Umaskini wa kaya Tanzania washuka-Ripoti
Licha ya kuwa umaskini vijijini bado uko juu lakini unapungua ambapo mwaka 2011/2012 ulikuwa asilimia 33.4. Hali ni tofauti na maeneo ya mjini ambapo umaskini unaongezeka. Picha|Mtandao.
- Ripoti mpya ya mapato na matumizi katika kaya inaonyesha umaskini wa mahitaji muhimu umepungua kutoka asilmia 28.2 mwaka 2011-2012 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017-2018.
- Kwa wastani kila Mtanzania anatumia Sh49,320 kwa mwezi kujipatia mahitaji muhimu.
- Mkoa wa Rukwa ndiyo unaoongoza kuwa na kaya nyingi zenye umaskini wa mahitaji muhimu kwa asilimia 45.
- Serikali yasema ripoti hiyo ni kioo katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya mapato na matumizi katika kaya inaonyesha umaskini wa mahitaji muhimu katika kaya za Tanzania Bara umeshuka kwa asilimia 1.8 ndani ya kipindi cha miaka saba iliyopita huku mkoa wa Rukwa ukiongozwa kwa kiwango kikubwa cha kaya zenye umaskini.
Pia umaskini wa chakula umepungua kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia nane katika kipindi hicho.
Ripoti hiyo, iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwishoni mwa wiki iliyopita, inaonyesha kuwa umaskini wa mahitaji muhimu umepungua kutoka asilmia 28.2 mwaka 2011-2012 hadi asimia 26.4 mwaka 2017-2018.
Hiyo ni sawa na kusema kuwa robo au kaya 26 kati ya 100 zilizopo Tanzania Bara zinaishi na umaskini wa mahitaji muhimu ikilinganishwa na kaya 28 kati ya 100 mwaka 2011/2012.
Kiwango hicho cha umaskini kiko chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji muhimu wa kitaifa ambapo kwa wastani kila Mtanzania mtu mzima anatumia Sh94,997 kwa mwezi.
Wakati umaskini katika kaya kitaifa ukipungua, ripoti hiyo inaeleza kuwa hali ya umaskini katika maeneo ya vijijini iko juu kwa asilimia 31.3 ukilinganisha na maeneo ya mjini ambayo ni asilimia 15.8.
Licha ya kuwa umaskini vijijini bado uko juu lakini unapungua ambapo mwaka 2011/2012 ulikuwa asilimia 33.4. Hali ni tofauti na maeneo ya mjini ambapo umaskini unaongezeka.
Mwaka 2011/2012 ulikuwa asilimia 15.4 lakini umeongezeka hadi kufikia asilimia 15.8 mwaka 2018.
Soma zaidi: Siku ya umaskini duniani yageuzwa kuwa siku ya Vicoba Tanzania
Katika mpangilio wa kimkoa, mkoa wa Rukwa ndiyo una kiwango kikubwa cha kaya zenye umaskini kwa asilimia 45 ukifuatiwa na Simiyu (asilimia 39.2) huku Dar es Salaam ukirekodiwa kuwa na kiwango cha chini kabisa cha kaya zenye umaskini kwa asilimia nane pekee.
Utafiti huo wa mapato na matumizi katika kaya ulianza kufanyika tangu mwaka 1991/1992 ili kupata taarifa muhimu za umaskini na hatua zilizopigwa kuboresha maisha ya Watanzania.
Lakini pia hutumika kufuatilia na kutathmini malengo ya maendeleo ikiwemo Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2016/2017 hadi 2020/2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizindua ripoti hiyo jijini Dodoma, alisema takwimu bora hutoa fursa kwa Serikali kufanya mapitio ya sera, mipango na mikakati kulingana na hali ilivyo kwa wakati husika na pia kupima ilikotoka, ilipo na kutabiri inakoelekea hivyo kupima mwenendo wa jitihada za Serikali.
“Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli, inatambua umuhimu wa takwimu zenye ubora, kwa kuwa ndiyo macho na masikio ya Serikali katika kufuatilia na kutathmini mipango ya maendeleo ya nchi”, alisema Majaliwa.