Unayafahamu majukumu aliyonayo mwekezaji kwenye ‘startups’?
- Mwekezaji anatakiwa akuunganishe na watu mbalimbali ili uweze kukuza soko la biashara yako.
- Mwekezaji mbali na fedha zake anapaswa atoe msaada kwako na sio kukutawala wewe au kampuni yako.
- Hakikisha unatoa ripoti mara kwa mara kwa mwekezaji wako ili akupe msaada pale unaposhindwa kujiendeleza.
Kwa waanzilishi wengi wa kampuni changa moja ya masuala yanayoumiza vichwa ni kutafuta mitaji kutoka kwa wawekezaji ambao fedha zao huchangia kwa kiwango kikubwa kulifanya wazo kuwa biashara kubwa, inayoishi na kutoa mchango unaotakiwa kwa jamii.
Hata hivyo, kama wewe ni mwanzilishi wa kampuni na unayesaka mtaji kukuza biashara uliwahi kujiuliza mwekezaji anapaswa kufanya nini baada ya kuweka fedha zake?
Karibu kwenye mwendelezo wa makala ya jinsi ya kuongeza mtaji katika kampuni zinazochipukia (Startups) ambapo leo tunaangalia majukumu ya mwekezaji katika kuongeza mtaji wa kampuni.
Mtaalam wa masuala ya uwekezaji na ujasiriamali, Eric Osiakwan kutoka kampuni ya Chanzo Capital ya nchini Ghana anaendelea kukujuza zaidi kuhusu uwekezaji kwenye kampuni zinazochipukia maarufu kwa Kiingereza ‘Startups’.
Osiakwan, aliyekuwa ziarani jijini Dar es Salaam hivi karibuni, anawashauri wajasiriamali waliowekeza katika teknolojia kutafakari na kufahamu kwa undani aina ya mwekezaji wanayemuhitaji katika kampuni zao.
Hata hivyo mwekezaji ana majukumu mengi zaidi ya kutoa mtaji tu kuwekeza pesa zake na hapa tutaziona kazi hizo kwa upana wake.
Kutoa mtaji
Lengo la mwekezaji anayekupata mtaji wa fedha au ujuzi ni kuona biashara yako inakua ili na yeye apate faida.
Osiakwan anashauri kuwa ili upate mtaji kutoka kwa mwekezaji hakikisha angalau una uwezo wa kuzalisha angalau nusu ya kiasi unachomuomba ili kujenga uaminifu na matumaini ya kuendelea kukusaidia.
“Kama hujawahi kuingiza Sh500,000 huwezi kumpata mwekezaji atakayekupa 1,000,000,” amesema Osiakwan.
Siku zote mjasiriamali lazima akumbuke anawajibu pia wa kusaka maarifa yatakayomsaidia kuongeza ufanisi wa kazi yake. Picha| Zahara Tunda.
Anakuletea uzoefu wake
Wawekezaji wengi ni watu ambao wanakuwa na uzoefu wa muda mrefu katika eneo wanalokuja kuwekeza hivyo kama anawekeza katika biashara yako jipange kutumia vizuri maarifa na ujuzi utakaopewa kulingana na mazingira yanayokuzunguka.
Mtaalam huyo, ambaye pia ni mwekezaji barani Afrika, anasema mwekezaji ana nafasi kubwa ya kuua au kuinua kampuni yako ni vema kumsoma vizuri mwekezaji wako hasa katika eneo la uzoefu, ujuzi na uelewa wa jambo analowekeza.
Anakufungulia milango ya kujuana na watu wengine
Mwekezaji halisi atakufungulia milango ya kufahamiana na watu mbalimbali ambao watakusaidia kwa namna moja au nyingine.
Hivyo kipindi unatafuta mwekezaji jiulize kama ana uwezo wa kukufungulia njia ya kukutanisha na wateja wengine ambao wanaweza kusaidia biashara yako kukua zaidi.
Kama hawezi kukusaidia katika hilo inabidi utafakari njia nyingine utakazotumia kupata fursa ya kukutana na watu wenye ujuzi.
Zinazohusiana:
- ‘Startups’ zinavyoweza kuondokana na dhana potofu ya upatikanaji wa mitaji
- Utambulisho, uwekezaji kuzibeba ‘Startups’ Tanzania
Mwekezaji anatakiwa amuweke mjasiriamali kwanza
Osiakwan anabainisha kuwa mwekezaji anatakiwa amuweke mjasiriamali mbele, hii inamaanisha kuwa asitumie kampuni yako kujinufaisha au kujitangaza bali akupe nafasi ya kuonekana na kukujengea misingi mizuri ya kukua.
Kama mwekezaji atakuwa anataka kujiweka yeye mbele kwa kila kitu fahamu kuwa hakufai na anaweza kukuletea shida hapo baadaye.
Mwekezaji anatakiwa akusaidie sio kukutawala
Kama wewe ni mjasiriamali wa kampuni inayochipukia kumbuka kuwa mwekezaji anatakiwa kukusaidia na sio kukutawala katika uendeshaji wa wa kampuni yako.
“Kumbuka kumpa ripoti mwekezaji wako ili aweze kukusaidia mahali ulipokwama,” anasema Osiakwan
Ukimpa mwekezaji nafasi ya kukutawala basi unakuwa umeondoa dhana ya uwekezaji. Jifunze kutenganisha nafasi ya mwekezaji na mwanzilishi wa startup.
Latest