Rahma Bajun: Mjasiriamali anayetamba kimataifa
- Awashauri vijana kutokata tamaa kwenye biashara wakue na biashara zao.
- Kuwa na nidhamu ya muda ni jambo muhimu katika kufanikiwa katika ujasiriamali.
Huenda wewe ni mmoja wa watu ambao hawaamini kuwa kazi ya kushona na kubuni mitindo ya mavazi inaweza kumuingizia mtu kipato na kumuweka kwenye ramani ya dunia.
Basi ni tofauti kabisa, kwani kupitia kazi ya kushona nguo za mitindo mbalimbali kwa kutumia cherehani, imewatoa watu wengi kimaisha na kuwafanya kutambulika na taasisi kubwa duniani kutokana na umahiri na ubunifu walionao katika sekta ya ushonaji nguo.
Mmoja wa watu hao ni Rahma Bajun; Mtanzania mjasiriamali aliyewekeza nguvu zake kwenye ubunifu wa mitindo ya mavazi na ushonaji wa nguo za wanaume na wanawake zenye asili ya Afrika kwa kutumia vitenge.
Rahma (29) ambaye ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa kampuni ya ushonaji nguo ya MnM Clothing Line yenye makao yake jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa wanawake wachache ambao wameteka soko la ushonaji nguo la Afrika Mashariki na kujipatia mafanikio lukuki.
Kutokana na bidii na kuamini anachokifanya, Rahma ametajwa katika Jarida la Forbes kuwa miongoni mwa vijana wajasiriamali 30 wa Afrika ambao biashara zao zinakuwa kwa kasi (30 Most Promising Young Entrepreneurs in Africa 2018).
Forbes la Marekani ambalo hutambua wajasiriamali na mabilionea sehemu mbambali duniani, lilimtambua Rahma kama mmoja ya vijana 30 wanaochipukia katika ujasiriamali barani Afrika kutokana na shughuli yake hiyo ya ushonaji.
Heshima hiyo kwa binti hiyo ilitokana na uwezo wake wa kutumia vizuri rasilimali na kubuni mavazi yenye muonekano wa kuvutia kwa wateja wake.
Mafanikio ya Rahma siyo ya bahati mbaya, yametokana na juhudi, uvumilivu na kujituma licha ya kukutana na vikwazo vingi katika safari yake.
Baadhi ya watu mashuhuri nchini kama Maria Tsehai Sarungi na Zitto Kabwe huva nguo hizo zilizoshonwa na kampuni ya Rahma. Baadhi ya wateja wake wakuu wa wanatoka katika mataifa mbalimbali ulimwenguni zikiwemo nchi jirani za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Rwanda.
Hivi karibuni Nukta ilifanya mahojiano na Rahma ambayo yanaweza kuwa chachu kwa vijana wenye ndoto za kufika kwenye kilele cha mafanikio katika ujasiriamali.
Nukta: Ulijisikiaje kuwepo kwenye orodha ya vijana 30 wenye mustakabali mzuri kiujasiriamali Afrika katika Jarida la Forbes?
Rahma: Nilishtuka na kufurahi kuona kwamba ninachofanya kinapiga hatua na watu wanaona na wanakubali tunachokifanya.
Nukta: Safari yako ya ubunifu wa masuala ya ushonaji ilianzia wapi?
Rahma: Safari yangu imeanzia mbali sana. Nimekuwa nikifanya kazi kwenye sekta za vijana na harakati za vijana kwa muda mrefu na nakumbuka nilikuwa napata nafasi ya safari za nje ya Tanzania kwenda kwenye masuala ya utamaduni. Kila nikienda nje nilikuwa napenda kuvaa nguo za vitenge au zenye rangi ya bendera ya Taifa. Nikienda kwa fundi kushona nilikuwa nampangia na kubuni jinsi navyotaka kitenge changu au nguo yangu ishonwe na iweje.
Rahma akiwa katika duka lake la nguo zilizoshonwa tayari. Picha|Zahara Tunda.
Nukta: Kipi kilikusukuma zaidi na kuona ni wakati wa wewe kujikita katika ujasiriamali wa kushona?
Rahma: Mwaka 2013 nilikuwa nafanya kazi na watu wa Sweden na nilikuwa naenda sana Burundi kule nilikuwa naona vitenge vingi kutoka Kongo, nilikuwa napata vitenge vizuri vyenye rangi za kiafrika nikirudi nikawa napeleka kwa mafundi kushona lakini changamoto ilikuwa inakuja kwa mafundi aidha achelewe kukushonea au ashone tofauti na mlivyokubaliana. Nikawa najiuliza kwanini inakuwa hivi? Nikaanza rasmi kufanya tafiti kwa jinsi gani nitaweza kumpatia mtu nguo kwa wakati na kumshonea ikawa na hadhi anayoitaka mteja.
Nukta: Kwahiyo baada ya tafiti zote rasmi mlianza lini hadi leo tunakujua Rahma Bajun wa MnM Clothing line?
Rahma: Tulianza rasmi mwaka 2016 kuwa na ‘center’ yetu ya kushona, nilianza na fundi mmoja baada ya mwezi nikawa na mafundi wengine, mpaka leo tuna wafanyakazi saba. Pia, nje ya hapa tuna mafundi wengine zaidi ya 20 ambao tuanawatumia tukiwa na oda nyingi. Ila mimi kazi yangu kubwa ni kusimamia ‘design’ (mtindo) pamoja na ‘quality’ (ubora) ya nguo.
Nguo na bidhaa nyingine kutoka MnM clothing line picha| Zahara Tunda.
Nukta: Unaonaje mwelekeo wa kazi hii ya ushonaji Tanzania?
Rahma: Inakuwa na watu wengi wanafanya hadi wasomi, lakini zamani ilizoeleka ni kazi ya watu wasiosoma au walioshindwa maisha, ila sasa watu wanaichukulia ni kazi nzuri.
Nukta: Mnashona nguo za aina gani?
Rahma: Sisi tunashona nguo za aina zote yaani za maharusi, ofisini na za matukio mbalimbali licha ya kushona tunabuni pia mikoba, mabegi, notebooks na viti na meza za matairi.
|
Mabegi yaliotengenezwa na kubuniwa kwa vitenge kutoka MnM. Picha| Zahara Tunda.
Nukta: Malighafi zenu katika kushona mnazitoa wapi?
Rahma: Malighafi nyingi tunazinunua nchini, lakini kuna vitenge vingine ni vya Kongo na hapa tunajitahidi pia kutengeneza nguo kwa kutumia kanga ili kutangaza nchi yetu katika mavazi ya kanga.
Nukta: Mnakumbana na changamoto gani katika sekta hii ya ushonaji?
Rahma: Kwa mimi changamoto kubwa; kwanza hatuna vifaa na ‘fabrics’ (malighafi) ambazo zipo Tanzania, vifaa tunanunua vya India, China au Uturuki na bado kama vitenge vya Kongo unaweza ukaenda nunua Kenya au Uganda bado usafiri na gharama za kuviingiza nyingi. Vilevile suala la kukatika kwa umeme ni changamoto kubwa mashine tunazozitumia kushona zinahitaji sana umeme hivyo ukikatika unakuwa unaturudisha nyuma sana.
Nukta: Ulifikiria nini kuanzisha mtandao wa MnM online shopping?
Rahma: I ‘think’ (nafikiri) ni njia nyingine ya kuongeza thamani ya biashara, kwa kuwa watanzania na ambao sio watanzania wengi nje ya Tanzania wangependa kuona na kununua nguo au bidhaa zetu. Kwa hiyo kuweka mtandaoni bidhaa hizo kumetufanya tuweze kuwafikia wale ambao watashindwa kuja dukani kwetu kununua basi wataona mtandaoni na kuchagua wanachokitaka.
Rahma akionyesha baadhi ya urembo na mito iliyobuniwakwa folonya za vitenge.Picha|Zahara Tunda.
Nukta: Unaushauri gani kwa vijana wanaoogopa sana kujiajiri?
Rahma: Nawashauri waangalie wanachokipenda na waanzie chini kabisa wakue na biashara zao pia wasikate tamaa mapema.
Nukta: Umesema wewe umeajiriwa na bado unaweza kumudu biashara yako, je unajigawaje?
Rahma: Najitahidi sana kutunza muda, naamka mapema sana nawahi ofisini saa moja na nusu kabla ya muda wa kuingia ofisini ambao ni saa 2:00 asubuhi na natoka jioni saa 11 hadi saa 2:30 usiku na hapo naenda MnM kuhakikisha mambo yameenda vizuri na kama kuna kazi ya kufanya nitafanya.
Nukta: Unajiona wapi miaka 10 ijayo?
Rahma: Hili ni swali gumu sana ambalo mara nyingi nashindwa kujibu. Kusema ukweli naona kama si mimi au MnM basi sekta ya ushonaji itakuwa imekuwa na unaona sasa hivi watu wanashona hata za harusi.
Nukta: Neno la mwisho kabisa kwa watu wote wanaosoma makala hii.
Rahma: Nachoweza kusema ni kwamba nafurahi kuona Watanzania wa kawaida kutoka familia za kawaida wanafanikiwa hata hivyo ili kujenga nchi yetu inahitaji jitihada za kila mtu ili tuweze kuipata Tanzania tunayoitaka.