Majaliwa:Vijana acheni tabia ya kuchagua kazi
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua maadhimisho wiki ya Vijana kitaifa kwenye viwanja vya Mpilipili mjini Lindi, Oktoba10, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Amesema vijana wanapaswa kujishughulisha na kazi zote za uzalishaji kama moja ya kujikwamua kimaisha.
- Azindua mradi wa kitaifa wa mafunzo ya ujenzi na kilimo cha kisasa kwa vijana.
Dar es salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka vijana waondokane na dhana ya kuwa kazi bora ni zile za kukaa ofisini, bali wafanye kazi za uzalishaji mali ili kukuza vipato vyao.
Waziri mkuu amezindua mradi wa kitaifa wa mafunzo ya ujenzi na kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalunyumba (greenhouse) kwenye viwanja vya maonesho vya Ngongo, jana jioni (Oktoba 10, 2019) mjini Lindi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa kwa mwaka 2019.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza jana jioni (Oktoba 10, 2019) katika maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa kwa mwaka 2019 inayofanyika mkoani Lindi, amesema vijana wanapaswa kujishughulisha na kazi zote za uzalishaji kama moja ya nafasi iliyotolewa na Serikali kupitia fursa waliyoianzisha kwa vijana.
“Nataka vijana muondokane na dhana ya kwamba kuwa na ajira ni lazima uwe umekaa mezani na umeshika kalamu. Ajira ni kazi yoyote ya halali inayompatia mtu kipato iwe ni biashara ndogondogo, mama lishe au bodaboda,” amesema Majaliwa.
Aidha, Majaliwa amezindua mradi wa kitaifa wa mafunzo ya ujenzi na kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalunyumba (greenhouse) ambayo inaweza kuwasaidia vijana waliojiajiri katika sekta ya kilimo.
“Maeneo mengi nchini hayana mvua za kutosha. Kwa hiyo tumeanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya matone na siyo kwa kuchimba mifereji. Kitalunyumba kinahitaji nafasi chini ya robo eka, na humo ndani kuna matuta manne tu. Kwa kutumia tenki la maji, unatumia maji kidogo sana kwa kila mche, kwa sbabu yanatoka kwa matone,” amesema Majaliwa.
Zinazohusiana:
- Majaliwa awataka vijana kujitokeza kwa wingi uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura
- Majaliwa awatoa hofu wakulima, wanunuzi wa pamba
Septemba 2019, vijana 8,700 kutoka katika Halmashauri 83 za mikoa 12 wamepatiwa mafunzo ya ujenzi na kilimo ndani ya kitalunyumba.
Mikoa hiyo ni Mwanza, Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Geita, Mbeya, Lindi, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Kagera na Simiyu huku maandalizi ya kutoa mafunzo kwa vijana kutoka katika Halmashauri 102 zilizobaki za mikoa 14 yamekamilika, na yataanza kutolewa kabla ya Novemba, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema Serikali ilifanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 56 ya nguvukazi nchini ni vijana lakini wanakabiliwa na changamoto ya kukosa ajira, hivyo kuja na suluhu hiyo ya kuwapatia vijana fursa ya kupata ajira.
“Katika utafiti mwingine wa Serikali, tulibaini kuwa kundi kubwa la vijana linaajiri na kuajiriwa lakini pia vijana hawa wanakosa ujuzi unaotambulika rasmi ndiyo tukaja na mkakati wa Taifa wa uwezeshaji wa vijana kwa kuboresha mazingira na kuwapa stadi na ujuzi mbalimbali” amesema.