Njia za kugundua kamera zilizofichwa kwenye chumba

October 4, 2024 9:15 am · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link

Katika dunia ya leo kamera na vinasa sauti vinazoweza kufichwa kwa urahisi vimeenea zaidi kuliko wakati wowote kwa sababu ya maendeleo ya kiteknolojia yaliyorahisisha utengenezaji wa vifaa vidogo ambavyo ni vigumu kugundua.

Vifaa hivyo vidogo ambavyo mara nyingine haviwezi kuonekana kwa macho kirahisi, vinaweza kuharibu faragha yako katika sehemu tofauti kama hoteli, nyumba za Airbnb, vyumba vya kubadilisha nguo, au hata maeneo ya mikutano. 

Nukta habari tumekuletea mbinu na zana zinazoweza kutumika kugundua aina hiyo ya vifaa.

Kagua mtandao wa Wi-Fi 

Kamera nyingi za kisasa hutumia huduma ya mtandao wa Wi-Fi, hivyo ili kutambua uwepo wa kamera hizo kagua orodha ya vifaa vilivyounganishwa kwenye mtandao wa Wi-Fi kwenye chumba ulichopo kupitia kipengele cha mpangilio ‘setting’ kwenye simu yako au kompyuta na kisha kutafuta machaguo ya Wi-Fi ili kufuatilia vifaa vyote vinavyoonekana. 

Zana ya Wireless Network Watcher inayochunguza na kuonyesha orodha ya kompyuta na vifaa vyote vinavyounganishwa kwenye mtandao kwa wakati.

Kisha tumia nywila uliyopewa au programu tumishi ya router kutafuta sehemu inayoonyesha vifaa vilipowekwa. Ikiwa chaguo hilo halipatikani, tumia programu ya ‘Wireless network watcher’ katika vivinjari vya mtandaoni au ya ‘Who is on my Wi-Fi’ kutoka Play store kuona vifaa vyote vilivyounganishwa, ukiona kifaa kisichoeleweka kichunguze kwa makini hicho kinaweza kuwa kamera iliyofichwa.

Tumia tochi 

Mwanga wa simu unaweza kusaidia kugundua lenzi ya kamera. Zima taa chumbani na angazia mwanga kwenye sehemu zinazoweza kuficha kamera, kama vile pembe za vyumba au vifaa vya umeme.

Mara zote kamera zinatumia lenzi ambazo zina tabia ya kuakisi mwanga ili kurekodi. Hapa unaweza kutumia hata simu, cha kufanya zima taa zote kisha washa tochi kwenye simu yako na ukichunguze chumba kwa makini. 

Zingatia maeneo yanayoweza kuficha kamera kama vile vifaa vya kugundua moshi (Smoke detectors), mimea, au sehemu za juu za samani na uangalie kwa makini kama kuna mwangaza wowote unaong’aa kwa mbali au mwanga unaoakisiwa ambao unaweza kuwa ishara ya lensi ya kamera. 

Tumia Bluetooth

Ikiwa kamera hazijaunganishwa kwenye Wi-Fi, zinaweza kutumia Bluetooth. Hivyo ili kugundua uwepo wa kamera weka simu yako kwenye hali ya kuunganisha ‘Bluetooth’ na uangalie vifaa inavyoweza kugundua na uzingatie vifaa visivyoeleweka tofauti na vifaa vingine vya teknolojia ya nyumbani kama runinga na redio.

Utakapogundua kuwepo na vifaa vyenye majina yanayokupa wakati mgumu kuvitambua kirahisi tumia intaneti kuvitambua kwa jina na aina.

Tumia program tumishi za kugundua kamera

Kuna programu tumishi ambazo ni maalum za kwenye simu zinazoweza kugundua kamera zilizofichwa kwa kutumia teknolojia ya mtandao au kuhisi mwanga na mawimbi ya sumaku.

Programu ya ‘Hidden camera detector’ inayopatikana Play store inasaidia kugundua kamera na maiki zinazoweza kuwa zimefichwa, inapatikana pia kwenye App store ya Apple kama ‘Hidden camera detector’. Programu nyingine ni  ‘Hidden camera detector -peek’ ya App store, ‘Glint Finder – Camera Detector’ na ya Play store na.

Mwonekano wa programu tumishi ya Hidden Camera Detector ukionesha kifaa mojawapo kilichoshukiwa

Programu hizi hutumia sensa ya simu kutambua mawimbi ya Wi-Fi au Bluetooth ambayo mara nyingi kamera zilizofichwa hutumia kutuma video na sauti.

Kwa baadhi ya kamera zinazohifadhi video pasi na kuzituma kwa kutumia mawimbi yoyote itakua vigumu kuzigundua kwa mbinu hii, pia Program hizi zinaweza kugundua mawimbi ya vifaa vingine kama vile routers, simu au spika za Bluetooth hivyo uchunguzi wa kina utahitajika.

Chunguza matundu ya hewa

Mara nyingi kamera za siri huwekwa kwenye matundu ya hewa, kuta, vifaa vya kugundua moshi, au maeneo mengine yenye samani. Chunguza kwa makini sehemu zenye matundu yoyote na zinazoingiza hewa ndani ya chumba.

Tumia kifaa cha kugundua miale ya mwanga

Hii ni njia inayofanya uchunguzi kwa kina zaidi ya zote ikiwa bado una wasiwasi lakini ni yenye gharama zaidi kwani inahitajika kununua kifaa cha uchunguzi wa miale au cha kugundua joto dogo ambalo huzalishwa na kamera. 

Kifaa cha kugundua miale kinachosaidia kubaini vitu mbalimbali zikiwemo kamera zinazofichwa kwenye kuta, samani au katika mazingira ya giza kwa kuhisi joto. Picha |Amazon

Vifaa vya aina hiyo vinaweza kugharimu kati ya Sh408,000 hadi Sh544,000 na vinaweza kutumika kuchunguza kuta, vioo, au samani na sehemu nyingine yoyote unayotakiwa kuchunguzwa kwa ukaribu ili kutafuta vifaa vya kielektroniki vinavyofichwa.

Tumia kamera ya simu

Kamera nyingi hutumia mwanga wa ‘Infrared’ ambao macho ya kawaida hayawezi kuuona kama unaotumiwa na rimoti za zamani za televisheni hasa kama hazijaunganishwa kwenye Bluetooth au Wi-Fi.

Ili kugundua kamera iliyofichwa kisiri kwa kutumia mwanga wa ‘infrared’ unaotoka kwenye kamera iliyofichwa kwa kutumia kamera ya simu, zima taa zote chumbani kisha rekodi video kuzunguka maeneo yote chumbani.

Baada ya hapo angalia video hiyo ili kukagua na kuona kama kuna alama ya miale itakayoonekana ya rangi nyeupe ambayo hutoka kwenye kamera inayowezekana kufichwa mahali mwanga unapotokea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks