Air Tanzania yaja na huduma mpya malipo tiketi za ndege

September 9, 2021 11:07 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Mteja anaweza kulipia malipo ya tiketi ya ndege kidogo kidogo.
  • Huduma hiyo imepewa jina la “Kibubu”.
  • Itatoa hamasa Watanzania kutumia usafiri wa ndege.

Dar es Salaam. Katika kuimarisha ushindani wa usafiri wa anga, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limezindua huduma mpya ya kulipitia malipo ya tiketi za ndege kidogo kidogo kabla ya siku ya safari haijafika. 

Huduma hiyo imepewa jina la “Kibubu” ambapo mteja anaweza kupanga safari mapema na kulipia tiketi yake kidogo kidogo hadi wiki moja kabla ya safari yake.

“Hii huduma ni kwa wateja wetu wote na ni kwa safari zetu zote za ndani na nje ya nchi,” amesema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha ATCL, Josephat Kagirwa leo Septemba 9, 2021 jijini Dar es Salaam.

Amesema mteja atatakiwa kuweka Sh50,000 kwa mara ya kwanza na kiasi kinachobakia atatakiwa kulipa kidogo kidogo kwa kiwango anachokimudu mpaka safari yake itakapofika.

Huduma hiyo ambayo pia inadumisha na kuimarisha uhusiano wa ATCL na wateja wake, huenda ikawasaidia watu wanaopenda usafiri wa ndege lakini wanakosa nauli kwa wakati.

Kwa sasa, wateja watafanya malipo ya awali ya tiketi zao (booking) katika ofisi za ATCL na hapo baadaye huduma hiyo itakuwa inafanyika kwa njia ya benki.

Kwa mujibu wa ATCL, masharti hayo hayatofautiani na tiketi za kawaida na endapo mteja atahirisha safari, watazingatia vigezo na masharti kabla ya kumpangia safari nyingine.

Ofisa Masoko wa ATCL, Grace Magubo amesema Watanzania wajitokeze kutumia huduma hiyo kwa sababu ni rahisi na salama ya kujipatia tiketi kulingana na uwezo wako.

Amesema watatoa zawadi kwa watu ambao wataweza kuwahamasisha watu kutumia huduma hiyo ambapo ni pamoja kutoa tiketi ya ndege kwa nusu bei ya mahali unapotaka kwenda.

Kwa sasa, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lnachuana vikali na Shirika la ndege la Precision Air baada ya kampuni ya ndege ya FastJet kumwaga manyanga miaka miwili iliyopita.

Katika hotuba zake Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisema kuwa Serikali yake itaendelea kuilea ATCL kimkakati ii liweze kujiendesha kwa ufanisi ikiwemo kulitua mzigo wa madeni makubwa na kulipa ahueni ya baadhi ya tozo na kodi. 

ATCL ina vituo 23 ambavyo ndege zake zinatua ndani na nje ya nchi ambapo inatarajia kufufua safari ambazo zilisitishwa hasa wakati wa janga la Uviko-19 ikiwemo za kwenda India.

Enable Notifications OK No thanks