Sababu zinazofanya usipande na vitu hivi kwenye ndege

October 18, 2018 1:09 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kwa wasafiri wa ndege, usalama ni jambo muhimu kuliko yote.
  • Wasafiri wa mara ya kwanza wanapashwa kufuatilia kwa karibu aina ya mizigo wanayotakiwa kusafiri nayo.
  • Ufahamu wa mizigo unayoruhusiwa na usiyoruhusiwa kubeba utakusaidia kukamilisha ndoto zako.

Una ndoto za kupanda ndege? Au una mpango wa kupanda ndege siku za hivi karibuni? Ni jambo jema lakini unapaswa kufahamu mambo kadhaa ambayo yatakusaidia kukamilisha ndoto yako na kukuepusha na usumbufu unaoweza kutokea kabla ya kufika uwanja wa ndege.

Kila sehemu ambayo inawakutanisha watu wa kada tofauti kuna taratibu zake. Hata usafiri wa ndege una taratibu zake za mizigo unayoruhusiwa au usiyoruhusiwa kubeba. Ufahamu huo utakusaidia kujipanga kabla hujatoka nyumbani na kuhakikisha safari yako inakuwa ya mafanikio.

Inspekta Mkuu Kitengo cha Usalama wa Usafiri wa Anga (TCAA), Burhani Majaliwa ameiambia Nukta kuwa kuna mizigo ya aina mbili ambayo abiria anapaswa kuielewa wakati wa safari yake na kuiweka katika mfumo unaokubalika na mamlaka za ukaguzi kwenye viwanja vya ndege.

“Kuna mizigo ya mikononi (hand or carry-on luggage) ambayo abiria huruhusiwa kuingia nayo ndani ya ndege na mizigo mikubwa inayohifadhiwa kwenye eneo la mizigo wakati wa safari (Check in or Hold baggage),” anasema Majaliwa.


 Vitu visivyoruhusiwa kwenye ndege

Usafiri wa ndege ni tofauti na usafiri mwingine wa ardhini ambapo suala la usalama linapewa kipaumbele cha kwanza kuliko mambo yote.  Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ambayo imepewa jukumu la kusimamia usalama wa viwanja vyote vya ndege nchini imeelezea kwa kina orodha ya vitu visovyoruhusiwa kwenye ndege.

Orodha hiyo inaongozwa na Kanuni za usalama wa usafiri wa anga (Civil Aviation Security Regulations) za mwaka 2015 ambazo zimetoa mwongozo vitu ambavyo abiria hataruhusiwa kusafiri navyo isipokuwa kwa utaratibu maalum ni pamoja na silaha, milipuko na vitu vyenye ncha kali. 


 Vitu vinavyoweza kulipuka

Vitu vyote ambavyo vinavyoweza kulipuka na kusababisha madhara kwa abiria wengine wa ndege huwezi kupita navyo kwenye dawati la ukaguzi. Vifaa hivyo ni kama baruti, fataki, maguruneti, kitu chochote kinachotoa miale ya mwanga na midoli. 


Vitu vinavyoweza kuwaka kirahisi

Vitu vinavyoweza kuwaka haraka ni pamoja na dawa za wadudu, vimiminika vyenye asili ya maji au mvuke, mafuta ya kujipaka, kupikia na taa, tochi zinazotumia gesi, mishumaa, vifaa vya kuwashia sigara, viberiti, rangi, vipengezo. 


 Kemikali mfu na vimiminika

Kemikali hizo ni pamoja na dawa za kusafishia maji, mitungi midogo ya gesi, mitungi ya kuzimia moto, gesi ya machozi, mitungi ya kupulizia rangi, sabuni za kufuria na kuogea na betri isipokuwa zinazotumiwa kwenye viti vya kubebea wagonjwa.

Vimiminika vingine ni kama maji, mafuta ya kujipaka, losheni, pafyumu vyenye ujazo wa zaidi ya mililita mia moja (100mls) haviruhusiwi kwenye mzigo wa mkononi. 

“Kimiminika chochote kilichozidi mililita 100 kinaruhusiwa kusafiri tu endapo kitawekwa kwenye mzigo mkubwa utakaokwenda kwenye “hold” ambao abiria atapewa mwisho wa safari yake,” anaeleza Majaliwa.


Vifaa vyenye ncha kali

Mfano wa vitu hivyo ni visu, nyembe, sindano, mikasi. Lakini unaweza kuviweka pamoja na vikakaguliwa na ikiwa vitakidhi vigezo vya usalama vitafungwa vizuri na kuhifadhiwa sehemu salama ili kujihami kabla havijaleta madhara.


Vifaa vya michezo

Mipira inayotumika kwenye mchezo mbalimbali ikiwemo ya magongo, pete, kriketi, fimbo za mchezo wa gofu, barafu, mezani (Mipira hii inaweza kuruhusiwa ikiwa imepata kibali cha ukaguzi lakini sio kwenye viwanja vyote). Baadhi ya malighafi zinazotumika kutengenezea vifaa vya michezo nazo haviruhusiwi kutegemeana na masharti ya ndege husika.


 Silaha

Silaha za kawaida ambazo hutumika kwa matumizi binafsi haziruhusiwi isipokuwa kama mtu amefuata taratibu za kumiliki silaha za nchi husika na ameripoti kwenye mamlaka ya ndege. Silaha hiyo itahifadhiwa sehemu maalum kwenye ndege na abiria atakabidhiwa mwisho wa safari.

Silaha za moto, vita, vifaa vya kutengenezea silaha kama risasi, vyuma, unga, vilipuzi, viwashaji na vitu vingine vinavyodhaniwa ni silaha ambavyo vinaweza kuleta madhara kwa abiria haviruhusiwi ndani ya ndege.


 Zana za kijeshi na Vifaa vya ulinzi binafsi

Fimbo fupi au vigongo, seti ya kadi zinazotumika kwenye kamali, kombati za mikononi na miguuni, vifaa vya kubebea funguo, gesi inayotumika kutuliza fujo, silaha za kijeshi, fimbo zilizounganishwa na vyuma, silaha yenye umbo la nyota yenye ncha kali na vifaa vya kutetemesha mwili.

“Baadhi ya vitu vinavyokatazwa kwenye ndege ni kwasababu vina viashiria vya kuhatarisha usalama na vinaweza kuwadhuru abiria na wafanyakazi wa ndege,” inaeleza sehemu ya mwongozo wa usalama wa TAA.

Wateja wanashauriwa kuwasiliana au kufanya utafiti wa mashirika ya ndege wanayosafiria na nchi wanazokwenda ili kufahamu kwa kina mizigo wanayoruhusiwa kubeba  ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea.

Mwongozo wa TAA unaeleza kuwa, “Kila ndege inajiendesha kwa taratibu zake za mizigo ambazo zinaonyesha vitu usivyoweza kubeba au kuweka kwenye mizigo inayokaguliwa. Abiria wanashauriwa kuangalia vitu visivyoruhusiwa kabla ya hawajakata tiketi ya ndege, ili kuwasaidia kupita kwenye ukaguzi wa usalama wa uwanja wa ndege  kwa haraka na ufanisi kadri inavyowezekana.”


Inayohusiana: Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’


Vitu unavyoruhisiwa kuvibeba 

Kulingana na Shirika la Kimataifa la Viwanja vya Ndege (ICAO) ambalo linafanya kazi kwa karibu na Mamlaka za viwanja vya ndege vya kila nchi ikiwemo Tanzania limeorodhesha baadhi ya vitu ambavyo abiria anaweza kuingia navyo kwenye ndege. 

Mashine zinazotumika kupaka make-up usoni

Hizi ni zile zinazotumiwa na wanawake kuongeza urembo na mvuto kwenye nyuso zao.


Vinywaji baridi (Pombe)

Pombe inayoruhusiwa ni ile yenye zaidi ya asilimia 24 lakini sio zaidi ya asilimia 70 ya kilevi na unaruhusiwa kubeba kinywaji cha lita tano tu na kinatakiwa kiwe wazi kwenye chombo maalum. Vinywaji vyenye kilevi ambacho kina asilimia chini ya asilimia 24 kinaruhusiwa kupita kwenye mabegi ya ukaguzi.

Chupa ndogo za vinywaji hivyo zinatakiwa kuwekwa vizuri kwenye begi moja ili visitingishike na kupasuka. Lakini kila nchi ina taratibu zake za aina na uzito wa pombe anayoweza kutumia msafiri wa ndege.


Seti ya pembe za wanyama

Unaweza kusafiri nazo kwenye begi la mkononi au mzigo mkubwa utakaokwenda kwenye “hold” ambao abiria atapewa mwisho wa safari yake. Hata hivyo, lazima ufuate taratibu zote za maliasili za nchi husika ikiwa ni moja ya njia ya kukabiliana na ujangili.

 

Fuvu la mifupa bandia

Mara nyingi mifupa bandia hutumiwa na watu waliopata ajali au majeraha katika miili yao ili kuhakikisha wanatembea na kufanya shughuli zao kama kawaida.

Pia unaruhusiwa kubeba nguo, viatu, mablanketi na mkanda. Vitu vingine ni darubini, mashine ndogo za kuchanganya matunda na viuongo (inaruhusiwa kama imeondolewa meno ya kusagia), mashine ya kupima kiwango cha sukari mwilini, pini za kubania nywele, tufe, mkate uliokaushwa, kamera na stendi yake. 

TAA inasisitiza kuwa wasafiri wa ndege wanapaswa kufuatilia mara kwa mara mabadiliko ya taratibu za usalama ikiwemo vitu vinavyoruhusiwa na visivyoruhusiwa. Pia wanapaswa kuwasiliana na mashirika ya ndege wanayosafiria ili kuhakikisha hawapati usumbufu wakati wote wa safari. 

Taarifa za ndege zitakusaidia kufahamu bei na uzito wa mzigo ambao utalipia ikiwa umezidisha kiwango kinachohitajika.

“Mfano mashirika mengine huruhusu abiria kubeba hadi kilo 20 bila malipo ya ziada na kuna mashirika mengine ambayo hutoza kwa kila mzigo abiria anaobeba kwa kila safari,” anafafanua Majaliwa kutoka TCAA.

Tahadhari nyingine ni kuwa usipokee mzigo wa mtu yeyote kwa madhumuni ya kuusafirisha, hata kama anamfahamu mtu huyo. Inawezekana abiria akapewa madawa ya kulevya, nyara za serikali au kitu chochote kinachokatazwa bila yeye kujua na mwisho wa siku akaingia matatizoni.

Enable Notifications OK No thanks