Upatikanaji wa dawa bado kitendawili Tanzania
- Upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya washuka.
- Mikoa 11 iko chini ya wastani wa kitaifa wa upatikanaji wa dawa wa asilimia 66.4.
- Serikali yasema itaimarisha mifumo kuongeza dawa mikoani.
Dar es Salaam. Licha ya Serikali ya Tanzania kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu kwenye vituo vya kutolewa huduma afya, mikoa 11 ukiwemo Mkoa wa Tanga haijaweza kufikia wastani wa kitaifa wa upatikanaji wa dawa kimkoa, jambo linaloweka afya za Watanzania mashakani kwa kukosa matibabu kwa wakati.
Dawa aina 312 ndizo zimeainishwa kuwa ni dawa muhimu na za kipaumbele cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa lengo la kuhakikisha kuwa zinapatikana nyakati zote katika Bohari ya Dawa (MSD).
Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2021/22 iliyowasilishwa bungeni Mei 11 na Dk Dorothy Gwajima, katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021, hali ya upatikanaji wa dawa hizo katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ilifika asilimia 75.6 ikishuka kutoka asilimia 80 kipindi kama hicho 2019/20.
Hata wakati, upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya ukishuka kidogo, takwimu za wizara hiyo zinaonyesha kuwa wastani wa upatikanaji wa dawa kimkoa kwa sasa umefikia asilimia 66.4 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Hiyo ni sawa na kusema takriban watu 7 kati ya 10 wanaokwenda katika vituo vya kutolea huduma wanapata dawa muhimu.

Licha ya wastani huo ambao ni theluthi mbili ya kiwango cha upatikanaji wa dawa kimkoa, hakuna hata mkoa mmoja ambao ulioweza kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa dawa.
Mathalan, Mkoa wa Dar es Salaam ambao ndiyo wenye kiwango cha juu cha upatikanaji wa dawa Tanzania Bara umefikia asilimia 76.2 ya upatikanaji wa dawa hizo muhimu kwa binadamu.
Wakati Dar es Salaam ikiongoza, Mkoa wa Tanga ndiyo umeshika nafasi ya mwisho katika upatikanaji wa dawa muhimu kwa kuwa na asilimia 49.6. Tanga ndiyo mkoa pekee ambao haujafikia nusu ya upatikanaji wa dawa muhimu kitaifa.
Mkoa huo umeungana na mikoa mingine 10 ambayo upatikanaji wa dawa muhimu uko chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 66.4.
Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inaitaka Serikali kwa kushirikiana na wadau kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuzingatia ubora na mahitaji ya nchi.
“Kuhakikisha kwamba dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vinapatikana wakati wote, kwa kiasi cha kutosha na ubora unaotakiwa,” imeeleza sehemu ya sera hiyo.
Soma zaidi:
Mikakati itakayosaidia kuongeza kasi ya upatikanaji wa dawa
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Sikika katika moja ya andiko la masuala ya dawa, linapendekeza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) isiwe msambazaji (mshitiri) bali kuwawezesha wauzaji binafsi kusambaza dawa kwenye vituo vya afya.
Pia inashauri Serikali iweke mifumo imara ya kudhibiti upotevu wa dawa vituoni. Mfumo ulioanzishwa wa kielektroniki wa kuendesha hospitali (GoT-HoMIS) ukisimikwa vituo vyote nchini utaweza kusaidia kupunguza tatizo hilo.
Waziri wa Afya, Dk Gwajima amesema mwaka 2021/22 Serikali itaimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kulingana na
Dk Gwajima katika hotuba yake amesema katika mwaka 2021/22 Serikali imetenga Sh151.4 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa ambazo zitasambazwa katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma za afya.
Kati ya fedha hizo, Sh4.6 bilioni zimetengwa mahususi kwa ajili ya usambazaji wa dawa ili kuhakikisha vituo vya afya vinakuwa na dawa muhimu wakati wote zinazoendana na mahitaji.
Latest