Ada ya maegesho ya magari kulipwa kielektroniki Dar
- Ni maegesho ya magari katika barabara zinazomilikiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura).
- Malipo yatafanyika kwa njia ya mtandao badala ya fedha taslimu.
- Itasaidia kudhibiti ‘vishoka’ na upotevu wa mapato ya Serikali.
Dar es Salaam. Ifikapo Septemba Mosi mwaka huu, Mkoa wa Dar es Salaam utaanza kutumia mfumo wa ulipaji ada ya maegesho ya magari kwa njia za kielektroniki ili kudhibiti uvujaji wa mapato ya Serikali baada ya mfumo huo kuzinduliwa rasmi leo jijini hapa.
Ada hizo zitahusu maegesho ya magari katika barabara zinazomilikiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) na zitakuwa zikilipwa kwa njia ya mtandao badala ya fedha taslimu.
Serikali imeamua kuwekeza katika mfumo huo kuondoa changamoto mbalimbali za ukusanyaji wa ada kwa njia ya kulipia fedha taslimu, jambo lililokuwa linatoa mwanya wa upotevu wa mapato.
“Kulikuwepo na watu ambao si wafanyakazi wa Tarura, jiji au manispaa walijianzishia utaratibu wa kukusanya ushuru wa maegesho, mapato hayo yaliishia mikononi mwao. Mfumo wa ulipaji ada za maegesho kwa njia za Kielektroniki ni mwarobaini wa watu hao,” amesema Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla aliyekuwa akizindua mfumo huo leo.
Pia utaondoa kero ya watu wasiojulikana wanaojifanya wasimamizi wa maegesho ya magari wanaovamia wakazi wa Dar es Salaam kwa ajili ya kuwataka kulipia ada.
“Mfumo wa ulipaji ada ya maegesho kwa njia za Kielektroniki wa TARURA ni mfumo mzuri ambao unakwenda kuisaidia serikali katika kudhibiti mapato yake lakini pia unaenda kuondoa kero kwa wananchi,” amesema Makalla.
Ifikapo Septemba Mosi, 2021 Mkoa wa Dar es Salaam utaanza kutumia mfumo wa ulipaji ada ya maegesho kwa njia za Kielektroniki hatua inayotajwa kudhibiti uvujaji wa mapato ya serikali, hii ni kufuatia mfumo huo kuzinduliwa rasmi leo Agosti 24, 2021 na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla. Picha| Dar Mpya.
Mfumo wa ulipaji ada ya maegesho kwa njia za kielektroniki wa TARURA una faida mbalimbali ikiwemo kuondosha kero kwa mteja kwa kumpa nafasi ya kufanya malipo ya ada ya maegesho iwe malipo ya baada au kabla kutokana na uwezo wake kupitia mitandao ya simu.
Tarura inaungana na taasisi mbalimbali za Serikali ambazo zinatumia mifumo ya kielektroniki kufanya malipo na hivyo kuongeza wigo wa utumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu ambazo ni salama na zinaokoa muda.
Mkuu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Tarura, Stanley Mlula amesema mfumo huo wa kieletroniki unasimamia ukusanyaji na shughuli zote za mapato ya wakala hao wa barabara za mijini na vijijini.
Kwa mujibu wa Mlula, mfumo huo utaunganishwa na mfumo wa Jeshi la Polisi unaoruhusu kuwabaini na kuangalia watu wanaodaiwa.
‘Mazungumzo yameshaanza, mtu akikimbia na deni letu akikamatwa na polisi anaambiwa anadaiwa na Tarura,” amesema Mlula.
Latest