Tanzania, Uganda sasa kukamilisha mikataba ya bomba la mafuta mapema 2019

December 8, 2018 6:03 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Waziri wa Uganda amesema mabadiliko ya muundo wa kifedha katikati ya safari yamechangia kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo mkubwa.
  • Serikali hizo mbili zinatarajia kuwa taratibu na mikataba yote muhimu kuhusu mradi huo itakamilika katika robo ya kwanza ya mwaka 2019.
  • Kalemani aeleza kuwa yapo mambo ya msingi yanayotakiwa kukamilishwa kabla ya kuutekeleza mradi huo.
  • Atoa hofu kuwa mradi haujasimama na tayari maandalizi ya awali ya tafiti muhimu yamekamilika.

Dar es Salaam. Serikali za Tanzania na Uganda zimekubaliana kuharakisha mchakato wa kukamilisha mikataba yote muhimu itakayofanikisha ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Tanga baada ya sehemu ya mipango ya awali kushindwa kutekelezwa kwa wakati.

Mawaziri wanaoshughulikia nishati kutoka katika nchi hizo mbili leo (Desemba 7, 2018) walifanya  mkutano maalum Jijini hapa na wataalam wao uliolenga kutatua baadhi ya changamoto zilizojitokeza na kufanya mataifa hayo kutokamilisha baadhi ya mikataba muhimu ya uwekezaji ya kufanikisha ujenzi wa bomba hilo.

Hadi sasa nchi hizo zinazoshirikiana katika mradi wa bomba hilo la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) lenye urefu wa kilomita 1,443, hazijasaini mikataba ya kiuwekezaji (Host Government Agreements, HGA) na wawekezaji ambayo awali ilitarajiwa kuwa imesainiwa mwishoni mwa mwaka huu.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema wamekubaliana kuharakisha kukamilisha masuala yote muhimu ambayo hayajakamilika ili kuruhusu kusainiwa kwa HGAs na kwamba vikao vinavyofuata kukamilisha masuala hayo vitafanyika katika wiki ya tatu ya Januari 2019 nchini Uganda.

Katika majadiliano hayo, Dk Kalemani amesema wamekubaliana kwamba kila nchi itahakikisha inasimamia kwa nguvu zake zote ili mradi uanze kutekelezwa kwa haraka iwezekanavyo. 

“Tulipanga uanze kutekelezwa mwaka huu lakini yapo mambo ya msingi sana ya kupitia kabla ya kuingia kuanza kuutekeleza, hayo ndiyo tunakamilisha,” amesema Dk Kalemani.

Dk Kalemani ameeleza kuwa mradi huo unapaswa kuwa na manufaa kwa pande zote mbili zinazohusika wakati wa utekelezaji wake kwa kuwa sehemu kubwa ya mradi huu inachukua sehemu ya Tanzania.

Kati ya kilomita 1,445 za bomba hilo, kilomita 1,149 zipo Tanzania ikiwa ni zaidi ya robo tatu ya mradi huo likipitia katika mikoa minane na wilaya 24.

“Lipo jukumu la kila aina la kuchukua tahadhari za kutosha kuhakikisha mradi huu unakuwa na manufaa kwa Watanzania,” amesema.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani akizungumza na wanahabari leo baada ya kumaliza mkutano na Serikali uliokuwa ukijadili mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga. Picha|Wizara ya Nishati.

Kalemani amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo haujasimama na “kimsingi ndiyo tunaanza kwa spidi kubwa kuutekeleza ili ukamilike kama tulivyopanga”.

Kwa sasa, ameeleza kuwa upande wa Tanzania wamekamilisha maandalizi ya utafiti wa kijiolojia na kijiofizikia na wanaendelea na uchimbaji wa mashimo ambapo wameshamaliza Tanga, Manyara na sasa wapo wilayani Kondoa mkoani Dodoma.

“Kwa hiyo hatua za awali za utekelezaji zimeshaanza hivyo tathmini  zote za mazingira, fidia na ustawi wa jamii zimekamilika na hatua inayofuata ni kuingia katika utekelezaji baada ya majadiliano kukamilika,” amesema Kalemani ambaye alikuwa Mwenyekiti mwenza katika mkutano huo uliomalizika leo.

Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni amesema kuwa wanatarajia taratibu na mikataba muhimu yote na wawekezaji itakuwa imekamilishwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2019.

Muloni amesema kuwa mpango wa awali wa kusafirisha mafuta ya kwanza mwaka 2020 “upo hatarini” baada ya wawekezaji kuchelewa kufanya maamuzi ya mwisho (Final Investment Decision) ya kiuwekezaji katika bomba hilo linalotarajia kugharimu Dola za Marekani 3.5 bilioni sawa na zaidi ya Sh8 trilioni. 

Mradi huo unatekelezwa na kampuni za mafuta za Total, Tullow Oil, Shirika la Taifa la Mafuta la China (CNOOC) kwa ubia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Mafuta la Uganda (UNOC). 

“Tulitarajia kampuni zinazowekeza katika mradi huu wangefanya maamuzi ya mwisho ya uwekezaji mwishoni mwa mwaka jana hivyo ujenzi wa mradi ungeanza kujengwa mwaka huu na ifikapo mwishoni mwa mwaka 2020 bomba lingekuwa limekamilika,” amesema Muloni na kuongeza;

“Lakini hadi sasa tunavyozungumza sasa hawajafanya maamuzi hayo.”


Zinazohusiana: 


Muloni ameeleza kuwa baada ya mazungumzo na wawekezaji hao, Serikali ya Uganda iliamua kuchagua njia ya Hoima-Tanga kwa kuwa njia hiyo ilikuwa ya gharama nafuu kwa kuwa ilikuwa haigharimu zaidi ya Dola za Marekani 12.2 kwa pipa moja la mafuta ghafi katika usafirishaji.

“Hayo ndiyo yalikuwa makubaliano yetu lakini katikati ya safari wakati tukikamilisha masuala muhimu , muundo wa biashara na kifedha (financial model) ulileta mambo mengine ambayo yalikuwa yanaenda mbali zaidi ya tulivyokubaliana ndiyo maana tumechelewa kutekeleza mradi,” amesema.

Ili “wasonge mbele”, Muloni amesema iliilazimu Serikali ya Uganda ambayo ndiyo chanzo cha mafuta kuwasiliana wawekezaji hao juu ya matarajio yao kutoka katika mradi huo unaotarajia kuongeza uwekezaji wa kigeni kwa asilimia 60 kwa Tanzania na Uganda.

“Sasa inabidi tuhuishe makubaliano yetu na Tanzania ili kuhakikisha kila nchi inaingia mkataba na wawekezaji na kuanza kutekeleza mradi mapema iwezekanavyo,” amesema Muloni.

Enable Notifications OK No thanks