Uber yafyeka wafanyakazi wengine 3,000

May 19, 2020 6:12 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Uamuzi huo ni kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni hiyo.
  • Biashara ya usafiri ya kampuni hiyo imeporomoka kwa asilimia 80 japo matumaini ya kurejea kwenye reli yameanza kuonekana,
  • Bolt ambaye ni mpinzani wa Uber hana mpango wa kufuta mtu yeyote kazi.

Dar es Salaam. Kampuni ya usafiri wa mtandaoni ya Uber imepunguza  wafanyakazi wengine 3,000 duniani ikiwa ni hatua iliyochukua kukabiliana na makali ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19).

Kampuni hiyo yenye makao makuu nchini Marekani imekuwa msaada kwa watu wanaoishi katika majiji makubwa kupata usafiri wa taxi, bajaj na bodaboda kwa kutumia simu zao za mkononi. 

Mapema mwezi Mei, wafanyakazi 3,700 wa kampuni hiyo ulimwenguni walipoteza kazi zao na sasa wafanyakazi wengine 3, 000 nao wanaondolewa kwa kile kinachodaiwa ni kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni hiyo. 

Muendelezo wa kufyeka ajira za wafanyakazi hao umepitiliza kiwango ambacho kilitolewa hapo awali ambapo mpango mkakati wa kampuni hiyo uliweka wazi kupunguza wafanyakazi 5,400. 

Kwa mujibu wa tovuti ya The Verge, hadi sasa wafanyakazi 6,700 kati ya wafanyakazi 27,000 wenye ajira ya kudumu wamepoteza kazi zao. 

Aidha, maamuzi hayo huenda yamechochewa na hasara ya Sh67.14 trilioni ambayo kampuni hiyo imepata katika robo ya kwanza ya mwaka 2020 huku ikiwa ni hasara kubwa kuwahi kutokea kwenye robo tatu zilizopita.

Siyo jambo la kushangaza kwani Uber imeripoti anguko la asilimia 80 kwenye biashara yake ya usafiri na Mkurugenzi Mtendanji wa kampuni hiyo Dara Khosrowshahi, ameweka wazi katika maongezi yake na wawekezaji wa kampuni hiyo kuwa “sitoipamba kwa sukari. Covid-19 ina athari kubwa katika biashara ya usafiri ya Uber.”


Zinazohusiana


Hata hivyo, Khosrowshahi amesema kwa kipindi cha wiki tatu zilizopita, wameanza kupata ongezeko la matumizi ya usafiri wake na hivyo huenda ikawa ni taa ya kijani ya kampuni hiyo kurudi kwenye reli yake.

Hali inayoisumbua Uber, imekuwa ni tofauti kwa mpinzani wake yaani Bolt (hapo mwanzo Taxify) ambapo kampuni hiyo licha ya kuona makali ya Covid-19, imesema haitopunguza wafanyakazi.

Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Bolt Markus Villig katika mahojiano yake na shirika la habari la CNBC amesema kammpuni hiyo yenye wafanyakazi 1,400 kote ulimwenguni, haitafuta mtu yeyote kazi kwani imekuwa ni kampuni ya kubana matumizi tangu awali.

Villig amesema mbali na kuwapumzisha baadhi ya wafanyakazi wake kwa kipindi kifupi ambapo watarejea kazini hali ikiwa shwari.

Kampuni hiyo yenye makao makuu yake nchini Estonia inapanga kuendelea kuboresha huduma zingine zinazotolewa na kampuni hiyo zikiwemo usambazaji wa chakula.

“Hatuna mpango wa kufuta watu kazi,” amesema Villig.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW