Unawezaje kupata taarifa za kidijitali za mpendwa aliyeaga dunia? 

September 9, 2024 5:43 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kutuma maombi yatakayoambatana na cheti cha kifo kupitia nyenzo maalum ya ‘Google’.

Dar es Salaam. Baada ya kuangalia jinsi ya kuandaa mirathi mtandaoni kupitia akaunti ya kidijitali leo tuendelee mbele zaidi ambapo tutaangazia jinsi ya kupata taarifa hizo ikiwa mhusika ameaga dunia.

Kwa kawaida ni ngumu kupata taarifa za mtandaoni za mtu aliyefariki ila kupitia nyenzo maalum ya ‘Google’ unaweza kupata baadhi ya taarifa hizo endapo ukithibitisha uhusiano wako na marehemu.

Ili kupata taarifa hizo kutoka Google utahitaji kuwa na cheti cha kifo cha mpendwa wako, huku kwa watumiaji wa Apple wakitakiwa kuwa cheti cha kifo  pamoja na barua ya mahakama inayothibitisha wewe ndiye mrithi wa taarifa za mtandaoni.

Jambo unalohitajika kufanya ni kuwasiliana na Google ili kuomba taarifa ya akaunti, Hili linawezekana kwa kutumia nyenzo ya usimamiaji wa mirathi ya kimtandao kupitia kipengele cha udhibiti wa akaunti isiyotumika yaani Google’s Inactive Account Manager ili kutambulika kama mtu unaeaminika kuweza kupata taarifa baada ya muda wa akaunti kutotumika kwa muda mrefu.

Anza mchakato kwa kutuma ombi lenye maelezo ya akaunti ya marehemu na uhusiano mlionao, kisha wasilisha cheti cha uthibitisho wa kifo cha mtu huyo, huenda pia ukahitajika kutoa hati za ziada kama cheti cha ndoa ili kuthibitisha uhusiano wenu.

Baada ya kufuata taratibu hizo Google itafanya mapitio ya akaunti na kukagua ombi lako kwa makini ili kutathmini hali na kubaini kama wanaweza kukupa ruhusa ya ufikiaji unaohitaji. 

Taarifa zinazoweza kupatikana zinajuimisha kumbukumbu muhimu kama picha na video zilizohifadhiwa kwenye google drive, machapisho yaliyoandikwa kupitia ‘Google Docs’, namba za simu, baadhi ya barua pepe na matukio ya kwenye kalenda.

Kumbuka kuwa Google hutanguliza ufaragha za usalama wa taarifa za watumiaji wake hata baada ya kifo, hivyo kuna aina ya taarifa ambazo haziwezi kufikiwa hata baada ya kuwasilisha hati zinazohitajika endapo mhusika hatoandaa mirathi ya taarifa alizoruhusu kupatikana.

Taarifa zisizoweza kupatikana ni nywila na maelezo mengine yakuwezesha kuingia kwenye akaunti, maelezo, namba na taarifa nyeti  za akaunti ya benki, mawasiliano ya faragha yanayolindwa na sheria, taarifa zilizosimbwa kwa njia fiche na utumiaji wa YouTube.

Taarifa zilizohifadhiwa kwenye simu au kompyuta yenye nenosiri (password), alama ya kidole, au utambuzi wa uso haziwezi kupatikana kabisa. 

Nchini Tanzania, cheti cha kifo hutolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambapo pia unaweza kutumia mfumo wa kidigitali kufanya maombi ya cheti hicho. Picha|RITA.

Hata hivyo, itakusaidia kuondoa usimbaji fiche (encryption) uliotumia neno la siri ili kuwezesha kukihuisha kifaa chako katika hali ya kwanza kama kilivyotoka kiwandani (factory reset).

Kupitia chapisho lake Google inaeleza, “Katika hali fulani tunaweza kutoa maudhui kutoka kwenye akaunti ya mtumiaji aliyefariki. Katika matukio haya yote, wajibu wetu mkuu ni kuweka taarifa za watu salama na faragha

…Hatuwezi kutoa maneno ya siri au maelezo mengine ya kuingia mtandaoni (login details). Uamuzi wowote wa kukidhi ombi kuhusu mtumiaji aliyefariki litafanywa tu baada ya ukaguzi wa makini.”

Changamoto ya kutopatikana kwa baadhi ya taarifa muhimu kama meseji na barua pepe zinazoweza kuhitajika ili kushughulikia mambo muhimu kama fedha na taarifa nyingine binafsi inabainisha ulazima wa kupanga mapema warithi wa mirathi ya kidijitali. 

Pia mazungumzo ya wazi kati ya wanafamilia au watu wenye ukaribu kuhusu akaunti za mtandao na maneno ya siri yanaweza kupunguza mzigo wakati wa kipindi kigumu.

Unaweza kuanza mchakato wa kufanya taratibu za urithi kwa kidijitali kwa kutembelea kiunganishi hiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks