Majaliwa aingilia kati hospitali za Aga Khan ‘kutopokea’ kadi za NHIF
- Ameitaka hospitali ya Aga Khan wakamilishe majadiliano na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili watumiaji wa bima za mfuko huo watibiwe katika hospitali za Aga Khan.
- Hospitali hiyo imesema haijakataa kupokea kadi za bima za NHIF bali inatoa huduma hiyo kwa wagonjwa walio wabunge.
- Inaangalia uwezekano wa kuwajumuisha wagonjwa wengine wasio wabunge.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) kukamilisha majadiliano na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuwapa fursa watumiaji wa bima za mfuko huo kutibiwa katika hospitali za Aga Khan.
Majaliwa ametoa agizo hilo jana (Mei 28, 2019) alipokutana na viongozi wa taasisi ya AKDN pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma.
Machi mwaka huu Mkurugenzi wa Tiba na Afya wa hospitali ya Aga Khan, Dk Ahmed Jusabani alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa hospitali hiyo ilikuwa inapokea kadi za bima za NHIF lakini mwaka 2012 walisitisha kupokea kadi hizo kutokana na matatizo yaliyojitokeza.
Lakini kwa sasa hospitali hiyo inapokea kadi za wagonjwa walio wabunge na inaendelea na majadiliano na NHIF ili kuwajumuisha watumiaji wengine wasio wabunge.
“Katika hospitali ya Aga Khan ya Dar es Salaam tunawapokea wabunge, mazungumzo ya bodi yanaendelea yataeleza ni jinsi gani tunaweza kuwapokea na wagonjwa wa kawaida na siyo wabunge pekee,” alisema Dk Jusabani, Machi 5, 2019 wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la hospitali hiyo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema jana Serikali inatambua mchango unaotolewa na taasisi ya AKDN katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya nchini.
“Nilijionea kazi kubwa inayofanyika pale Hospitali ya Aga Khan Machi, mwaka huu, niliongea na wagonjwa na kupata maoni yao, lakini kikubwa tu mpunguze gharama na muimarishe huduma zenu,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongoza mazungumzo kati yake, na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (wa pili kushoto) pamoja na Viongozi wa Taasisi ya Aga Khan, Ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Mei 28, 2019. Picha||Ofisi ya Waziri Mkuu.
Viongozi hao walikutana na Waziri Mkuu ili kumuarifu juu ya mpango wa taasisi hiyo wa kuanzisha kituo maalum cha matibabu ya saratani nchini (Specialised Cancer Care Facility) ambao unatarajiwa kugharimu dola za Marekani 15 milioni (Sh34.46 bilioni).
Kituo hicho kitaendeshwa kwa ubia baina ya hospitali za Ocean Road, hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Bugando na Aga Khan.
Akitoa maelezo kuhusu mpango wa kujenga kituo hicho, Mwakilishi Mkazi wa AKDN, Amin Kurji, amesema wameshawasiliana na hospitali zote tajwa na sasa wanashirikiana na wataalamu wa wizara ya afya ili kukamilisha suala hilo.
“Tatizo la saratani hapa nchini ni kubwa kwa sasa. Lakini tunataka watu watambue kwamba ukiugua saratani haimaanishi kwamba utakufa mara moja. Inaweza kutibika endapo mgonjwa atawahi kupata matibabu,” amesema Kurji.
Zinazohusiana:
Amebainisha kuwa kwa sasa hivi hapa nchini hakuna kituo maalum cha matibabu ya saratani lakini kituo hicho kitatoa huduma zinazotembea za upimaji na utoaji tiba hadi mikoani.
“Huduma hizi zitakuwa zinatolewa kwenye mikoa yote kupitia njia ya mtandao, ilhali vituo vikuu vya Dar es Salaam na Mwanza vitakuwa vikitoa majibu kwa madaktari husika,” amesema.