Ndege kugeuzwa kumbi za sinema, migahawa Singapore
- Ni za Shirika la ndege la Singapore ambapo wateja watapata huduma ya chakula kwenye ndege zake bila kuhitaji kusafiri.
- Pia wataweza kuangalia filamu na kusikiliza muziki ili wajihisi wako angani.
- Hatua hiyo ni kuongeza wigo wa mapato wa shirika hilo.
Dar es Salaam. Licha ya kuwa kazi ya ndege ni kuwasafirisha watu na mizigo katika maeneo mbalimbali kupitia anga, baadhi ya mashirika ya ndege duniani yameanza kubuni huduma mpya zinazowawezesha watu kufurahia usafiri huo hata kama hawasafiri.
Shirika la ndege la Singapore (SIA) limetambulisha shughuli tatu ikiwemo huduma ya chakula zitakazokuwa zinatolewa kwenye ndege zake ambazo ziko katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Changi uliopo nchini Singapore.
Shughuli hizo zitakuwa zinatolewa wakati ndege haisafiri kuwawezesha watu wanaopenda kufurahia mandhari ya kukaa ndani ya ndege ili kuwapatia mtazamo mpya.
Shirika hilo katika taarifa yake ya hivi karibuni, limesema Oktoba 24 na 25, 2020, wateja wake watapata fursa ya kuingia kwenye ndege yake aina ya Jumbo A380 ili kupata chakula na burudani kwenye mgahawa uliopo ndani ya ndege hiyo.
“Wateja watakula vyakula mbalimbali vitakavyoandaliwa na wahudumu huku wakitazama filamu na kupata burudani nzuri ndani ya ndege,” imesema taarifa ya shirika hilo.
Ili kupata fursa ya kuingia kwenye ndege hiyo yenye ghorofa moja (double-decker), unatakiwa kulipia Dola za Marekani 50 (Sh115,998) ili ukae daraja la kawaida.
Wanaotaka kukaa katika daraja la juu (business class) wao watalipia Dola za Marekani 220 (Sh510,397) na daraja la watu binafsi ni Dola 440 sawa na Sh1.1 milioni.
Sehemu ya ndani ya ndege aina Jumbo A380 ya Shirika la Ndege la Singapore. Picha|SIA.
Licha ya kuwa ukiingia kwenye ndege hiyo ya kifahari, haitapaa angani lakini utafurahia huduma bora za kwenye ndege ili upate hisia sawa na mtu aliyepo angani.
“Wale wataokaovaa nguo za kitamaduni kama “sarong kebaya”, “cheongsam”, “saree”, mashati ya batiki watapata zawadi maalum,” limesema Shirika hilo.
Tiketi za kuingia kwenye ndege hiyo zitaanza kuuzwa kuanzia Oktoba 12 mwaka huu kupitia tovuti ya KrisShop.com.
Katika huduma yake ya pili, shirika hilo litatoa fursa ya wateja wake kutembelea kituo chake cha mafunzo (SIA Training Centre) ambapo watajifunza jinsi ya kuendesha ndege, kutoa huduma kwenye ndege na warsha za unadhifu kwa wahudumu wa ndege.
Ili kupata fursa ya kutalii katika kituo hicho, tiketi zitaanza kuuzwa kuanzia Novemba 1, 2020 ambapo shughuli hiyo itafanyika Novemba 21, 22, 28 na 29, ingawa SIA haijasema gharama za utalii huo.
Soma zaidi:
- Waziri azungumzia ndege za ATCL kuchelewa, kuahirisha safari
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
- ATCL inavyojitanua kimataifa
Kama hautaki kutoka nyumbani, pia unaweza kufurahia huduma hizo popote ulipo.
Kuanzia Oktoba 5 mwaka huu, shirika hilo litazindua huduma yake ya SIA@Home ambapo wakazi wa Singapore watasambaziwa chakula chenye hadhi ya juu na kati kinachotolewa kwenye ndege zake moja kwa moja kwenye nyumba zao.
Wakazi hao wanaotakiwa kuweka oda za chakula wanachopendelea, pia wanaweza kuagiza vitu vya gharama ambavyo wasafiri wanavipata wakati wakisafiri na ndege hizo ikiwemo mvinyo na suti.
Shirika hilo limeamua kutoa huduma hizo baada ya kufanya utafiti kuhusu mahitaji ya soko, ushindani wa biashara ya ndege na kuamua kugeukia shughuli nyingine ambazo zitasaidia kupata mapato zaidi wakati huu wa janga la Corona (COVID-19).
Latest