Majaliwa atoa maagizo kukabiliana na athari za El Nino Tanzania
- Ni pamoja na kuboresha miundombinu, kuelimisha wananchi na kuandaa mikakati ya kukabiliana na athari.
- Wananchi washauriwa kuzingatia taarifa kutoka TMA.
- Wasisitizwa kuweka akiba ya chakula na kulima mazao yanayostahimili ukame.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaagiza mawaziri, wakuu wa mikoa na taasisi zote za Serikali kuchukua hatua za kukabiliana na athari za ongezeko la mvua nchini El Nino, ikiwemo kuainisha na kuandaa rasilimali za kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na maafa na kuelimisha wananchi kuhama maeneo hatarishi.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza wakati akitoa hoja ya kuaihirisha Bunge la 13 jijini Dodoma amewaambia wabunge kuwa mafuriko yatayotokana na El Nino, yanaweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo za kiafya, kiuchumi, kijamii, na upotevu wa mali hivyo ni vema tahadhari zikachukuliwa mapema kuzuia na kukabiliana na athari hizo.
“Idara zinazohusika na mazingira na miundombinu, zihakikishe barabara zinapitika wakati wote, mitaro na kalavati yanazibuliwa na yanaimarishwa, na kusafishwa ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi,” amesema Majaliwa.
Hata hivyo, baadhi wa wananchi jijini Dar es Salaam wameonekana wakilalamika kwa Serikali kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu rafiki ya kusafirisha maji ya mvua jambo lililosababisha kufurika kwa maji katika baadhi ya barabara na kuchochea uwepo wa foleni, hatua inayokwamisha ufanyaji wa shughuli za kiuchumi kwa ufanisi.
Soma zaidi : TAA kukabidhiwa rasmi uwanja wa ndege KIA, Novemba 10, 2023
Waziri Mkuu Majaliwa amezisisitiza sekta za umeme, maji na mawasiliano kuweka mipango ya kuzuia madhara na uharibifu katika huduma hizo, huku wakitakiwa kuwashirikisha wadau wa maafa wakiwemo wananchi, taasisi za umma na sekta binafsi katika mipango yote ya usimamizi wa maafa.
Aidha, wananchi wametakiwa kutoa taarifa mara moja punde yanapotokea maafa ili kupata msaada, huku kamati zote za maafa za kijiji, wilaya, mkoa na Taifa zikitakiwa kujipanga kwa dharura yoyote itakayojitokeza.
Zingatieni taarifa za TMA
Ili kufahamu muelekeo wa mvua za El Nino, Majaliwa amewasihi Watanzania kujenga utaratibu wa kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kutekeleza miongozo inayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikiwemo kuhama maeneo hatarishi na kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi kwenye maeneo salama.
Soma zaidi : Mambo muhimu ya kuzingatia unapokata rufaa ya mkopo HESLB 2023 – 24
Maeneo yatayokumbwa na mvua nyingi
Kwa mujibu wa TMA mikoa itakayokabiliwa na mvua za juu ya wastani ni pamoja na Kagera, Mwanza, Manyara, Geita, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Kusini mwa Mkoa wa Simiyu, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Mafia na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro.
Wakaazi wa maeneo hayo wameaswa kuweka akiba ya vyakula kwa wingi kwa kuwa mvua zinaweza kuathiri upatikanaji wa chakula pamoja na kulima kwa wingi mazao yanayostahimili hali ya mvua nyingi, ili kuepukana na changamoto ya uhaba wa chakula.