TRA yawafunda washauri wa kodi Arusha

August 16, 2024 6:58 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Elimu hiyo itaongeeza uelewa wa mabadiliko ya kodi zilizopo katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2024.

Arusha. Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) imetoa elimu juu ya mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya mwaka 2024 kwa washauri wa kodi jijini Arusha ili kuongeza uelewa na ukusanyaji wa kodi kwa wananchi.

TRA imetoa elimu hiyo ikiwa ni miezi miwili tangu kuanza kwa mwaka mpya wa fedha na utekelezaji wa mabadiliko ya kodi katika Sheria ya Fedha Julai Mosi 2024.

Miongoni mwa Sheria mpya za Kodi  zilzoanzwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha ni pamoja na watengeneza maudhui mtandaoni kukatwa kodi ya asilimia tano kutokana na malipo ya kazi zao pamoja na kutoza kodi kwa asilimia tatu kwa wauzaji wa mali za kigiditali.

Alex Mwambenja, Afisa Msimamizi wa Kodi Kanda ya Kaskazini aliyekuwa akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika leo Agosti 16, 2024 jijini Arusha amesema kuwa malengo ya mafunzo hayo ni  kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na kutoa fursa ya kupokea maoni kutoka kwa walipa kodi.

“Tunavyotoa semina hii tunawapa fursa ya kutoa maoni ushauri na namna bora ya sisi kama TRA kukusanya kodi kwahiyo wasiogope wafike katika semina zetu ambazo zinaendelea nchi nzima watupe maoni yao na sisi tuboreshe utendaji wetu..

…Lakini maoni yanayohusu sera au sheria tutayachukua na kuwasilisha Wizara ya Fedha kwa kamishna wa wa sera za kodi ili baadae waziri wa fedha awaslishe bungeni kwasababu mabadiliko ya sheria za kodi ni mchakato endelevu,” amesema Mwambenja.

Wakwepa kodi kufikiwa

Rose Damaseni ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo amesema elimu hiyo itawasaidia kuongeza uelewa na kuwafikia wakwepa kodi na kupunguza vitendo hivyo nchini.

“Kupitia elimu hii na sisi kama washauri wa kodi tumepata uwezo wa kwenda kuwaelemisha walipa Kodi mitaani…ninaamini hata vitendo vya baadhi yao kufunga maduka kukimbia maafisa wa TRA vitapungua,” amesema Damaseni.

Kwa upande wake CPA Yussuph Zege mshauri wa kodi mkoani Arusha amesema kuwa utaratibu huo unaofanywa na TRA unawasaidia kuongeza uelewa na ufahamu kuhusu sheria mpya kwa kuwa sio wote wamepata nafasi ya kuzipitia baada ya kupitishwa rasmi na Serikali.

“Kuna Sheria mpya za kodi zimebadilishwa  au zimepewa hadhi mpya hivyo tumekuja hapa kupewa elimu sahihi ili kuhakikisha kwamba hao walipa kodi wanalipa kodi bila kuathirika kutokana na Sheria mpya,” amesema CPA Zege.

Ili kuendelea kuongeza uelewa wa mabadiliko ya kodi yaliyopo katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 TRA imesema itandelea kutoa elimu kwa washauri wa kodi na wananchi katika mikoa ya Manyara na Singida.

Enable Notifications OK No thanks