Serikali yazindua kadi janja kupunguza changamoto za abiria wa mwendokasi Dar

September 2, 2024 7:37 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Zitasaidia kupunguza foleni ya tiketi na kupunguza kutembea na fedha taslimu kwa ajili ya nauli.
  • Kuuzwa Sh 5,000 katika vituo vya mabasi yaendayo haraka.

Dar es Salaam. Serikali imezindua rasmi matumizi ya kadi janja katika vituo vya mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam hatua inayotarajiwa kupunguza baadhi ya changamoto ikiwemo foleni ndefu ya kukata tiketi au kulazimika kutembea na fedha taslimu kwa ajili ya nauli muda wote.

Hatua hiyo ya Serikali inakuja wakati ambao kumekuwepo na malalamiko kwa baadhi ya abiria wa mabasi yaendayo haraka kukaa vituoni kwa muda mrefu wakisubiri tiketi au wakati mwingine kukosa usafiri kwa kuwa mawakala hawana fedha za kuwarudishia abiria wanaotoa hela kubwa kununua tiketi yaani chenji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa aliyekuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa tukio hilo lililofanyika kituo kikuu cha mabasi yaendayo haraka leo Septemba 2, 2024 Kimara Mwisho amesema mfumo huo mpya wa kidijiti unaleta mapinduzi ya utoaji huduma wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART, kujibu hoja za wananchi na kutatua changamoto za kulipa nauli.

“Tunatambua kwamba hapo awali kabla ya mfumo huu wananchi walipata changamoto nyingi, wapo waliokua wakilalamika kuhusu kutorudishiwa chenchi kamili ya nauli zao, mfumo huu unakwenda kujibu malalamiko,” amesema Mchengerwa jijini Dar es Salaam.

Mchengerwa ameongeza kuwa teknolojia hiyo mpya iliyogharimu zaidi ya Sh11 bilioni kufunga mageti janja 300 katika vituo mbalimbali inatarajiwa kuokoa muda unaotumika na abiria kupanga foleni ya kukata tiketi, kuongeza imani ya abiria kwa huduma za  DART, kuepusha uvujaji wa mapato ya Serikali pamoja na kudhibiti watumishi wasio waaminifu.

Licha ya kutarajiwa kuwarahisishia safari abiria, mfumo mpya utasaidia wasimamizi wa mfumo huo kupata taarifa za abiria zitakazo wawezesha kufanya maamuzi ili kuboresha huduma na kupunguza udanganyifu.

Aidha, Mchengerwa amewataka maofisa wa DART kuhakikisha kuna upatikanaji rahisi wa kadi janja pamoja na kuhakikisha mfumo wa kadi hizo zinafungamanishwa na kadi janja nyingine zinazotumika kwenye usafiri ili kuwapunguzia abiria adha ya kubeba wa kadi nyingi wanapotumia usafiri huo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa akielekezwa jinsi ya ‘kuscan’ kadi janja kwenye geti janja na Mtendaji Mkuu wa DART Dkt Athumani Kihamia. |picha na Davis Matambo

Kuna uhaba wa mabasi

Hata hivyo Mchengerwa amebainisha kuwa anatambua kuna upungufu wa mabasi 170 kwenye barabara ya Kimara na mabasi 500 barabara ya Mbagala ambapo amewashauri watendaji wakuu wa mradi wa mabasi hayo kushirikisha kampuni za wananchi wazawa kuongeza idadi ya mabasi hayo ili kutatua changamoto iliyopo.

“Hakikisheni mabasi haya yamepatikana kabla ya Disemba, ongezeni ubunifu wakaribisheni Watanzania kushiriki kwenye zabuni za kuhudumia mabasi, zipo kampuni zina mabasi zaidi ya 300, nina imani kubwa kwa kuwa sasa kuna SGR mabasi mengi leo hii abiria sio wengi, wakaribisheni wale wadau wamiliki wa mabasi waje washirikiane na Serikali, tusitumie tu wawekezaji wa nje,” amesema Mchengerwa.

Bado uelewa ni mdogo

Licha Serikali kuzindua mfumo huo wa kidijiti, baadhi ya abiria bado hawatambui chochote kuhusu matumizi ya kadi hizo na ambapo wakidai gharama ya Sh 5,000 ya kununua kadi hiyo ipo juu jambo linaloweza kukwamisha juhudi za kuhamia kwenye uchumi wa kidijiti.

Iddi Kipenjo miongoni mwa abiria waliokuwepo kwenye kituo cha mabasi yaendayo haraka cha Kimara ameiambia Nukta Habari kuwa ni vyema wakapata kwanza elimu ya matumizi sahihi ya kadi hizo.

“Kwanza sijui kama kuna hizo kadi ndio naona hapa, kabla ya kuzizindua ni vyema wangetufundisha matumizi yake, isitoshe Sh5,000 ya kununulia kadi ni bei kubwa sana ukizingatia bado unatakiwa kuijaza nauli ya safari zako” amesema Kipenjo.

Jinsi kadi zinavyofanya kazi 

Ili kutumia mfumo huo, abiria atatakiwa kwanza kununua kadi janja kwa Sh 5,000 kisha aweke pesa anayotarajia kuituimia kama nauli kwa kipindi fulani.

Kadi hizo zinapatikana kwenye vituo vya mabasi yaendayo haraka na salio huongezwa kwa mawakala waliopo vituoni au kwa kutumia salio lililohifadhiwa kwenye simu.

Abiria wanaweza kutumia kadi janja hizo kuingia na katoka kituoni kwa njia ya ku ‘scan’ kwenye geti janja. 

Usajili wa kadi janja unafanyika kwa kutumia kitambulisho cha taifa (NIDA), cha mpiga kura au hati ya kusafiria.

Licha ya matumizi ya kadi janja za kidijiti kuanza leo bado kumekuwa na idadi kubwa ya abiria wanaondelea kutumia mfumo uliozoleka kukata tiketi kwa kutumia pesa taslimu hali inayotafsiri kuhitajika kwa juhudi za kuwaelewesha wasafiri wa mabasi hayo faida za matumizi ya kadi hizo.

Habari hii imeandikwa na Davis Matambo na Hemed Suleman

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks