Anayetapeli watu mikopo kwa majina ya viongozi Tanzania atiwa mbaroni
- Ni mmiliki wa kampuni ya VICOBA Foundation inayodaiwa kuwatapeli wananchi kwa kutoa mikopo mtandaoni.
- Pia inadaiwa kutumia majina ya viongozi wa Serikali kutimiza uhalifu huo akiwemo Rais Magufuli.
- Benki Kuu ya Tanzania yawatahadharisha wananchi na kampuni zinazotoa mikopo mtandaoni.
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema mmiliki wa kampuni ya VICOBA Foundation anashikiliwa na vyombo vya dola kwa ajili ya uchunguzi kwa madai ya kujihusisha na utapeli wa kutoa mikopo kwa kutumia majina ya viongozi wa Serikali akiwemo Rais John Magufuli kwa njia ya mtandao.
Taarifa ya BoT iliyotolewa leo (Januari 9, 2020) inaeleza kuwa imebaini uwepo wa kampuni za kitapeli ikiwemo ya VICOBA Foundation inayodaiwa kutoa mikopo kwa wananchi ndani ya muda mfupi baada ya kujiunga kwa kuweka amana kwa njia ya mtandao.
“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuufahamisha umma kwamba mmiliki wa VICOBA Foundation kwa sasa anashikiliwa na vyombo vya dola ambavyo vinaendelea na uchunguzi ili kuchukua hatua stahiki,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, BoT haijaweka wazi jina la mmiliki huyo wala bila kueleza kiundani mkoa anaoshikiliwa.
www.nukta.co.tz inaendelea na jitihada za kuwatafuta viongozi wa kampuni hiyo licha ya hatua za awali kugonga mwamba. Hadi sasa, hakuna taarifa za anuani ya makazi ya kampuni hiyo mtandaoni, tovuti wala mitandao ya kijamii inayoonyesha shughuli na mawasiliano yao.
Zinazohusiana:
- NMB yaingiza sokoni huduma tatu za kidijitali kwa mpigo.
- BoT yashusha tena riba kwa benki za biashara Tanzania.
- Ukopeshaji sekta binafsi waongezeka zaidi ya mara 10 Tanzania.
BoT imeeleza kuwa kampuni hiyo pia imekuwa ikitumia majina ya viongozi wakuu wa nchi na watu mashuhuri katika kufanikisha utapeli wao yakiwemo majina ya Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hasan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kampuni hiyo inadaiwa kutoa mikopo ya kuanzia Sh2 milioni hadi Sh10 milioni baada ya mteja kulipia ada ya kujiunga ya kati ya Sh200,000 hadi Sh500,000.
BoT imesema ili kuvutia wananchi, kampuni hiyo imekuwa ikiudanganya umma kuwa ni taasisi ya Serikali jambo ambalo halina ukweli wowote.
Aidha, uchunguzi wa awali wa BoT unaonyesha kuwa kampuni hiyo haina hata ofisi ya kudumu.
Katika kuwaokoa wananchi wengine kuingia katika mikono ya matapeli hao, benki hiyo imewataka wananchi kuchukua tahadhari juu ya uwepo wa kampuni za kitapeli zinazodai kutoa mikopo ndani ya muda mfupi kwa njia ya mtandao.
Aidha, imetoa onyo kwa mtu, kikundi au taasisi yoyote inayojihusisha na biashara ya upokeaji amana au utoaji wa mikopo bila kuwa na leseni kuacha mara moja, la sivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Latest