajiri unaokadiriwa kuwa shilingi bilioni 5.2 katika kipindi cha miaka miwili dhidi ya mshahara wake wa jumla ya dola 93,000 kila mwaka tuhuma ambazo makamu huyo wa Rais alizikanusha kwenye mkutano wake na wanahabari Oktoba 7, 2024 akisema sehemu kubwa ya pesa zake zinatokana na urithi wa mali za kaka yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks