Dalili, tiba dhidi ya minyoo ya tumboni
- Minyoo hiyo huingia mwilini kwa kula chakula au kunywa maji ambayo siyo salama.
- Inashauriwa kufuata kanuni za usafi ikiwemo kukata kucha.
- Endapo mwanafamilia mmoja atakutwa na minyoo, familia yote inashauriwa kutafuta tiba.
Dar es Salaam. Kama kijana, niwapo nyumbani matarajio ya wazazi wangu na wanafamilia ni kula chakula kingi kwani ni uhalisia kuwa nina hekaheka za kutosha kila siku.
Ni matarajio ya mama yangu aone nikikata pande kubwa la ugali na kujaza sahani ama vijiko vingi vya ubwawa ili nishibe na nijenge mwili wangu kama walivyo vijana wengine.
Hata hivyo, siku zote kiasi cha chakula changu kimekuwa mjadala kwa familia nzima kwani ugali ninaokula ni kama ule unaoliwa na mtoto wa miaka mitatu. Siyo mchana, siyo usiku.
“Yaani wewe unazidiwa hadi na mwanao,” mama yangu hunitania huku akilinganisha chakula changu na cha wajukuu zake ambao wananiita mimi baba yao mdogo.
Mara zote, nyumbani wamekuwa wakiiona hiyo kama dalili ya minyoo ya tumboni na kusema ninatakiwa nipewe dawa za minyoo ninywe.
Nimetumia vidonge lakini wapi! Hali ni ile ile. Tutalijadili tatizo langu siku nyingine lakini leo, tuongelee hii minyoo ya tumbo inayohusishwa na chakula na tuifahamu zaidi.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa afya kutoka hospitali ya Kumbukumbu ya Rabininsia ya mkoani Dar es Salaam, Dk Godfrey Ngowi, minyoo ipo aina nyingi na mtu anaweza kuonyesha dalili tofauti tofauti kulingana na aina ya minyoo aliyonayo.
Dk Ngowi amesema minyoo inaingia mwilini kwa njia tofauti ikiwemo kunywa maji au kula chakula chenye vimelea na kula udongo ambao unaweza kuwa na wadudu hao.
“Njia nyingine ni kula nyama ambayo ina maambukizi na haijaiva vizuri. Inaweza kuwa nyama ya ng’ombe, samaki na hata kitimoto,” amesema Dk Ngowi.
Mtaalamu huyo amesema pia mtu anaweza kupata minyoo ya tumboni kwa kuchangamana na kinyesi, au kuwa katika maeneo ambayo siyo safi.
Ili kujua kuwa unamaambukizi ya minyoo, inashauriwa kuonana na wataalamu wa afya. Picha| Medical News Today.
Utajuaje kama una minyoo?
Dalili za minyoo hutofautiana kati ya mtu na mtu kulingana na kiwango cha maambukizi na aina ya mnyoo alionao mtu.
Dk Ngowi amesema dalili ambazo zinajulikana kwa wengi ni pamoja na kuhara, kutapika, kuhisi kichefuchefu na kupungua uzito ghafla.
“Kwa wengine wanaweza kuwa wanahara kinyesi ambacho kina damu na ute au kamasi. Wengine pia hukumbwa na maumivu makali ya tumbo,” amesema mtaalamu huyo.
Tovuti ya afya ya WebMd imeandika kuwa, dalili nyingine ni kuwa na muwasho katika sehemu ya haja kubwa hasa wakati wa usiku na kwa baadhi ya wanawake, muwasho katika sehemu za ukeni.
Na kwa tatizo la mlo, WebMd imesema pale mtu anapopitia mabadiliko ya kiwango chake cha chakula ikiwa ni kula kupita kiasi au kukosa hamu ya kula ni dalili mojawapo ya kuwa ana minyoo.
Kinga dhidi ya minyoo
Ili kuepukana na minyoo, inashaurwa kufuata kanuni za usafi ikiwemo wa mazingira, mwili na chakula unachotumia.
WebMd inashauri kunawa mikono yako kwa maji safi kabla ya chakula na baada ya kwenda chooni au kuwabadilisha watoto kwa wakati. Hiyo itakusaidia kuhakikisha haupati minyoo kwa njia ya chakula.
Dk Ngowi anashauri kukata kucha, kufua nguo zako na mashuka ya kulalia mara kwa mara na kuepuka kula nyama ambayo haijaiva vizuri kwani inaweza kuwa na maambukizi hasa nguruwe, ng’ombe na samaki.
Mtaalamu huyo pia anashauri, endapo mwana familia mmoja atakutwa na minyoo, inatakiwa wanafamilia wote wakapime na kutumia dawa za minyoo na mara nyingi dozi mbili huwa suluhu kwa wengi.
Kukabiliana na minyoo, inashauriwa kunawa mikono kwa maji safi na sabuni mara kwa mara hasa unapojua umeshika sehemu ambayo sio salama. Picha| Sight Savers.
Matibabu ya minyoo
Fahamu: Kabla ya kuanza kutumia dawa za minyoo, hakikisha umemtembelea mtaalamu wa masuala ya afya ili kufahamu kiwango cha maambukizi na dawa sahihi kwa ajili ya tatizo lako.
Hilo ni muhimu kwa sababu dalili za minyoo zinaendana na dalili za magonjwa mengine hivyo, dalili pekee haziwezi kukupatia jawabu la nini kinakusumbua bali vipimo vya kitaalamu.
Mfamasia kutoka Mkoani Mwanza, Winfrida George ameiambia Nukta Habari kuwa minyoo hutibiwa kwa dawa tofauti tofauti kulingana na dalili alizonazo mgonjwa na ndiyo maana, inashauriwa kuonana na mtaalamu kwanza kabla ya kuamua kubugia dawa na vidonge.
George amesema dawa za minyoo ni pamoja na “Albendazole tablet 400mg” ambayo hutumika mara moja kwa siku tatu mfululizo. Dawa zingie ni “mebendazole na levamisole” ambazo pia mtu ataelekezwa na daktari matumizi yake.
“Zakuzuia kuhara ni pamoja na metrinidazole na tinidazole na kama anahara damu, erythromycin, azthromycin na zingine zipo nyingi zitamsaidia,” George amesema kujua dawa ipi itafanya kazi inahitaji vipimo ili kubaini aina ya mnyoo na aina ya maambukizi.
Latest
