The Conjuring: Shetani alinifanya niyafanye haya
- Ni filamu inayomhusu kijana aliyemuua baba mwenye nyumba wake.
- Kesi yake inazua utata baada ya kudai sio yeye aliyeua bali mapepo.
- Mambo yana shika kasi baada ya vifo na kesi za aina hiyo kuongezeka.
Dar es Salaam. Imezoeleka shetani kuhusishwa pale kila baya la mwanadamu linapofanyika. Iwe mwizi, jambazi au muongo kafanya yake, ukimuuliza sababu ya kufanya hayo, jibu ni shetani.
Je, itakuwaje pale mauaji yanapopelekea kuvumbuliwa vitu vingine ambavyo shetani alishawishi watu wafanye?
Hata ungekuwa wewe ndiyo askari, ungefanya nini pale unapomsimamisha mtu na anakubali kusimama lakini anapogeuka, anakuwa ametapakaa damu huku sentesi ya kwanza kuongea ni “nahisi kuna mtu nimemuumiza”.
Ni kana kwamba hajui damu hizo kazitoa wapi na hata hapo alipo, hajui amefikaje.
Hilo ndilo lililotokea kwa askari ambaye alisimamisha Arne, kijana ambaye alimuua mwenye nyumba wake kwa kumchoma kisu mara 22 na akidai alikuwa chini ya shinikizo la mapepo.
Anapokamatwa na kufikishwa mahakamani, wapelelezi wa matukio ya kutatanisha Ed na Lorraine Warren wanakuwa msaada kwake.
Kesi ya Arne inakuwa ni kesi ya kwanza nchini Marekani ambayo madai yake ni mauaji yaliyofanyika chini ya shinikizo la mapepo.
Baada ya kesi hiyo kusambaa kama moto wa mbuga kavu, inaibua kesi zingine nyingi ambazo zilitokea kwa mazingira ya kutatanisha tena kama ya kesi ya Arne ikiwemo kesi ya kifo cha Katie Lincoln ambaye pia aliuawa kwa kuchomwa kisu mara 22.
Baada ya kiza kinene, wapelelezi hao wanabaini kuwa, Jessica ambaye ni rafiki wa karibu kwa Katie alimchoma rafiki yake kisu mara 22 na inadaiwa naye alikuwa chini ya mshawasha wa mapepo kama ilivyokuwa kwa Arne.
Soma zaidi:
- Kutoka binti mpole hadi kubwa la maadui
- Zingatia haya kabla haujaamua kujichora “tatoo”
- Watanzania walivyoipokea huduma mpya ya sauti ya Vodacom Tanzania
Siku sio nyingi, kazi ya upepelezi wa Ed na Lorraine inazaa matunda baada ya kugundua chanzo cha anayesababisha watu kujikuta wamewaua watu wanaowapenda au wanaowafahamu.
Wanagundua kuwa ipo madhabahu ya mtu ambayo bila kuivunja na kuiharibu, vifo vitazidi kuendelea hivyo wanaanza safari yao kwa hatua moja inayozaa hatua nyingine.
Safari ya kuitafuta madhabahu hiyo inaanza huku ikitanguliwa na vikwazo ambavyo hawana budi kuvivuka.
Kujaribiwa kiasi cha kutaka kuuana, nguvu ya huba ikiishinda nguvu ya giza na sheria kupindishwa ni sehemu ya utakayoyashuhudia katika filamu ya “The Conjuring”.
Mahakama inaamini uwepo wa Mungu pale mtu anapoapa kusema ukweli, vipi pale mtu anaposema umefanya kosa chini ya mshawasha wa shetani?
Je, pale mtu anapokuwa amemuua mwenzi, ni nani ameua? Yeye au ndio tuseme shetani amemtuma.
Tukutane wiki ijayo.
Latest
