Watatu washinda vyombo vya moto kampeni ya Exim Bank
- Mmoja ashinda gari mpya aina ya Mazda CX-5, mwingine ashinda Bajaj ya TVS.
- Ni baada ya kuibuka washindi wa kampeni ya Tap Tap utoboe iliyoendeshwa na benki hiyo.
Dar es Salaam. Matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya kidijiti yamewawezesha watu watatu kushinda zawadi za vyombo vya moto kutoka benki ya Exim, ikiwa ni miongoni mwa fursa adimu kwa watumiaji wa huduma za kibenki Tanzania.
Washindi hao Geofrey Muganyizi, Irene Dominick, Bhavesh Gorecha waliopatikana kupitia droo ya mwisho ya kampeni ya kidigitali ya ‘Tap Tap utoboe’ iliyoendeshwa na benki hiyo yenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam.
Kati droo hiyo iliyofanyika Septemba 13 mwaka huu kwa usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Muganyizi aliibuka mshindi wa kwanza na kushinda gari jipya aina Mazda CX-5.
Mazda CX-5 ni miongoni mwa magari yanayobamba sokoni kwa sasa nchini yakipendwa haswa na vijana kutokana na muonekano wake na uimara.
Mshindi wa pili wa droo hiyo ya mwisho alikuwa ni Irene aliyejishindia pikipiki ya magurudumu matatu aina ya TVS wakati mshindi wa tatu Gorecha yeye akijinyakulia pikipiki aina ta Boxer BMX.
Benki hiyo imebainisha kuwa tangu kuanza kwa kampeni hiyo mwezi Juni, zaidi ya wateja 200 wameshinda zawadi za fedha taslimu ambapo washindi 10 kila wiki walipata zawadi ya Sh 50,000 huku washindi 10 kila mwezi wakiondoka na kibunda cha Sh100,000 kwa kipindi chote cha kampeni.
Mshindi wa pili wa kampeni ya ‘Tap Tap utoboe’ Irene Dominick akiwa ndani ya bajaji aina ya TVS aliyozawadiwa na Benki ya Exim. Picha|Exim Bank.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Stanley Kafu alieleza wakati wa makabidhiano ya zawadi hizo kwa washindi hao kuwa kampeni hiyo imechangia kuongeza uelewa na matumizi ya huduma za kidijitalii.
“Kampeni ya Tap Tap Utoboe imekuwa na matokeo mazuri katika kuongeza uelewa na matumizi ya huduma zetu za kidijitali. Tumefurahi kuwa wateja wetu wengi wamevutiwa na huduma hii na hili limedhihilishwa na ongezeko la miamala ya kidijitali tangu kampeni hii ianze mpaka sasa hivi hata kama imeisha,” amesema Stanley.
Kampeni hiyo ya miezi mitatu, ni sehemu ya jitihada za benki ya Exim kuhimiza jamii kufanya miamala kwa njia ya kielekroniki kama simu za mkononi na kuchagiza jitihada za Serikali kuchochea matumizi ya mfumo wa kifedha wa kidijitali.
Matumizi ya huduma ya kifedha kidijitali yamechochea kwa kiwango kikubwa kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini kutokana na kufikika kirahisi tofauti na huduma za kutegemea matawi ya benki pekee.
Geofrey Muganyizi, mshindi wa kwanza wa kampeni hiyo amesema hakuwa kufikiri kuwa siku moja angeweza kushinda chombo cha moto kwa kufanya tu miamala kama ilivyotokea.
“Kiukweli sikuamini kama naweza kushindi gari mpya kwa kufanya miamala yangu kwa simu na mtandao bila kuingia gharama zozote. Maana bahati nasibu zingine hadi utoe kitu ndo uwe mshindi lakini hii ya kipekee sana,” amesema Muganyizi.
Exim ni miongoni mwa benki zinazochuana vikali katika ubunifu wa huduma za kifedha kidijitali nchini huku ikiongeza mapato na faida mwaka hadi mwaka.
Katika mwaka wa fedha ulioishia Disemba 2023, benki hiyo iliripoti faida ya baada ya kodi ya Sh60.5 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 37.2 kutoka Sh44.1 bilioni iliyorekodiwa mwaka 2022.