Kutana na ‘TO’ aliyekataa udaktari na kukimbilia fani ya uhandisi umeme

January 8, 2019 2:19 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mwanafunzi bora kitaifa mtihani wa kidato cha nne mwaka 1998/1999. 
  • Alikataa kuwa daktari wa binadamu kwa sababu hakutaka kusomea fani ya wazazi wake.
  • Ndoto yake ilianza kutimia alipopata fursa ya kuingia ndani ya kichwa cha treni wakati huo akiwa darasa la tano.
  • Anaamini nguvu ya mafanikio inajengwa na ubunifu, nidhamu, kutunza muda na kujenga mtandao wa marafiki.

Dar es Salaam. “Tangu nilipokuwa mtoto mdogo sikupenda kuwa daktari japokuwa wazazi wangu wote walikuwa madaktari na sikupenda walipokuwa wakienda kazini usiku wanapokuwa na zamu za usiku.”

Hayo ni maneno ya Khadija Mkocha, mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 1998/1999 (Walifutiwa matokeo ya mtihani waliofanya mwaka 1998 na walifanya tena mtihani wa
kidato cha nne Januari, 1999). 

Kwa sasa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Idara ya  Umeme na Uhandisi wa Mawasiliano Pepe (Electronics and Telecommunications Engineering). 

Tangu akiwa mdogo aliamua kuishi ndoto zake na kuachana na hulka iliyojengeka katika jamii kwa wazazi kuwapangia watoto wao kusomea fani wanazofanyia kazi.

Anasema wazazi wake ambao kitaaluma ni madaktari wa binadamu hawakuwa na jinsi zaidi ya kukubali uamuzi wake ambapo hakupenda kuwa daktari tangu akiwa mdogo.

Licha ya wazazi kukubali maamuzi yake, jamii iliyomzunguka haikumuelewa kwa sababu waliamini angefuata nyayo za wazazi wake lakini yeye alishikiria msimamo wake na kuukataa udaktari kwa sababu kwa nyakati fulani fani hiyo ilimnyima muda wa kukaa na familia yake.

“Changamoto kubwa niliyoipata, hasa baada ya kumaliza kidato cha nne ni pale ambapo watu wengi walionizunguka hawakuelewa ni kwa nini sikuwa na nia ya kusomea udaktari wa binadamu, ukizingatia kuwa wazazi wangu wote wawili ni madaktari,” anasema Khadija. 

Mwaka 1992 wakati yuko darasa la tano katika shule ya msingi Azimio mkoani Mbeya, ndoto yake ya kuwa mhandisi ilianza kuchomoza alipopata nafasi ya kuingia kwenye kichwa cha treni cha karakana ya shirika la reli la Tazara (Tanzania and Zambia Raiway Authority) iliyopo mkoani Mbeya.

Hapo alikutana na mtaalamu wa umeme kutoka Sierra Leone aliyekuwa na ukaribu na wazazi wa Khadija ambao walikuwa wanaishi katika nyumba za wafanyakazi wa Tazara. 

“Siku moja alituchukua na kutupandisha katika kichwa cha treni. Siku hiyo nilifanya uamuzi kuwa nitakuja kuwa Mhandisi! Nilipofika kidato cha sita nilishajua ningependa kubobea zaidi katika electronics (Umeme),” anasema Khadija.

Khadija Mkocha akiwa katika moja ya majukumu yake ya kufundisha. Picha|Frickr.

Baada ya kukamilisha masomo ya kidato cha sita katika shule ya sekondari wa wasichana ya Msalato ya jijini Dodoma mwaka 2001 alijiunga na chuo cha UDSM katika kilichokuwa kitivo cha uhandisi na kusomea shahada ya Mawasiliano Pepe ambapo alihitimu mwaka 2005.

Miaka miwili baadaye aliajiriwa chuoni hapo na mpaka sasa ni Mhadhiri Msaidizi ambaye bado anasaka elimu zaidi ya shahada ya Uzamivu (PhD in Telecommunications Engineering). 


 Pamoja na kufaulu vizuri hakujiamini

Siku ya kupata matokeo yake ya kidato cha nne, Khadija alibubujikwa na machozi kuashiria furaha aliyokuwa nayo katika kutimiza ndoto zake za kuwa mhandisi wa umeme. 

Wakati huo  wasichana wachache walikuwa wanaingia kwenye fani ya sayansi kwa sababu masomo hayo yalikuwa yakidhaniwa ni ya wanaume pekee yao.


Zinazohusiana:


Hata wakati akisubiri kwenda kidato cha tano, Khadija hakuliona jina lake miongoni mwanafunzi waliochaguliwa kujiunga katika shule mbalimbali licha ya kufanya vizuri katika masomo yake.

“Baada ya kupata matokeo, tulikuwa tukisubiri kujua tumepangiwa shule gani. Kati ya wanafunzi 39 tuliomaliza pamoja kidato cha nne, 26 walipangiwa shule mbalimbali lakini 13, mimi nikiwemo tulitafuta sana majina yetu bila mafanikio. 

“Tuliingiwa na wasiwasi sana. Kumbe sisi 13 tulikuwa tumepangiwa kwenda Msalato, shule ya wenye vipaji maalumu. Hii ilikuwa kinyume na hofu tuliyopata. Pamoja na kuwa tulifaulu vizuri, hatukujiamini kabisa,” anasema.


“Una uwezo gani? Unapenda nini? Unataka kwenda wapi? Baada ya hapo, ni kujua je, katika mazingira uliyopo, ni nini unachoweza kufanya kitakachokusogeza karibu zaidi na kutimiza malengo yako?” – Khadija Mkocha.


Nidhamu na kutunza muda vimempaisha zaidi

Anaamini malezi na nidhamu aliyofunzwa na wazazi wake tangu akiwa mdogo imechangia kwa sehemu kubwa katika mafanikio yake. 

“Nimelelewa na wazazi wenye nidhamu lakini walioheshimu mawazo yangu na chaguo langu tangu nikiwa mtoto mdogo,” anasema Khadija  na kuongeza,

“Shuleni nilipata kujifunza kupanga na kutumia vizuri muda, pamoja na umuhimu wa kutunza mawasiliano na maelewano na wale tunaokuwa nao wakati wote.” 

Mbali na taaluma aliyonayo, anajishughulisha na mambo mengine ya kijamii ikiwemo kufanya ibada na kujumuika na vijana wenye mawazo ya kibunifu kutengeneza bidhaa za mikono.

“Ninasoma sana vitabu vinavyohusu mambo ninayotaka kuyafanya, yaani nikisoma kitabu hujaribu kutumia kile nilichokisoma. Zaidi ya haya, pia hupenda kupika na kutengeneza hand crafts (bidhaa za mkono), nikisaidiana na wanangu. Tunapika keki na kuwauzia majirani,” anasema Khadija.

Mhadhiri huyo anawakumbusha vijana wenye ndoto za kufanikiwa katika maisha kuweka bidii katika kila wanalolifanya.

“Usizime ndoto zako. Fanya ibada kwa dhati na weka bidii katika kila unalofanya huku ukisimamia uamuzi wako, utafika!,” anasema. 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV