Maeneo ya uwekezaji yanayoweza kukuongezea kipato

January 30, 2020 9:07 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wekeza katika ujenzi wa majengo ya ofisi au nyumba za kuishi watu.
  • Unaweza kuanzisha kampuni, biashara au kuingia ubia na marafiki.
  • Kwa kila uwekezaji, fanya utafiti kwanza kabla ya kuweka pesa zako.

Umuhimu wa maisha unakuja pale unapotimiza kusudi lako la kuishi duniani. Lakini haitakuwa na maana kutimiza kusudi kama hatujawekeza katika kuboresha hali za maisha yetu ikiwemo kuwa na afya bora na kupata kipato kizuri cha kukidhi mahitaji ya familia.

Licha ya kuwa tunatakiwa kutengeneza kipato na kuweka akiba, bado tunatakiwa kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kutuongezea kipato zaidi. 

Uwekezaji wa fedha zako ambazo umeweka akiba au unazipata kila mwezi utakua una maana kama hauna madeni makubwa au mahitaji ya muhimu ambayo huwezi kuishi bila kuyatimiza. 

Kama bado unafikiri utafanyia nini pesa ambazo umehifadhi kwenye kibubu chako, haya ndiyo maeneo ambayo unaweza kuwekeza na kukupatia kipato zaidi:

Wekeza katika ujenzi wa majengo ya biashara au nyumba za kuishi. Katika aina hii ya uwekezaji, unaweza kutafuta ardhi na ukajenga ofisi au maduka ambayo utayapangisha kwa watu na kila mwezi ukajipatia kodi kutoka kwa wapangaji. 

Kama hiyo haitoshi, jenga nyumba za kuishi na zipangishe kwa watu. Uwekezaji wa majengo ni mzuri kwa sababu nyumba zinadumu na zinaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali, licha ya kuwa inaweza kuchakua muda mrefu kurejesha gharama na kupata faida iliyokusudiwa. 


Zinazohusiana: 


Biashara au kufungua kampuni ya kuuza bidhaa au kutoa huduma inaweza kuwa njia nyingine ya matumizi sahihi ya akiba ua kipato chako. Angalia katika eneo ulilopo, watu wanahitaji nini zaidi ili uwape. 

Mathalani, kama unaishi eneo lenye muingiliano wa watu wengi, unaweza kufungua mgahawa na kutoa huduma ya chakula. Hii itasaidia kutoa ajira kwa watu ambao watakusaidia kukamilisha malengo uliyojiwekea. 

Pia unaweza ukaingia ubia na marafiki au watu wenye ujuzi fulani kwenye jamii ambao ukiwekewa mazingira mazuri ya uwekezaji unaweza kuzalisha kipato. 

Unaweza kuweka pesa zako kwa biashara iliyokosa mtaji kwa nia kuzalisha faida ambayo mtagawana na wahusika kulingana na makubaliano yenu. 

Wekeza katika kujiendeleza katika elimu. Kama unafikiri kuna uhitaji wa kujiendeleza kielimu ili kupata maarifa na ujuzi ambao unaweza kukusaidia hapo baadaye kukuongezea kipato katika kazi au biashara yako, basi fanya hivyo. 

Usiogope kujielimisha na kupata maarifa mapya kwa fedha zako mwenyewe. Unaweza kutoa fedha zako kusoma kozi za muda mfupi au masomo ya ziada ambayo hayaingiliani na ratiba za kazi zako huku ukiwa na malengo ya kufika sehemu fulani. 

Hakikisha kile unachosomea kwa wakati huo, kitaongeza thamani katika maisha yako na kukupeleka katika ngazi ya juu ya mafanikio yako. 

Wekeza katika ujenzi wa majengo ya biashara au nyumba za kuishi. Katika aina hii ya uwekezaji, unaweza kutafuta ardhi na ukajenga ofisi au maduka ambayo utayapangisha kwa watu na kila mwezi ukajipatia kodi kutoka kwa wapangaji. Picha|Tierra Mallorca/Unsplash.

Ikiwa hataki mihangaiko ya kufungua biashara, unaweza kununua hisa au hati fungani za kampuni za kibiashara. Faida za kununua hisa ni kutajirika kwa njia ya kupata gawio kila mwaka, baada ya kampuni husika kupata faida na kugawa faida kwa wanahisa wake.

Wakati huo huo mnunuzi wa hisa anapata faida ya kuwa sehemu ya wamiliki wa kampuni hiyo na kupata faida kutoka katika fedha aliyowekeza bila yeye kuhangaika kufanya kazi.

Hizi ni baadhi ya njia unazoweza kuzitumia kuwekeza fedha zako. Muhimu, fanya utafiti kwanza wa faida na hasara ya aina ya uwekezaji unaofanya ili kujiweka katika nafasi ya kufanikiwa zaidi kuliko kupoteza fedha zako. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW