Ndani ya Ifisi: hifadhi ya wanyamapori inayotoa pumziko kwa wakazi wa Mbeya
- Ni mahali pekee ambapo utaona wanyamapori na kutembea katika korongo.
- Mbuga yenye Kasuku mwenye zaidi ya miaka 30.
- Ni moja ya sehemu nzuri ya kupumzika na familia kipindi cha likizo katika mkoa wa Mbeya.
Mbeya. Licha ya Mbeya kuwa mji unaosifika kwa kuwa na ardhi nzuri inayovutia na yenye rutuba ya kutosha lakini kuna vingi vilivyojificha katika mkoa huu vitakavyokufanya ufurahie uwepo wako mkoani humo.
Hali ya hewa ya Mbeya haichoshi kutembea kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo katika mji huu uliobarikiwa kuwa na safu za milima na madhari nzuri ya kijani. Wenyeji huita Mbeya “Green City” yaani Jijini la Kijani.
Hata wakati ukipanda Mlima Loleza na kutembelea jiji kati maarufu kama Uhindini kuna mahali hautakiwi kukosa kufika iwapo wewe ni mpenzi wa kutazama wanyamapori: Hifadhi ya Wanyamapori na Makumbusho ya Ifisi (Ifisi zoo and Museaums0.
“Bustani” hiyo ya wanyama iliyopo kilomita 4.3 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe ina korongo kwa ajili ya kwenda kuzunguka na kuangalia wanyamapori wafugwao wakiwemo swala, fisi, ngedere, nyumbu na chatu.
Sanjari na utalii wa wanyama hao, kwa wanaofika katika kivutio hicho cha kulipia watafanikiwa kuona nyumba ya utamaduni au makumbusho yenye vifaa vya kitamaduni kutoka kwa watu wa makabila ya Nyanda za Juu Kusini wakiwemo Wanyakyusa, Wafipa, Wasafwa, Wahehe na Wabena.
Kwa wapenzi wa ‘camping’ na watu wanaopenda kupumzika sehemu ambapo watakuwa huru na utulivu wa kutosha huenda eneo hilo likawa suluhisho kwa muda wakati wakijipanga kwenda kwenye hifadhi kubwa za jirani na mkoa huo kama Kitulo, Ruaha au Katavi.
Baadhi ya watalii waliotembelea Ifisi wakiwa eneo mojawapo la nymba za asili. Picha|Zahara Tunda.
Ifisi, iliyofunguliwa mwaka 2008 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ipo umbali wa Kilometa 19 kutoka Mbeya Mjini ikiwa pembezoni mwa barabara inayoelekea nchini Zambia.
Kuingia na kufurahia vivutio vya Ifisi lazima uvunje ‘kibubu’ kidogo.
“Wakubwa wanapaswa kulipa Sh3,000 wakati wanafunzi wa sekondari wanalipa kiingilio Sh2,000. Wanafunzi wa shule za msingi na watoto Sh1,000. Huku hakuna tofauti kwa kulipia maana hadi wageni nao wanalipa kiingilio cha aina moja,” anasema Stanley Kiduko, Msimamizi Msaidizi wa Ifisi.
Wanafunzi wakiwa michezoni ndani ya Bustani ya wanyama ya Ifisi. Picha|Zahara Tunda
Kiduko ameiambia Nukta kuwa sehemu kubwa ya wanaotembelea zoo hiyo ni wageni huku kundi kubwa la wenyeji wanaofika kutembelea kivutio hicho wakiwa wanafunzi jambo linaloonyesha kuna wenyeji wengi ambao hawajabahatika kufanya utalii huo wa ndani.
Je, utaona nini ukiwa Ifisi?
Ukiwa Ifisi utamuona kasuku mwenye umri wa miaka 32 ambaye ni kivutio katika zoo hiyo huku kukiwa na tausi ambao wa kiume huwa wazuri na wenye rangi za kuvutia. Vilevile utaona Nungunungu pamoja na bata aina mbalimbali watakaokufanya ufurahie mandhari hiyo ambayo huchagizwa na ubaridi kidogo wa jiji hilo.
Hata hivyo, kuna wanyama kama fisi, sungura, ngedere wa aina mbalimbali, nyoka kama chatu na wengine wengi.
Kinachovutia zaidi ni jinsi utakavyoweza kupanda kibao maalumu ambapo utaona kwa karibu madhari ya bustani ya wanyama kwa ukaribu zaidi vilevile utapata bahati ya kuzungushwa porini na kuona swala wakiwa katika harakati zao za kujitafutia chakula.
Sehemu inayotumika kuangalia madhari ya eneo lote la Bustani ya Ifisi. Picha| Zahara Tunda
Inafaa kufundishia watoto urithi wa Taifa
“Ni sehemu nzuri sana kuwaleta watoto, kwanza wanajifunza na kuwaona wanyama ambao wanawaona kwenye vitabu tuu” anasema Mwalimu Faudhiat Mpamba kutoka Good Shepherd academy.
“Nawashauri wazazi na walimu wawalete watoto wao kwa kuwa pia pana sehemu ya michezo ambayo inamfanya mtoto afurahie kuwepo hapa,” anamalizia Faudhiat.
Licha ya kuwa wanaishi katika mji huo, baadhi ya wakazi wa Mbeya wanasema kwa wale ambao hawana uwezo mkubwa wa kwenda kuona vivutio vya wanyamapori katika hifadhi za Taifa Ifisi huenda ikawasaidia kujua utajiri wa wanyamapori uliopo nchini.
“Mimi napapenda Ifisi kwa kuwa hutumii gharama kubwa kupafikia na unaangalia wanyama na kipindi ambacho hakuna mvua huwa wanatupeleka hadi kule juu nyikani kuona swala na kuangalia madhari nzuri ya korongo,” anasema Chando Adam, mkazi wa Mbalizi jijini hapa.
Msimamizi wa bustani ya Ifisi, Stanley Kiduko akimuelezea mwandishi kuhusu ngoma za asili za wakazi wa Nyanda za Juu Kusini. Picha|Zahara Tunda.
Ukiachana na hoteli inayomilikiwa na zoo hiyo, kwa wageni wanaweza kupata malazi katika hoteli za jirani Mbalizi au Mbeya mjini ambapo kwa taxi usafiri ni wastani wa Sh20,000 au Sh1,000 kwa wanaotumia daladala.
Pamoja na fursa ya kutoa utalii katika mkoa huo, zoo hiyo inakabiliwa na changamoto za miundombinu kutembelea wanyama waliopo porini katika eneo hilo kwa kuwa wakati wa masika barabara huwa mbovu kuingia katika korongo hilo.
Eneo la Korongo linavyooneka ukiwa juu kwenye eneo la kuangalia madhari ya Bustani ya Ifisi.Picha| Zahara Tunda.
Pia, ili kuona wanyama wote baadhi ya watalii watapaswa kulala maeneo hayo kwa kuwa baadhi ya wanyama hawaonekani nyakati za mchana na uongozi umelazimika kuruhusu wageni kuingia usiku.
Kama ilivyo kwa vivutio vingine vya kitalii nchini, zoo ya ifisi imechangia kuwapa ajira baadhi ya wakazi wa mji huo wanaofanya shughuli za uhudumu, watoa usafiri kama taxi na bodaboda na wanaouza vyakula na watoa huduma za malazi.