Programu tano bora za elimu Tanzania mwaka 2020

January 5, 2021 6:10 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Smart Class, Ubongo Kids na Shule Direct ambazo zinatoa huduma ya kielimu kuanzia ngazi ya chekechea hadi vyuoni.
  • Programu nyingine huenda zikawafaa waajiriwa na wajasiriamali.

Dar es Salaam. Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia ongezeko la programu nyingi za simu na kompyuta zenye dhamira ya kuboresha utoaji wa elimu na upatikanaji wa zana za kujifunzia kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari.

Kila programu ina malengo ya kutoa suluhu ya changamoto za kielimu Tanzania kuhakikisha Taifa linafikia adhimio la nne la malengo endelevu la elimu bora licha ya ukweli kuwa baadhi ya programu hizo zinatofautina kiwango cha ubora na mawanda yake. 

Kwa mwaka 2020, timu ya Nukta Habari imefanyia uchambuzi baadhi ya programu zilizoanzishwa Tanzania na kuzipima katika urahisi wa kuzitumia, upatikanaji na wingi wa vifaa na zana za kujifunzia. 

Ukilinganisha na miaka ya nyuma, programu hizi za kidijitali zimezidi kuimarishwa ubora na waanzilishi wake wameonekana kujitoa katika kuhudumia Watanzania. 

Mchango wa wabunifu hao katika kuboresha elimu ulionekana zaidi wakati Taifa lilipokuwa katika janga la ugonjwa wa corona. Baadhi ya wanafunzi waliokuwepo nyumbani baada ya shule kufungwa walinufaika na ubunifu huu wa Watanzania kwa kujifunza zaidi.  

Hata hivyo, si programu zote za simu na kompyuta zinazotoa huduma za elimu Tanzania zitashika namba moja. Pia, ukweli ni kwamba kiwango kikubwa cha watu waliopakua programu au app husika huenda isiwe pia kiwango sahihi cha kupima ubora wa huduma husika. 

Tunaamini kuwa zipo baadhi ya programu zisizo maarufu kutokana na ama uchanga wake au ukosefu wa mitaji wa waanzilishi wake kuzitangaza lakini zina mchango mkubwa katika kuboresha elimu nchini kupitia jukwaa la kidijitali. 

Baada ya uchambuzi uliofanyika, hii ndiyo orodha ya programu tano bora za elimu kwa mwaka 2020 kutoka Tanzania. 

Mchango wa wabunifu hao katika kuboresha elimu ulionekana zaidi wakati Taifa lilipokuwa katika janga la ugonjwa wa corona. Picha| Core Tanzania.

5. Programu tumishi (app) ya Mtabe

Programu hii inatoa huduma ya notsi za wanafunzi kwa njia ya mtandao au njia ya ujumbe mfupi (SMS) ikilenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia hususan vitabu kwa wanafunzi.

Kinachoipa kete programu hii ni uwezo wake wa kuwafikia wanafunzi wenye intaneti na wasiokuwa nayo bila malipo. 

Kwa ambaye anakifaa kinachomwezesha kutumia intaneti, anaweza kupakua app ya Mtabe na kujipatia notsi kwa ajili ya kujisomea na kama hilo ni ngumu, Mtabe inapatikana pia katika mtandao wa WhatsApp, inayopatikana kwa sehemu kubwa kwenye baadhi ya simu za wazazi. 

Kwa ambaye hana kifaa kinachotumia intaneti, anaweza kuitumia programu hiyo kwa meseji za kawaida maarufu kitaalamu kama USSD japo siku za hivi karibuni ufanisi wake umekuwa na matokeo mseto. 

Kati ya changamoto za programu hii ni pamoja na kutokupatikana katika simu zinazotumia programu endeshi ya iOS hususan za iPhone na ugumu wa kupata taarifa za kutumia mfumo wa SMS. 

Njia ya kujiunga na Mtabe kwenye simu ambayo ni kutuma neno “SAJILI” kwenda “0745622622”  inayoelekezwa haitoi majibu kwa haraka kama inavyotangazwa jambo linalotengeneza ugumu kwa mwanafunzi kupata majibu ya haraka. Hata njia fupi ya SMS ya kutuma swali kwenda 91011 huchelewa kutoa majibu jambo ambalo Mtabe watatakiwa kulitatua katika mwaka 2021. 

Licha ya kutoa suluhu muhimu katika upatikanaji wa zana za kujifunzia,  baadhi ya taarifa za kutumia mfumo wa mtabe ni ngumu kupata. Picha| Mtabe.

4. Elimu Tube Africa

Uzuri wa programu hii ni uwepo wa mafunzo ambayo huenda mwanafunzi au yeyote anayejifunza asiyapate darasani. Mafunzo yanayotolewa na jukwaa hili la mtandaoni yanaweza kumsaidia mtu yeyote kuanzia mjasiriamali, mwanafunzi na mfanyakazi wa kila rika.

Programu hiyo ya mtandaoni (web-based)  inatoa suluhu ya elimu ya uwasilishaji (presentation skills), jinsi ya kutengeneza fedha za ziada na mengine mengi huku ikimpatia mtumiaji kulipia mafunzo yake kwa njia mbalimbali zikiwemo za simu (Airtel money, M pesa na Tigo Pesa).

Hata hivyo, huduma inayotolewa na jukwaa hili inalipiwa kuanzia Sh5,000 na inampa mtu yeyote nafasi ya kufundisha somo fulani ilimradi ana ujuzi na amethibitishwa kufundisha kozi zinazohitaji uthibitisho zikiwemo za masuala ya afya. 

Pia, Jukwaa hili linaweza kuwa ajira kwa wadau ambao wanafaa kuwa walimu kwani ni sehemu ya wao kujiongezea kipato. Kwa kila kozi inapolipiwa, mwalimu anapata asilimia 70 ya malipo hayo huku asilimia 30 ikirudi Elimu Tube Africa.

Hata hivyo, moja ya changamoto ambayo huenda ikaikabili huduma hii ni udhibiti ubora wa madhui ya watu wanaotoa mafunzo. Je, kwa kiwango gani wanachofundisha kinakidhi viwango wakati wote?

Ili kuboresha ubora wa mafunzo, ni vema uongozi wa Elimu Tube ukaweka vigezo vikali zaidi juu ya  mtu anayetoa somo fulani ili mafunzo yanayotolewa yawe yanategemewa (reliable).


3. Smart Class

Kwa wazazi ambao hawapendi kuwaona watoto wao wakiwa wamekaa bila kujishughulisha katika kipindi cha likizo, huenda wakafurahishwa na programu hii.

Smart Class inayopatikana kwa njia ya mtandao ni programu inayowaunganisha walimu na wanafunzi kwa ajili ya masomo ya ziada. Siyo wanafunzi pekee bali ni mtu yeyote ambaye ana nia ya kujifunza jambo hata iwe jinsi ya kupanda mahindi na maharage.

Hii inaipatia Smart Class sifa ya kuwafikia watu wa rika zote huku ikitoa ellimu iliyopo katika mtaala wa elimu na kuwafikia hata watu wa kawaida wakiwemo wakulima, wana muziki na wanaohitaji kujifunza mapishi. 

Kupitia jukwaa hilo la elimu, mwanafunzi anaweza kusoma kwa njia ya mtandao na hata kukutana kwa gharama kuanzia Sh3,000 kwa saa moja.

Smart class inatoa nafasi ya mtu kujifunza somo lolote katika ngazi yoyote kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu ikiwa na masomo mengi yakiwemo mtaala wa darasani, kilimo, mapishi, afya, muziki na michezo.

Licha ya kuwepo walimu waliothibitishwa, baadhi ya waalimu bado ni wanafunzi wa chuo kikuu na hivyo huenda wasifikie kiwango kizuri cha ufundishaji. Ili Smart Class itimizie lengo la kuwafikia wengi zaidi yapaswa kuongeza kasi ya kujitangazai kuongeza walimu kwa baadhi ya masomo yakiwemo kupika keki ambalo lina mwalimu mmoja. 


Soma zaidi:


2. Shule Direct

Programu hii inapatikana mtandaoni na pia inapatikana kama app katika simu za Android na vifaa vinavyotumia mfumo endeshi wa iOS hivyo kuwa na mawanda mapana ya kuwafikia wanafunzi.

Kupitia jukwaa hili, mwanafunzi anaweza kupata vitu vya kujifunzia kuanzia Notsi, vitabu, mitihani ya zamani na hata majaribio (quiz) na uwezo wa kuchati na mwalimu roboti almaarufu kama Ticha Kidevu ambaye ana uwezo wa kujibu swali la mwanafunzi ndani ya muda mfupi.

Jukwaa hili la elimu la bure linawanufaisha wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita kwa kuwapatia nafasi ya kufanya majadiliano ndani ya jukwaa hili pasipo na mipaka ya sehemu walizopo. 

Pia, maudhui yaliyopo katika tovuti na programu ya Shule Direct, yanamfikia mwanafunzi kwa njia ya maandishi na video jambo ambalo linaweza kuwa msaada kwa wanafunzi wengi hasa katika masomo ya sayansi.

Ndani ya Shule Direct, kuna video  mbalimbali zikiwemo 29 za somo la Kemia (chemistry) zilizo na maelezo ya jinsi ya kufanya vipimo ya sampuli (sample testing) ambavyo wanafunzi hufundishwa shuleni. Video hizo za sayansi ni moja ya vitu vya kipekee vinavyofanywa na programu za kidijitali zinazotoa elimu mtandaoni. 

Zaidi kuhusu jukwaa hili, ni uwezo wa mwanafunzi kununua vitabu vya masomo ya sayansi vya wanafunzi wa kidato cha tano na sita na uwepo wa mitihani ya wanafunzi wa darasa la nne, saba na kidato cha sita licha ya kujikita na wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi nne.

Kitu ambacho Shule Direct inaweza kukifanya ili kuwa bora zaidi, ni kuiangalia upya huduma ya Ticha Kidevu kwani majaribio yaliyofanyika hayakutoa majibu yanayoridhisha. Mfano, Ticha Kidevu aliulizwa sababu za vita vya maji maji kwa Kiingereza na alijibu kwa kutaka kumfahamu mwanafunzi zaidi na hata baada ya kufahamiana, hakutoa jibu.

1. Ubongo Kids

Moja ya ubunifu mkubwa wa Ubongo Kids ni kurahisisha masomo kwa kuweka katika mfumo wa burudani ikiwemo hesabu. Matumizi ya vikaragosi ama katuni, michezo ya kielimu na urahisi wa upatikanaji na wingi wa maudhui ni moja ya sifa zinazofanya huduma hii kuwa msaada mkubwa katika uchangiaji wa elimu Tanzania. 

Ubongo Kids ina programu ya simu (app), inafanya kazi katika tovuti (web-based) na isambaza maudhui yao katika redio na televisheni jambo linalosaidia kuwafikia watoto wengi zaidi wakiwemo wa vijijini ambao si rahisi kupata intaneti. 

Watoto hufundishwa alfabeti, kusoma na hisabati, maarifa ya jamii na stadi za kazi. Katika kipindi cha tathmini ya programu hii, mafunzo yaliyoonekana ni pamoja na ubaguzi wa kazi kati ya jinsia ya kiume na kike na umuhimu wa kufanya mazoezi pamoja na ushirikiano baina ya watu.

Mbali na kufanya mafunzo kuwa burudani, mbinu inayotumika na waendeshaji wa programu hii ya nyimbo za kuwafurahisha watoto inafanya programu hii kuwa bora kwa kumfundisha mtoto wako masomo ya awali na hata kufaa kwa burudani pale anapokuwa nyumbani ikiwa ni mbadala wa katuni za nchi za Magharibi kama Ben10, Sophia the First na nyinginezo. 

Kupitia Ubongo Kids, mzazi anaweza kuchagua lugha anayohitaji mtoto ajifunzie ikiwa ni Kiingereza, Kiswahili au Kifaransa, kutazama video, kupakua app mbalimbali na kucheza michezo ikiwemo ya kupaka rangi na kuhesabu.

Zaidi, matumizi ya wahusika walio na majina ya Kiswahili kama Kibena, Kiduchu, Koba, Baraka, Amani, Mama Ndege na Mzee Kigo huenda yakawapatia ukaribu wanafunzi kwa kuwa kwa namna moja ama nyingine majina hayo yanasadifu mazingira yao. Ni jitihada kubwa ya kutengeneza majina ya wahusika wa Kiswahili vichwani mwa watoto.

Ili kujenga ukaribu na watoto, Ubongo Kids au washirika wanaweza kutengeneza mabegi, fulana, madaftari na bidhaa mbalimbali za watoto zilizo na wahusika hao kama ilivyo kwa katuni zingine. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW