Rais Samia: Watanzania nipeni muda niisimamishe nchi kiuchumi

June 28, 2021 3:17 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema hitaji kubwa la Watanzania ni kuwa vizuri kiuchumi.
  • Amesema mambo mengine ikiwemo katiba yatafuata baadaye.
  • Watanzania watakiwa kushikamana kujenga uchumi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema anaomba apewe muda aisimamishe nchi kiuchumi kwanza na baadaye atashughulikia masuala mengine ya kisiasa ikiwemo mabadiliko ya katiba mpya na mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa Tanzania.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Juni 28, 2021 na wahariri wa vyombo vya habari Tanzania , Ikulu mkoani Dar es Salaam amesema kwa sasa kazi kubwa iliyopo ni kuifungua nchi kiuchumi ili kuboresha maisha ya Watanzania jambo litakalosaidia hata kuimarika kisiasa.

“Uwekezaji uwe mkubwa ajira ipatikane, pesa izunguke mifukoni, uchumi ukue wa mtu mmoja mmoja lakini tuzidi kukusanya mapato, tukusanye kodi nyingi tuweze kujifinance (kujifadhili) katika mambo yetu ya maendeleo,” amesema Rais Samia.

Amesema kufanikisha azma hiyo, ni jukumu la kila mmoja ndani ya nchi, “Serikali tuna jukumu hilo, vyombo vya habari, vyama vya siasa kwa sababu uchumi ukipanda umepanda uchumi wa Tanzania na kila mmoja wetu anafaidika.”

Kiongozi huyo mkuu wa nchi alikuwa akijibu swali la mwanahabari wa shirika la habari DW, Hawa Bihoga aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuanza mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.

Amesema ili kukamilisha jukumu hilo kubwa, amewaomba Watanzania wampe muda atalishughulikia hapo baadaye baada ya uchumi kusimama.

“Kama inavyosemwa nimeanza vizuri naomba nipeni muda niisimamishe nchi kwanza kiuchumi halafu tutashughulikia mengine. Tutashughulikia katiba, hiyo mikutano ya hadhara wakati ukifika,” amesema Rais.

Kwa sasa, vuguvugu la kudai katiba mpya limeanza tena kwa baadhi ya vyama vya siasa na wananchi kuonyesha muitikio na kuitaka Serikali kuanzisha mchakato ili kuweka misingi imara ya ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora uliojengwa katia taasisi na siyo watu.

Rais amesema kwa sasa, wameruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya ndani na wabunge kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao. 

“Watanzania tujime muda tufanye uchumi wetu ndilo la maana kwa Watanzania kuliko haya mengine, sisemi katiba si ya maana, ya maana sana lakini naomba nipeni muda niisimamishe Tanzania kiuchumi kwanza,” amesisitiza Rais.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV