Huyu ndiye mwanafunzi bora kidato cha nne mwaka 2020

January 15, 2021 12:21 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Paul Luziga akiwa na mama yake. Chanzo| Paul Cosmas Luziga


  • Ni Paul Luziga kutoka shule ya Sekondari ya Pandahill iliyopo mkoani Mbeya.
  • Mkuu wa shule hiyo aeleza jinsi Paul alivyokua na bidii ya kusoma.  
  • Mwanafunzi huyo amepokea kijiti hicho kutoka kwa Joan Ritte wa mwaka 2019.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limemtangaza Paul Cosmas Luziga kama mwanafunzi bora wa mwaka 2020 katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa leo Januari 15, 2021.

Luziga ambaye ni mwanafunzi mhitimu kutoka Shule ya Sekondari ya Pandahill iliyopo mkoani Mbeya amechukua taji hilo kutoka kwa Joan Ritte wa Shule ya St Francis aliyekua mwanafunzi bora mwaka 2019. 

Hiyo ina maana kuwa kwa miaka miwili mfululizo yaani mwaka juzi na 2020, mkoa wa Mbeya umefanikiwa kutoa mwanafunzi bora kitaifa. 

Akiongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) Mkuu wa Shule hiyo, Mtawa Zephania Lusanika amesema Luziga alionyesha matokeo mazuri tangu alipojiunga na kidato cha kwanza katika mtihani wa majaribio ya kujiunga na shule hiyo.

“Hadi anamaliza shule, Paul alikuwa ni kati ya wanafunzi watatu bora wa shule. Tulitarajia atafaulu lakini siyo kwa kiwango ambacho amekifikia,” ameeleza mwalimu huyo ambaye Nukta Habari ilikuwa ya kwanza kumtaarifu juu ya ufaulu wa mwanafunzi wake.


Soma zaidi: 


Paul azungumzia ushindi wake

Akiongea na Nukta, Paul amesema anafuraha isiyo na mfano na hakuwahi kutegemea kama ataweza kufikia katika nafasi hiyo.

“Ninasoma sana lakini ninamtegemea Mungu zaidi. Niliamini nitafannya vizuri lakini siyo kwa kiwango hiki,” ameeleza Paul ambaye changamoto ya ugonjwa wa Corona, haikuweza kuingilia kasi yake ya kujisomea na kupata matokeo mazuri. 

Paul amefaulu kwa daraja la kwanza pointi saba huku akiwa na alama “A” katika masomo yote yakiwemo fizikia, kemia, baiolojia na hisabati. 

Naye mama mzazi wa Paul, Lucy Mwogella amesema mtoto wake alikua akimtegemea Mungu na kwa kipindi chote kuelekea katika mitihani ambapo alifunga bila kula akiombea matokeo yake huku familia ikimsisitiza kusoma kwa bidii.

“Alikuwa na siku tatu za kuacha kula kila wiki. Ilipofika kipindi cha mitihani, tulimwambia aendelee na mitihani na sisi tutaendelea kuomba,” amesema mama huyo huku akitokwa na machozi ya furaha wakati akiongea na Nukta Habari muda mfupi baada ya matokeo kutangwa na Necta. 

Mama huyo amesema licha ya kuwa na uwezo mdogo kiuchumi, ataendelea kufanya kila awezalo kwa msaada wa Mungu kuhakikisha ndoto za mtoto wake zinatimia.

“Hali yetu ni ya kawaida kwani hatuna wa kumtegemea maana baba yake alifariki tangu mwaka 2018. Kwa sasa Paul anasomeshwa na kaka yake,” amesema Lucy. 

Kupata matokeo ingia hapa >>>>> https://bit.ly/2XIyOu0

Enable Notifications OK No thanks