TTCL yavunja rekodi watumiaji wa simu baada ya ‘kudumaa’ kwa miaka nane

January 29, 2019 2:05 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeongeza watumiaji wa huduma za simu hadi kufikia asilimia mbili Desemba 2018 kutoka asilimia moja iliyodumu kwa miaka nane iliyopita
  • Bado ina kibarua kigumu cha kuhimili ushindani kutoka kwa kampuni kubwa kama Vodacom, Tigo na Airtel ambazo zinashikilia soko la mawasiliano.

 Dar es Salaam. Hatimaye Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) imevunja rekodi ya miaka nane ya ongezeko la watumiaji wa simu wa mtandao huo, jambo linaloonyesha dalili ya kuibuka tena baada ya kudumaa katika kiwango cha umiliki wa soko kwa muda mrefu sasa.

Takwimu za mawasiliano zilizotolewa hivi karibuni na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa hadi Desemba 2018 Tanzania ilikuwa na watumiaji wa simu za mkononi kwa (voice telecom services) milioni 43.6 huku TTCL ikiwa na watumiaji wanaofikia 711,411 sawa na asilimia mbili ya watumiaji wote.

Ongezeko hilo pia la watumiaji wa TTCL ni karibu mara mbili ya watumiaji 429,735 waliokuwepo mwaka 2017 na mara tatu zaidi ya waliokuwa wakitumia mtandao huo mwaka 2016.

Kiwango hicho cha umiliki wa soko ni cha juu kuwahi kufikiwa na TTCL ndani ya miaka nane jambo linaloonyesha matumaini mapya kwa kampuni hiyo ya umma katika kuchochea ushindani katika sekta ya mawasiliano nchini. 

Ukuaji wa umiliki wa soko wa kampuni hiyo ulikuwa umedumaa ukicheza ndani ya asilimia moja tangu mwaka 2010.

Mara ya mwisho, TTCL kuwa na kiwango kikubwa cha umiliki wa soko la mawasiliano Tanzania ilikuwa mwaka 2009 ambapo ilikuwa na watumiaji 273,019 sawa na asilimia mbili ya watumiaji wote wa simu katika kipindi hicho. 

Miaka uliyofuata watumiaji walikuwa wakipungua hadi kufikia Desemba 2013, kampuni hiyo ilikuwa na watumiaji 210,766. 

Katika kipindi hicho muamko wa watumiaji wa simu za mezani ulipungua wakati idadi ya watumiaji wa simu za mkononi ikiongezeka kwa kasi huku kampuni za Tigo, Vodacom, Zantel, Airtel, Smart na Halotel zikijiongezea wateja na kuacha kampuni ya simu ya umma ikiwa nyuma. 

Lakini haikuwa mwisho wa TTCL, ilikusanya nguvu zake na idadi ya wateja ikaanza kuongezeka taratibu mpaka ilipotoka asilimia moja ya miaka nane na kufikia asilimia mbili mwaka 2018. 

Hata hivyo, TTCL bado ina kibarua kigumu  cha kuhimili ushindani na kuongeza idadi ya watumiaji ikizingatiwa kuwa kampuni ya Vodacom ndiyo inaongoza katika soko la mawasiliano ikifuatiwa na Tigo na  Airtel. 

Wakati kampuni hizo zikichuana katika soko, Serikali nayo imeendelea kuwatengenezea mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kuboresha huduma za mawasiliano vijijini ili kuyapa fursa kampuni hayo kuwafikia watu wengi zaidi.


Zinahusiana:


Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka 2018/2019, Waziri wa wakati huo Prof. Makame Mbarawa alisema Serikali iliingia mkataba na kampuni ya simu ya Viettel ya nchini Vietnam kufikisha mawasiliano ya simu vijijini mwaka 2014. 

Kupitia makubaliano hayo, Viattel maarufu kama Halotel ilipewa wajibu wa kufikisha mawasiliano katika vijiji 4,000 nchini. 

“Hadi mwezi Machi, 2018 Viettel walijenga minara na kufikisha mawasiliano ya simu katika vijiji 3,712 ambapo vijiji 288 vilivyosalia vinatarajiwa kupata huduma ya mawasiliano mwaka 2018/2019,” alisema Prof. Mbarawa.

Rais John Magufuli akionyesha mfano wa hundi ya Sh1.5 bilioni iliyotolewa na TTCL ikiwa ni gawio kwa Serikali baada ya kupata faida ya Sh28.5. Tukio hilo lilifanyika Januari 2018. Picha| Mtandao.

TTCL inafanya nini kushindana sokoni?

Licha ya kwamba TTCL imepiga hatua kidogo bado menejimenti ya kampuni hiyo watakuwa na kibarua kigumu katika kukuza idadi ya watumiaji wa huduma mbalimbali za simu zikiwemo intaneti, huduma za kifedha na sauti baada ya kampuni kubwa tatu za Vodacom, Tigo na Airtel kuchukua sehemu kubwa ya soko.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba ameiambia www.nukta.co.tz kuwa wanaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kuikuza kampuni hiyo ikiwemo kusogeza huduma kwa wananchi na kuongeza uwekezaji wa teknolojia, matangazo na utendaji wa ndani ili kuwafikia watu wengi hasa vijijini. 

“Tumejitahidi kwenda kwa wananchi na kujitangaza mkoa kwa mkoa tukawaeleza faida za kutumia huduma za TTCL,” amesema Kindamba.

Juni 2016, TTCL ilipata nguvu zaidi baada ya kampuni ya Bharti Airtel ya India kuingia makubaliano na Serikali ya kuachia hisa zao za asilimia 35 walizokuwa wakimiliki katika kampuni hiyo na imilikiwe na Serikali kwa asilimia 100.

Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa TTCL, Nicodemus Mushi amesema wameelekeza nguvu katika uwekezaji wa  kituo cha data na kutumia vizuri fursa ya kuunganisha wizara na taasisi za Serikali na usimamizi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) ili kuendelea kutoa ushindani kwa kampuni zingine.

“Kwa fursa hizi zinatupa nafasi ya kuongoza katika soko kwa maana ya viwango, gharama vyote tukiweka vizuri inaonyesha kabisa tuna nafasi ya kukua kwa haraka kwenda kutoa ushindani,” amesema Mushi.

Januari 2018 TTCL ilitoa gawio la Sh1.5 bilioni kwa Serikali baada ya kupata faida ya Sh28.5 bilioni mwaka 2017.

Enable Notifications OK No thanks