Maboresho makubwa mtandao wa WhatsApp
- Ni maboresho yatakayoruhusu akaunti moja kutumika na zaidi ya simu moja.
- Wadau wasema itakuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara na wenye makampuni.
- Changamoto za usalama na faragha zatolewa ufafanuzi.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha inafikia matarajio na kukidhi mahitaji ya watumiaji wake, mtandao wa WhatsApp umeendelea kufanya maboresho mbalimbali ili kuendelea kuwepo katika soko la ushindani.
Mtandao huo unaomilikiwa na kampuni ya Facebook unakusudia kufanya mabadiliko ya mfumo wake yatakayowezesha akaunti moja kutumika katika zaidi ya simu moja.
Hiyo ina maana kuwa mtumiaji anaweza akafungua WhatsApp katika simu zaidi ya moja na akaendelea kufanya shughuli zake za mawasiliano bila kikwazo chochote.
Licha ya kuwa WhatsApp haijatoa tamko lolote kuhusu maboresho hayo, kampuni ya Techradar ambayo inafanya uchambuzi wa maboresho yanayofanywa na mitandao ya kijamii imesema kama mtandao huo utafanikiwa utaondoa changamoto ya watu kulazimika kutumia namba moja ya simu kwa kifaa kimoja.
“Uchaguzi wa kuendesha WhatsApp katika zaidi ya kifaa kimoja ni jambo ambalo watu waliamini lingekuwepo tangu mwanzo, sasa rasmi inaonekana liko njiani,” imeeleza sehemu ya uchambuzi wa kampuni hiyo ya Marekani.
Kwa mujibu wa Techradar, maboresho hayo yatamuwezesha mtu kutumia akaunti hadi kwenye simu nne na zote zinaweza zikawa zinajitegemea. Picha| Shuyyerstock.
Endapo maboresho hayo yatakamilika na kupitishwa, huenda yatatua changamoto za watumiaji wa WhatsApp akiwemo mkazi wa jijini Dar es Salaam, Issa Kipande.
Issa Ameiambia Nukta kuwa, kwa WhatsApp ya sasa, akaunti moja ya mtandao huo inayosajiliwa kwa kutumia namba ya simu inaweza kutumika kwenye kifaa kimoja tu.
“Unapokua na simu mbili ni lazima kuwa na laini mbili tofauti ili zote ziweze kuwa na WhatsApp. Ukipoteza simu, umepoteza kila kitu,” amesema Kipande.
Changamoto hiyo inamfanya inalenga changamoto ya kupoteza taarifa muhimu ikiwa simu imepotea au kuharibika.
Kutumia WhatsApp kwenye kifaa zaidi ya kimoja siyo kitu kigeni kwa sababu sasa mtu anaweza kuitumia akaunti yake ya WhatsApp kwenye kompyuta akiwa ameunganisha na simu yake iliyo karibu na iliyounganishwa na intaneti.
Kwa mujibu wa Techradar, maboresho hayo yatamuwezesha mtu kutumia akaunti hadi kwenye simu nne na zote zinaweza zikawa zinajitegemea.
Ni sawa na kusema, kama una simu mbili, unaweza kutumia akaunti moja ya WhatApp huku kila simu ikiwa inajitegemea. Vivyo hivyo kwa walio na simu nne.
Zinazohusiana
- WhatsApp inavyowabeba wajasiriamali Tanzania
- Una kipi cha kujivunia miaka 10 kuzaliwa WhatsApp?
- WHO sasa yaingia Whatsapp kutoa taarifa za Corona
Mtaalamu wa Teknolojia ya mawasiliano (IT) kutoka kampuni ya Scan Code Tanzania, Prosper Susuma ameiambia Nukta kuwa hatua hiyo huenda ikawa msaada wa kurahisisha mawasiliano ya kampuni na wateja wao.
“Kuna wakati mtu unahitaji kuwasiliana na mtu kwa masuala ya kiofisi. Kama hauna simu ya ofisi, utalazimika kutumia namba yako binafsi kitu ambacho siyo kizuri,” amesema Susuma.
Hata hivyo, mtaalamu huyo amesema WhatsApp inapaswa kutengeneza mfumo ambao utasimamia simu zinazotumia akaunti moja ili kuepusha changamoto za usalama na usiri wa taarifa za watumiaji.
“Iwe rahisi kujua kuwa hii namba inatumika na watu wanne lakini aliyefanya kosa ni fulani mwenye simu fulani,” amesema Susuma.
Naye Mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano (IT) Jensen Kiswabi amesema licha ya kuwa maboresho hayo yana umuhimu sana, WhatsApp wanatakiwa kuwa makini na ulinzi wa mtu kwani vifaa vinavyotumika (simu) hupotea au kuharibika.
“Inaweza kuwa kitu kizuri kama kutakuwa na ulinzi zaidi. Mfano kama utakuwa hewani kwenye kifaa kimoja, vingine vizimwe hadi uwe unakitumia lakini zaidi ya hapo itakuwa imesaidia kupunguza shida ya kuwa na akaunti tofauti kwa kila simu,” amesema Kiswabi.
Kwa upande wake Lilian Patrick, mtumiaji wa mtandao huo mkoani Morogoro, maboresho hayo yatakuwa na faida kwake kwani yatamsaidia anapokuwa ameishiwa chaji kwenye simu yake nyingine huku simu ya ziada ikiwa na chaji.
“Simu yangu kuu inashuguli nyingi. Mara nyingi inaisha chaji mapema kuliko simu ya ziada. Kwa kuwa ninakuwa na uwezo wa kutumia WhatsApp kwenye simu zaidi ya moja, itaniweka hewani hata pale simu yangu kubwa itakapozima,” amesema Patrick.
Latest
