Waziri azungumzia ndege za ATCL kuchelewa, kuahirisha safari

May 30, 2019 9:03 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

ATCL imefanya maboresho makubwa katika ndege zake jambo linaloongeza ushindani katika usafiri wa anga Tanzania. Picha|Mtandao.


  • Amesema hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali za kiufundi katika menejimeti ya Shirika la Ndege la Tanzania.
  • Amesema wameanza kurekebisha tatizo hilo kwa kutoa taarifa ya maandishi kama ndege imechelewa zaidi ya nusu saa.
  • ATCL waagizwa kuwathamini wateja wake kwa kuwapa huduma bora.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema marekebisho ya kiufundi yameanza kufanyika katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuondoa tatizo la changamoto ya kuchelewa na kuahirishwa kwa safari za ndege, jambo ambalo limekuwa likiwaletea usumbufu watumiaji wa ndege za shirika hilo.

Mhandisi Nditiye ametoa ufanunuzi huo bungeni leo (Mei 30, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye aliyetaka kujua chanzo cha tatizo la ndege za ATCL kuchelewa na kuahirisha safari mara kwa mara na Serikali inafanya nini kurekebisha tatizo hilo. 

“Sasa hivi marekebisho yameshaanza kufanyika, ATCL wameanza kwenda vizuri, zile delay (kuchelewa) zimepungua sana na zile cancellation (kuahirisha) zisizo za msingi zimekuwa hazitokei tena,” amesema Mhandisi Nditiye. 

Amesema ziko sababu mbalimbali zinazosababisha ndege kuchelewa au kuahirisha ikiwemo sababu za kiufundi ambazo sasa zimerekebishwa na kupunguza tatizo lililokuwepo awali.  

“Ni kweli katika siku za hapa karibuni kumetokea uchelewaji au cancellation kwa shirika letu la ndege Tanzania, lakini Mheshimiwa Spika hili linatokana na sababu mbalimbali za kiufundi ambazo zimerekebishwa,” amesema.


Soma zaidi:


Amesema wizara yake imeanzisha utaratibu unaoitaka ATCL na menejimenti yake kutoa taarifa ya maandishi endapo ndege itachelewa kwa zaidi ya nusu saa na tayari agizo hilo limeanza kufanyiwa kazi. 

Hata hivyo, Mhandisi Nditiye amesema ATCL inapaswa kuwathamini wateja wake kwa kuwapa huduma bora na kuhakikisha wanawasafirisha kwa muda uliopangwa na kuachana na sababu zisizo za msingi za kuahirisha safari.  

“Tunaendelea kuwasisitiza ATCL kwamba wateja ndiyo wathamani sana kwahiyo delay (kuchelewa) zozote ambazo hazina sababu ya msingi ziepukwe sana,” amesisitiza.  

Katika swali lake, Nape amesema pamoja na kutambua jitihada za Serikali kuboresha mawasiliano na uchukuzi hasa katika maboresho yaliyofanyika katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), sasa hivi kumeanza tatizo la ucheleweshaji wa ndege kila mara watu wanaposafiri. 

“Hili jambo linakera sana. Chanzo cha tatizo hili ni nini? Na Serikali inachukua hatua gani kulirekebisha?” amehoji Nape.

Enable Notifications OK No thanks