Marekani, Uingereza zavutana matumizi ya mtandao wa 5G

January 29, 2020 7:11 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Uingereza umeiruhusu kampuni ya China ya Huawei kujenga miundombinu ya mtandao wa intaneti wa 5G.
  • Marekani yasema hatua hiyo itahatarisha usalama wa taifa na mahusiano ya kibiashara. 
  • 5G ni mtandao wa intaneti wenye kasi ya juu katika kupakua na kutuma vitu mtandaoni. 

Uingereza imetoa idhini ya ushiriki mdogo wa kampuni ya China ya Huawei katika ujenzi wa miundombinu ya mtandao wa intaneti wa 5G, jambo linaloweza kudhorotesha mahusiano yake ya kibiashara na usalama na nchi ya Marekani.

5G ni muendelezo wa mifumo ya intaneti inayotumiwa kuwezesha mawasiliano duniani kwa viwango vya juu zaidi ikilinganishwa na mifumo iliyotangulia ya 2G, 3G na 4G. 

G kwenye tarakimu hizo inawakilisha ‘Generation’, yaani kizazi fulani cha teknolojia ya mawasiliano kwa kuangazia zaidi uwezo wa data kwenye simu.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, uamuzi huo wa Uingereza unafuatia mkutano wa Baraza la Kitaifa la Usalama lililoongozwa na Waziri Mkuu Boris Johnson, na kubainisha kuwa hakuna kitisho chochote cha usalama ikiwa Huawei itapewa kazi hiyo. 

Mkutano huo umefanyika baada ya Umoja wa Ulaya (EU) kusema utairuhusu Huawei kuwa na jukumu dogo la kufunga miundombinu ya mtandao wa 5G katika umoja huo. 

Lakini EU imesisitiza kuwa, huenda wachuuzi ambao wamekuwa wakionyesha hatari ya kiusalama kwa Huawei kupewa jukumu hilo, wanaweza kutengwa katika utengenezaji wa miundombinu ya msingi ya mradi huo. ‘

Waziri wa masuala ya kidijitali wa Uingereza, Nicky Morgan amesema kuwa taifa hilo linataka uunganishaji wa kisasa na haraka iwezekanavyo wa 5G, lakini hilo halitaathiri usalama wa taifa, akimaanisha mtandao huo  wenye kasi kubwa zaidi utawezesha uhamishaji wa data mara moja.

Unaelezwa kuwa ni mtandao wa kuaminika na kutegemewa katika simu za mkononi kutokana na urahisi katika kuunganisha vifaa vingi vya kielektroniki kwa wakati mmoja (Internet of Things-IoT) ambavyo ni vifaa vinavyotuma data kwenda katika mtandao bila kuhusisha binadamu kwa binadamu au binadamu na kompyuta. Picha|Mtandao.

Marekani na Uingereza katika mvutano

Uamuzi wa Uingereza kuiruhusu Huawei  kusimika miundombinu ya mtandao wa 5G unafuatia mjadala wa miezi kadhaa juu ya maoni ya Marekani kuwa kampuni hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa taifa na China kuitumia kampuni hiyo kudukua taarifa muhimu za nchi hiyo.

Kampuni za simu nchini Uingereza zitakuwa na uwezo wa kutumia vifaa vya Huawei katika mitandao yao ya 5G lakini kampuni hiyo haitahusishwa katika maeneo muhimu ya usalama mtandaoni. 

Rais wa Marekani, Donald Trump, mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuzuiwa kwa bidhaa za Huawei, akidai kuwa China inatumia vifaa vya kampuni hiyo kudukua na kuingilia mawasiliano ya watu wake. 

Kwa mujibu wa sheria za China, kampuni za nchi hiyo zinaweza kufanya kazi yoyote inayoamriwa na Serikali. Lakini Huawei imekuwa ikikataa kuwa haiwezi kuisadia Serikali ya China kufanya udukuzi.

Huawei iko nchini Uingereza kwa muda mrefu sasa ikitoa huduma ya intaneti isiyo ya waya (wireless network) na inafanya kazi kwa uangalizi wa karibu wa mashirika ya usalama ya nchi hiyo tangu mwaka 2003.

Kwa mujibu wa kampuni ya Dell’Oro ya Marekani, Huawei inaongoza katika kumiliki soko la vifaa vya simu duniani kwa asilimia 28. Nokia inashika nafasi ya pili kwa asilimia 16 na Ericson nafasi ya tatu (asilimia 13). 

Soko kubwa la Huawei liko Ulaya na tayari imepigwa marufuku kuuza vifaa vyake Marekani. 


Soma zaidi: 


Mtandao wa 5G ni nini? 

Tume ya Mawasiliano ya Ulaya inakadiria kwamba kati ya mwaka 2020 na 2030, mtandao wa 5G utaweza kupakua filamu moja ya HD ya saa moja kwa sekunde sita pekee.

Kwa mujibu wa kampuni ya Samsung, Mtandao huo wa  5G utakuwezesha kupakua GB moja kwa sekunde (1GB/Sec) lakini inakadiriwa kupakua GB 10 kwa sekunde na baadaye itakuwa na uwezo wa kupakua GB 800 kwa sekunde.

5G ni njia rahisi na ya haraka ya kupakua na kuweka vitu mtandaoni. Utaweza kuangalia video na kusikia sauti yenye kiwango kizuri pasipo kukwama kwama kwa video au sauti hizo kwenye simu au kompyuta yako.   

Itapanua uwanja wa matumizi ya teknolojia hasa kwa wale wanaotumia mtandao kuendesha vyombo vya usafiri katika miji mikubwa duniani.

Unaelezwa kuwa ni mtandao wa kuaminika na kutegemewa katika simu za mkononi kutokana na urahisi katika kuunganisha vifaa vingi vya kielektroniki kwa wakati mmoja (Internet of Things-IoT) ambavyo ni vifaa vinavyotuma data kwenda katika mtandao bila kuhusisha binadamu kwa binadamu au binadamu na kompyuta.

Teknolojia ya 5G inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwaka huu wa 2020 duniani kote, huku nchi kama Marekani, China na Korea ya Kusini na Uingereza zinatarajiwa kuwa za kwanza kutumia mfumo huo katika nchi zao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW