Matumaini waliyobeba wanafunzi bora Tanzania

January 5, 2019 10:37 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wale waliotamba katika mitihani ya kidato cha nne na sita wakichukua masomo ya sayansi.
  • Licha ya hadhi walizonazo katika jamii wamechagua kuishi maisha ya kawaida wakiamini katika utu na siyo vitu.
  • Wanaamini nguvu ya ubunifu, nidhamu, mawasiliano na mtandao wa watu ndiyo nguzo muhimu kwa mtu kupata mafanikio.

Dar es Salaam. Imekuwa ni utaratibu wa kawaida kwa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutangaza ya wanafunzi waliofanya vyema kitaifa katika mitihani yao kuanzia darasa la saba hadi kidato cha sita kila mwaka.

Katika kila aina ya mtihani wa kitaifa, Necta humtambua mwanafunzi bora aliyefanya vizuri katika masomo yake, kwa lugha ya mtaani vijana wanapenda kumwita “Tanzania One” au “TO”.  

Swali la kujiuliza ni kuwa mafanikio ya kielimu wanayopata wanafunzi hao yanadumu na kuendelea hata baada ya kumaliza masomo?

Je, bado wanadhihirisha umahiri wao wa kufanya vizuri katika maeneo mengine ya kazi, maisha au hata kwenye familia? Je matokeo hayo katika masomo yanatafsiri uwezo wao na ubunifu katika maisha?

Nukta inakuletea majibu ya maswali hayo baada ya kufanya uchumbuzi na mahojiano ya baadhi ya wanafunzi bora waliotamba na kusikika kwenye vyombo vya habari miaka ya nyuma kutokana na uwezo waliouonyesha katika masomo ya kuhitimu elimu ya sekondari na nafasi walizonazo katika jamii.

Mnamo mwaka 1988, Veronica Sarungi kutoka shule ya sekondari ya Zanaki ya jijini Dar es Salaam alishika nafasi ya kwanza kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne katika masomo ya sayansi.

Veronica ni mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Prof Philemon Sarungi katika awamu ya tatu iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Lakini amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo kuwa Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Kwa sasa, Veronica ambaye nini dada wa Mwanaharakati na mwanzilishi wa kampeni ya mtandaoni ya  “ChangeTanzania”, Maria Sarungi, ni Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Aga Khan aliyebobea kufundisha somo la hisabati chini ya taasisi ya Kuendeleza Elimu Afrika Mashariki (IED).

Licha ya hadhi aliyonayo amechagua kuishi maisha ya kawaida akiamini kuwa binadamu wote ni sawa na kinachowaunganisha ni utu na sio nafasi walizonazo katika jamii.

“Baba yangu alikuwa ni mtu kawaida sana, kama mama yangu alikuwa anatuambia yaani nyie mko kama watu wa kawaida na mimi nashukuru miaka ile ya 1980 tulibahatika sana. Kwa mfano, pale shule ya msingi Osterbay tulisoma na mtoto wa Jaji Mkuu yaani hakuna ubaguzi kama kulima tunalima wote kwenye shamba la shule,” anasema Veronica.

Miaka 10 baadaye, mwaka 1998 akaibuka msichana mwingine Khadija Mkocha kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Francis ya mkoani Mbeya na kuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne akijikita katika masomo ya sayansi.

Mkocha ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyebobea katika fani ya Umeme na Uhandisi wa Mawasiliano Pepe. Yeye alikataa kuwa daktari wa magonjwa ya binadamu na kuvunja kasumba ya jamii ya mtoto kusomea kile wanachotaka wazazi.

“Tangu nilipokuwa mtoto mdogo sikupenda kuwa daktari japokuwa wazazi wangu wote walikuwa madaktari…” anasema Khadija.

Lakini anaamini katika nguvu ya ubunifu, nidhamu, mawasiliano na mtandao wa watu ili mtu afanikiwe katika maisha.

Yapo mengi yaliyofichika kuhusiana na wawili hawa ambao walifanya vizuri katika mitihani yao ya kidato cha nne na sita. Katika mfululizo wa makala hizi utafahamu kwa undani kuwa “TO” wakati huo ilikuwa ina maana gani katika jamii, lakini pia matumaini waliyobeba watanzania hawa katika jamii inayowazunguka.

Makala ijayo itaangazia safari ya Veronica Sarungi kwa undani.

Enable Notifications OK No thanks