Tanzania, Burundi zilivyojipanga kufanya biashara ya madini
- Zinakusudia kujenga mtambo wa pamoja cha uchenjuaji wa madini ya nickel.
- Tanzania kuishawishi Burundi kuuza baadhi ya madini yake kwenye vituo vya kuuzia madini vilivyopo mkoani Kigoma.
- Pia watajenga reli ya Uvinza Msongati hadi Kitega (Burundi) ili kuwezesha usafirishaji wa mizigo na madini.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali inafanya mazungumzo na nchi ya Burundi ya kujenga mtambo wa pamoja wa uchenjuaji wa madini ya nickel na kuishawishi nchi hiyo ikubali kutumia vituo vya madini vilivyopo katika mkoa wa Kigoma kuuza madini yake ili kuimarisha biashara na uchumi wa nchi hizo mbili.
Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo Septemba 19, 2020 wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya Rais wa Burundi, Èvariste Ndayishimiye mkoani Kigoma, amesema mazungumzo kuhusu suala hilo yanafanyika na matokeo yatatolewa baadaye.
“Lakini katika suala madini, leo tutazungumzia suala la kuruhusu nchi ya Burundi, baadhi ya madini yake kama dhahabu na kadharika yawe yanakuja kuuziwa hapa Kigoma.
“Bahati nzuri, sisi Tanzania tumefungua maduka ya madini, badala ya wenzetu Burundi kuhangaika kupeleka mahali pengine, leo tutakuja kuzungumza nao ili tuwaombe kama watakavyokubaliana kadiri tutakavyokuwa tunazungumza kwamba walitumie soko la madini la hapa Kigoma katika kufanya biashara,” amesema Rais.
Kwa sasa, Tanzania imejenga vituo vya kuuzia madini katika maeneo yote nchini yenye migodi ya madini, ikiwa ni hatua ya kurahisisha biashara hiyo.
Katika mazungumzo hayo pia Rais Magufuli na mgeni wake watazungumzia uwezekano wa kujenga mtambo wa pamoja wa kuchenjua madini ya nickel ili kuwezesha madini hayo yanayopatikana katika nchi zote mbili kuchakatwa vizuri kabla ya kuuzwa.
“Ndiyo maana leo tunataka tuzungumze na mazungumzo yameshaanza lakini tuyaweke kwenye spidi kubwa ili ikiwezekana tujenge huo mtambo mkubwa, tuanze kuchenjua madini ya nickel kwa nchi zote mbili, tuuze tupate fedha nyingi za kigeni na watu wetu wapate ajira,” amesema Rais.
Hata hivyo, Rais hakuweka wazi eneo ambalo mtambo huo utajengwa.
Rais wa Burundi Èvariste Ndayishimiye amewasili katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma kwa ziara ya Kiserikali ya siku moja na kupokelewa na Rais wa Tanzania Dk John Magufuli. #NuktaHabari
?Ikulu pic.twitter.com/KwWLoI0fgl
— Nukta Tanzania (@NuktaTanzania) September 19, 2020
Pamoja na biashara ya madini, Dk Magufuli amesema watazungumzia pia kuhusu ujenzi wa reli ya kutoka Uvinza Msongati hadi Kitega (Burundi) ili kuwezesha usafirishaji wa mizigo na madini hadi Kigoma.
“Tunataka watu wa Kigoma wakitaka kusafiri, watumie majini, watumie reli, watumie ndege. Reli hii itasaidia kusomba bidhaa pamoja na madini ya nickel,” amesema Rais wakati akihutubia wananchi waliokuja kumpokea Rais Ndayishimiye katika uwanja wa Lake Tanganyika.
Hatua hiyo itasaidia kuwa kitovu cha biashara inayofanyika katika eneo la maziwa makuu kwa sababu Serikali inaendelea na upanuzi wa kiwanja cha ndege na bandari ya Kigoma, ukarabati wa meli za Mv Liemba na Mv Sangara.
Amesema ili kuongeza kasi ya maendeleo ya mkoa huo na nchi za jirani, Serikali itanunua meli mpya mbili ambazo zitakuwa zinafanya shughuli zake katika Ziwa Tanganyika.
“Lakini leo tutakayokuja kuzungumza ni pamoja na kuimarisha uwekezaji na biashara kati ya nchi hizi mbili. Tunataka biashara iwe kubwa zaidi,” amesema Rais kabla ya kuhitimisha hotuba yake.
- Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza afariki dunia
- Rais Magufuli awaweka kitanzini wakuu wa mikoa wasiojenga vituo vya kuuzia madini
Biashara kati ya Tanzania na Burundi inazidi kuimarika. Mwaka 2016 biashara kati ya hizo mbili ilikuwa Sh115.15 bilioni, lakini sasa ni zaidi ya Sh201 bilioni.
Rais wa Burundi, Ndayishimiye amesema anaamini mazungumzo hayo yatazaa matunda mazuri kwa sababu wanaichukulia Tanzania kama mzazi tangu zamani.
“Najua kwamba tukiwa na amani Burundi na Kigoma wanafurahi kwa sababu tulikuwa tunawasumbua sana na wakimbizi,” amesema Rais huyo.
Amewashukuru Watanzania kwa mapokezi mazuri waliyofanya na nchi yake itaendelea kuimarisha mahusiano yaliyopo ikiwemo ya kibiashara.