Makonda aagiza kamera, taa za usalama kufungwa kwenye maduka Dar

January 8, 2019 5:52 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Taa na kamera za usalama zitawasaidia wafanyabiashara wa jiji la Dar es Salaam kufanya shughuli zao hadi nyakati za usiku ili kuongeza wigo wa mapato. Picha| colourbox.com


  • Hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango wa kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao mchana na usiku.
  • Wafanyabiashara nao watakiwa kufunga kamera za ‘CCTV’ kuimarisha usalama katika maduka yao.
  • Huenda mpango huo ukachochea uzalishaji, biashara na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Dar es Salaam. Huenda shughuli za uzalishaji, biashara na ukusanyaji mapato zikaongezeka katika Jiji la Dar es Salaam, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaaam, Paul Makonda kutangaza nia ya kufunga kamera na taa za usalama kwenye maduka ili wafanyabiashara wafanye shughuli zao kwa saa 24. 

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kiongozi huyo kutangaza mpango wa kuziruhusu baa kutoa huduma za vinywaji kwa saa 24, kinyume na utaratibu uliopo sasa ambapo shughuli hizo zimekuwa zikifungwa saa 6:00 usiku. 

Makonda aliyekuwa akizungumza na Wanahabari leo (Januari 8, 2019) jijini hapa amesema sambamba na hilo wafanyabiashara wanatakiwa kuanza kufunga kamera (CCTV Camera) katika maduka yao ili kuimarisha usalama nyakati za usiku.  

“Zipo changamoto ambazo tunahangaika nazo kuzitatua, mojawapo ni kuwa na security rights (taa za usalama) kwenye maduka lakini pia wafanyabiashara tunawasihi wafunge kamera,” amesema Makonda.


Zinazohusiana: 


Pia uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam unakusudia kukutana na wafanyabiashara kuangalia namna ya kutekeleza mpango huo kwa ufanisi utaochochea shughuli za uzalishaji, biashara ya bidhaa na kuiongezea Serikali wigo wa kukusanya mapato. 

“Sio muda mrefu tutakutana na wafanyabiashara wote wenye maduka, wenye shopping malls (Maduka makubwa) na wenye baa ambapo tutakubaliana kwa pamoja na uhakika hautazidi mwezi wa pili kutakuwa na tamko kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa ni ya usiku na mchana,” amesema.

Biashara ya bidhaa katika jiji hilo inachochewa zaidi na uwepo wa viwanda, soko, la Kariakoo na bandari ya Dar es Salaam ambayo inafanya kazi usiku na mchana, jambo linalohitaji mikakati ya kuongeza muda wa kufanya kazi wa taasisi zingine za biashara. 

Bandari hiyo imekuwa kiunganishi muhimu cha usafirishaji wa mizigo inayoingia na kutoka katika nchi za jirani za Congo DRC, Zambia, Uganda, Rwanda na Burundi kupitia reli ya kati na Tazara na mtandao wa barabara uliounganishwa nchi nzima. 

Enable Notifications OK No thanks