Tasaf kuziinua kaya masikini zaidi ya 5,000 Tanzania
- Zitaingizwa katika Mpango wa Taifa wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) ili ziweze kujikwamua kiuchumi.
- Ni zile ambazo hazikuwahi kupitiwa na mpango huo tangu awamu ya kwanza ilipoanza.
Mwanza. Serikali ipo mbioni kuziingiza zaidi ya kaya 5,500 za Tanzania kwenye Mpango wa Taifa wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) ili ziweze kujikwamua kiuchumi.
Kaya hizo zitakazoingizwa kwenye mpango huo ni zile ambazo hazikuwahi kupitiwa na mpango huo tangu awamu ya kwanza ilipoanza.
Mkurugenzi wa mawasiliano Tasaf Taifa, Zuhura Mdungi akizungumza baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya walengwa katika Wilaya za Magu na Misungwi mkoani Mwanza, amesema mpaka sasa zoezi la kuwatambua walengwa hao limeshakamilika na utaratibu wa kuwaingiza kwenye mpango utafanyika hivi karibuni.
“Tumefanya tathmini na tayari taratibu za kuwaingiza zitaanza hivi karibuni,”amesema Mdungi jana Februari 3 akiwa Mwanza.
Akiwa ameambatana na timu ya wataalam Tasaf Taifa, Mratibu wa mpango huo wilayani Magu, Daniel Sanyege ameeleza kuwa wilaya hiyo ina zaidi ya walengwa 4,998 ambao wengi wao wamenufaika na fedha hizo kwa kukuza uchumi wa familia zao.
Katika wilaya ya Magu pekee zaidi ya Sh3 bilioni zimetumika katika kipindi cha miaka sita kuzinusuru kaya masikini wilayani humo.
Soma zaidi:
- Siku ya Kutokomeza Umasikini Duniani ilivyogeuzwa kuwa Siku ya VICOBA Tanzania
- Umaskini wa kaya Tanzania washuka-Ripoti
Magu ilivyofaidika na fedha za Tasaf
Sanyenge anaeleza kuwa ruzuku inayotolewa na Tasaf imesaidia kaya nyingi masikini kuweza kupeleka watoto wao shule jambo ambalo limesaidia watoto wengi kufika ngazi ya chuo kikuu.
“Tuna watoto sita wanaotokea kaya masikini wanaendelea na masomo ya vyuo vikuu, watoto wengine 27 wanasoma elimu ya sekondari kidato cha tano na sita, haya ni mafanikio makubwa ambayo bila kuwezeshwa watoto hao wasingetimiza ndoto zao,” amesema Sanyenge
Mafanikio mengine ambayo walengwa wamefanikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za bati, kununuaa ng’ombe pamoja na kufanya miradi ya maendeleo.
“ Kabla sijaingizwa kwenye mpango huu nilikuwa nalala njaa, kwa sasa naishukru Tasaf kwa kuwa imenisaidia nimejenge nyumba na ninafanya ufugaji,”amesema Makoye Linda mkazi wa Nyashiwa wilayani humo.
Mbali na mafanikio hayo, Tasaf pia imefanikisha kujenga visima vya maji 150 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, pia wamefanikiwa kuchimba malambo 32 kwa ajili ya kunyweshea mifugo, kufulia na kufanyia ujenzi.
Mkazi wa kijiji cha Nyanag’omango wilayani Misungwi, Benedatha Shija anasema kabla ya mradi huo walilazimika kutembea umbali wa kilomita 10 kufuata maji.
“Taunaishukru Serikali kupitia Tasaf kwa kutujengea miradi ya maji ambayo tunatumia kwa matumizi ya nyumbani,” amesema Shija.