Wataalam wa benki kupigwa msasa utakatishaji fedha

September 18, 2018 8:09 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya fedha jinsi ya kutambua na kukabiliana na matukio ya utakatishaji fedha yanayotokea katika benki.
  • Utakatishaji fedha ni miongoni mwa matukio yanayoathiri mzunguko halali wa fedha.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha utakatishaji na udanganyifu wa fedha unadhibitiwa, Taasisi ya Mafunzo ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inakusudia kutoa mafunzo kwa wadau wa sekta ya fedha nchini ya kutambua na kukabiliana na matukio ya utakatishaji fedha yanayotokea katika shughuli za kibenki.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na taasisi hiyo, mafunzo hayo yatafanyika katika tawi la BOT la Mtwara Septemba 24 hadi 28 mwaka huu ambapo yanawahusu waatalam wa taasisi za fedha wanaohusika na ukaguzi, uhazini, mahusiano ya wateja na uendeshaji wa shughuli za benki.

“Mwishoni mwa mafunzo, washiriki kutoka taasisi za benki na wadau wengine watakuwa na maarifa katika maeneo mbalimbali ikiwemo mikakati ya kufuatilia akaunti, miamala yenye mashaka na jinsi ya kuepuka mianya ya kutokea kwa vitendo vya utakatishaji fedha,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 

Pia itakuwa ni jukwaa muhimu kwa wadau wa sekta ya fedha kufahamu mifumo ya kibenki inayohusika na ufuatiliaji wa miamala na hatari yoyote inayoweza kujitokeza wakati wa shughuli za kibenki ambapo watajengewa uwezo wa kudhibiti kabla tukio lolote la utakatishaji halijatokea.

BOT inachukua jukumu hilo la kutoa mafunzo, ikizingatiwa kuwa taasisi hiyo ndiyo mlezi na mwangalizi wa benki zote zilizopo nchini ili kuhakikisha shughuli zao zinazingatia sheria na kanuni zilizowekwa na kuwa sehemu ya kukuza uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha Haramu ya mwaka 2006 inataja utakatishaji fedha kama kosa la kisheria  ambapo adhabu yake ni kifungo au faini isiyopungua 100 milioni kutegemeana na thamani ya mali au fedha iliyotakatishwa.

Kitengo cha Kudhibiti Biashara (FIU) katika Wizara ya Fedha na Mipango kinatoa tafsiri ya Utakasishaji wa Fedha Haramu  kama shughuli au vitendo vyenye lengo la kuficha ukweli au asili ya fedha au mali iliyotokana na uhalifu. 

Pia inaweza kuwa namna ya kujipatia fedha haramu yaani zimepatikana kutokana na shughuli isiyo halali kisheria na kutafuta njia mbali mbali kuziwezesha fedha hizo zionekane kuwa ni halali. Baadhi ya shughuli hizo ni biashara ya dawa za kulevya, ugaidi na usafirishaji fedha kinyume na sheria. 

Vitendo vingi vya utakatishaji fedha hufanyika kupitia taasisi za fedha, jambo linaloathiri mzunguko wa fedha na shughuli za kiuchumi kutokana na fedha zisizo halali kuingizwa kwenye mfumo rasmi wa kibenki.

Utakatishaji fedha ni tatizo linaloitesa dunia ambapo mwaka 2015 Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Uharifu na Dawa za Kulevya (UNODC) ilifanya utafiti kubaini ukubwa wa tatizo ambapo iligundua kuwa Dola za Marekani 1.6 trilioni sawa na asilimia 3.6 ya pato la dunia zinatakatishwa kila mwaka.

Enable Notifications OK No thanks