Serikali kuanza kununua mahindi kutoka kwa wakulima wiki hii
- Imesema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) wataanza kununua zao hilo.
- Rwanda na Burundi waonyesha ni ya kununua tani 200,000 za mahindi.
Dar es Salaam. Serikali imesema itaanza kununua mahindi kutoka kwa wakulima kuanzia wiki huku ikiainisha kuwa tayari hatua za kusaka masoko nje ya nchi zimeanza kuzaa matunda baada ya Rwanda na Burundi kuonyesha nia ya kununua tani 200,000 za zao hilo.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amelieleza Bunge leo wakati wa maswali na majibu kuwa ununuzi huo wa mahindi unaonza juma hili utafanywa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).
Kauli hiyo Hasunga imekuja baada ya Mbunge wa Viti Maalumu Aida Khenani kuuza Serikali imejipangaje na ununuzi wa mahindi katika kipindi hiki cha mavuno.
Hata hivyo, Hasunga hakuweka bayana bei ambayo Serikali itanunua mahindi hayo kwa kilo kutoka kwa wakulima.
Mbali na kununua zao hilo, amesema Serikali imepata masoko makubwa ya mahindi katika nchi za kusini mwa Afrika na kwamba Rwanda na Burundi wanauhitaji wa tani 100,000 kila mmoja huku nchi ya Zibwabwe iIkihitaji tani laki 800,000 za mahindi na nchi nyingine.
Zinazohusiana:Tanzania yatajwa nchi zinazotegemea kuuza bidhaa ghafi duniani
“Soko sasa la mahindi ni kubwa sana wakulima wote wenye mahindi tunaomba wajitokeze na watuambie wana kiasi gani washirikiane na Serikali. Kuanzia wiki hii tasisi zetu ikiwemo NFRA na CPB wanaza kununua mahindi na kukusanya mahindi kutoka kwa wakulima mbali pomaja na wafanyabishara,” amesema Hasunga.
Pia amesema taasisi waliyoipa jukumu ya kupeleka mahindi nchini Zimbabwe nayo inaanza kununua mahindi wiki hii.
“Kwa hiyo wakulima wakae mkao wa kula kila mahali…wenye mahindi sasa hivi ni wakati wakula mkate mzuri,” amesema Waziri Hasunga.
Wakulima nchini wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa masoko ya mazao yao jambo linalowafanya wauze kwa bei za chini ambazo wakati mwingine huwa hazisadifu gharama halisi za uzalishaji.
Oktoba mwaka jana wakulima wa korosho waligomea kuuza zao hilo kwa bei ya chini na kuilazimu Serikali kuingilia kati kwa kuamua kununua kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo ili kuwanusuru wakulima hao na bei ndogo.
Wiki iliyopita Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kuwa bei ya chini ya pamba kwa kilo moja mwaka huu itakuwa ni Sh1,200 ili kuwaokoa na bei ndogo ambazo zingezidi kuwaumiza wakulima nchini.