Maoni: Tunaweza kuwapatia furaha Watanzania wengi zaidi kwa nishati jadidifu

February 14, 2019 12:15 pm · Charles
Share
Tweet
Copy Link
  • Kuna Watanzania wengi wanahitaji nishati endelevu na ya bei nafuu katika kukuza biashara zao na maisha yao ya kila siku.
  • Mmoja wa kina mama aliyejifungua mtoto akiwa kwenye zahanati yenyea umeme kwa mara ya kwanza wilayani Tunduru aliamua kumpatia mwanaye mchanga jina la ‘Solar’ kutimiliza furaha yake. 
  • Malengo ya Serikali ya kuwafikishia umeme Watanzania wote kwa asilimia 100 mwaka 2030 hayatafikiwa kirahisi iwapo hakutakuwa na uwekezaji wa kutosha katika nishati jadidifu. 

Katika kufanya shughuli zangu za kuwapelekea wananchi wa vijijini huduma ya umeme, yapo mambo mengi ya kukumbukwa ya namna ambavyo nishati hiyo inavyoweza kubadilisha maisha ya watu.

Lakini tukio lililotokea mwaka 2011 katika Kijiji cha Marumba, wilayani Tunduru, litabakia katika kumbukumbu zangu daima.

Mwaka huo kupitia mradi uliofadhiliwa na Benki ya Dunia, na kusimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wa ‘Lighting Rural Tanzania’ (LRTC 2010), tulizipatia zahanati 40 mkoani Ruvuma umeme kwa teknolojia ya Umemejua (Stand Alone Solar) ikiwa ni mara ya kwanza taasisi hizo za kiafya kupata huduma hiyo. 

Kati ya zahanati hizo 40, zahanati 20 zinatoka katika Wilaya ya Tunduru na zilizosalia zilikuwa wilayani Mbinga.

Kabla ya hapo huduma za maabara hazikuwa nzuri kutokana na kukosekana umeme wa kuwezesha kufanya vipimo vya kitabibu. Matibabu ya dharura usiku yalikuwa nadra kufanyika kutokana na ukosefu wa mwanga.

Hata hivyo, baada ya kuanza kutoa huduma hiyo, Zahanati hizo zilianza kutoa huduma kwa saa 24 kutokana na kuwepo kwa mwanga wa uhakika utokanao na umeme wa jua pamoja na kufanya vipimo vidogo vidogo (basic diagnosis) vya magonjwa kwa kuwepo umeme kwenye maabara.

Wahudumu wa afya walipatiwa taa za mkononi za umemejua maarufu kwa kiingereza ‘solar’ zilizokuwa na uwezo wa kuchaji simu hivyo kuboresha mazingira yao ya kazi. Mradi pia ulitoa mafunzo kwa mafundi sanifu 10 kwa kila wilaya kwa ajili ya kuendeleza teknolojia ya umemejua na kushughulikia matatizo yote ya kiufundi kwenye mifumo iliyosambazwa.

Moja ya nguzo za umeme katika Kijiji cha Ketumbeine wilayani Longido, Arusha inayotumika kusambaza umeme wa mradi mdogo wa umemejua (Solar minigrid). Wakazi wa eneo hili wamepunguziwa gharama za kufanya biashara na maisha kupitia nishati jadidifu. Picha| K15 Photos.

Katika hali tusiyoitarajia, baada ya mama kujifungua kukiwa na mwanga wa umeme katika zahanati ya Marumba wilayani Tunduru waliamua kumuita mtoto wao aliyezaliwa “SOLAR” kuonyesha furaha na kuridhika kwao kwa kuboreshwa kwa huduma ya afya kwenye zahanati yao.

Furaha hiyo huenda ilikuwa mara mbili yaani ya kujifungua mtoto akiwa salama lakini akiwa ni miongoni mwa kina mama wa kwanza kupatiwa huduma baada kuwepo umeme.

Kuna Watanzania wengi wanahitaji furaha kama aliyoipata mama Solar lakini kwa kuwa tu hawana nishati ya uhakika ya umeme wamejikuta wakishindwa kutumia ipasavyo fursa za kiuchumi zilizowazunguka na kukosa huduma bora za kijamii ikiwemo afya.

Uwekezaji madhubuti kama uliofanywa katika mradi huo wa Mbinga na Tunduru unaweza kuchagiza kwa kiwango kikubwa maendeleo nchini na kutoa tabasamu kwa kila mmoja wetu.

Hadi mwaka 2018, Serikali inakadiria kuwa zaidi ya asilimia 40 ya Watanzania walikuwa wamefikiwa na huduma ya umeme ikiwa ni ukuaji wa mara nne zaidi kutoka asilimia 10 iliyokuwepo mwaka 2010.

Kwa vijijini, kulikuwa na asilimia moja tu ya watu waliofikiwa na huduma ya umeme mwaka 2008 yaani sawa na kusema ni mtu mmoja tu kati ya 100 alikuwa akipata nishati hiyo. 

Hata hivyo, kwa sasa mambo ni tofauti baada ya watumiaji umeme maeneo ya vijijini kuongezeka mara 12 kwa makadirio ya mwaka 2018, kwa mujibu wa Wizara ya Nishati.

Pamoja na mafanikio hayo, bado tuna kazi kubwa ya kufanya kufikia Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Sustainable Development Goals, SDG) hapo mwaka 2030 ambapo watu wetu wote wanatakiwa wawe wamefikiwa na huduma ya nishati (Universal Access to Clean Energy).


Soma zaidi: 


Katika mpango mkuu wa nishati vijijini wa mwaka 2017 (Rural Energy Master Plan, 2017) Serikali imejiwekea malengo ya kuwa na asilimia 75 au robo tatu ya watu waliofikiwa na huduma ya umeme hapo mwaka 2022 na kuwafikia wote kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.

Pamoja na kuwa na malengo madogo ya kuwa na asilimia tano pekee ya mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji na matumizi ya jumla ya nishati kitaifa (Total Energy Mix) ifikapo mwaka 2040, bado nina uhakika kuwa teknolojia za nishati jadidifu zitatoa mchango mkubwa katika kutuwezesha kufikia malengo haya tuliyojiwekea na kuchagiza maendeleo ya Taifa katika nyanja zote za maisha.

Prosper Magali ni Mtaalamu wa Nishati Jadidifu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 17, ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Nishati Jadidifu (Tanzania Renewable Energy Association) na mmoja wa wakurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa ya Alliance for Rural Electrification yenye Makao yake Makuu Brussels, Ubelgiji na pia Mkurugenzi wa Miradi na Ubunifu wa Kampuni ya Ensol Tanzania Ltd, waendelezaji miradi ya nishati jadidifu wa hapa Tanzania. Makala hii ni maoni yake binafsi.

Enable Notifications OK No thanks