Tamu, chungu: Usafiri wa bodaboda kwa watoto
- Ni watoto kukosa usimamizi wanapotumia pikipiki.
- Hali hiyo husababisha majeraha na vifo.
- Wazazi, wadau watakiwa kuongeza elimu na ulinzi kwa watoto.
Dar es Salaam. Ni asubuhi ya saa 12 na kila awaye mfanyakazi yupo kwenye haraka ya kufika kazini kwake mapema. Wenye gari zao, wanaotumia daladala na hata wenye pikipiki, wote katika barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam, mwendo wao ni mpela mpela.
Nikiwa katika usafiri wa daladala kuelekea kazini, inapita bodaboda ambayo mwendo wake si haba. Inaendeshwa na kijana ambaye ameenea vizuri katika pikipiki hiyo.
Nyuma yake ni mtoto anayeonekana kuwa na miaka nane kiumbo lakini hajazidi miaka 10 ambaye mikono yake ameinyoosha hadi mwisho kushika pembe za koti la dereva wa pikipiki.
Sura yake akiwa ameilaza kiupande kwenye mgongo wa dereva, kwa jinsi kichwa chake kilikuwa kikipanda na kushuka, ni ishara kuwa mtoto huyo alikuwa anasinzia.
Hali hiyo huenda ingebadilisha asubuhi ya dereva huyo endapo wangefika tutani au kama mikono ya binti huyo ingeachia koti lake.
“Mtoto anasinzia huyoo! We bodaaaa!” Waliita baadhi ya abiria kwenye gari na dereva alipiga honi kadhaa lakini sauti zote hizo zilipeperushwa na upepo bila mafanikio ya kupata umakini wa dereva aliyekuwa akiendesha pikipiki ile.
Kutoka kwenye gari nililokuwepo, ilimlazimu mmoja wa abiria mwenzetu kushuka na kuita bodaboda na kuifukuzia pikipiki ile ambayo nambari ya usajili wake ilikuwa katika kibao cha njano ikimaanisha ni pikipiki binafsi.
Watu kwenye gari walibaki wakiongelea muda alioamshwa mtoto na kwa nini mzazi amekubali mtoto mdogo kupanda pikipiki bila tahadhari yoyote.
Siyo mara ya kwanza kushuhudia tukio hilo, lingine lilikuwa la “mshkaki” wa watoto watatu na dereva wa bodaboda ambaye naye, alikuwa anawapeleka watoto shule.
Bodaboda ni kati ya vyombo vya usafiri ambavyo vimekuwa chanzo kikubwa cha majereha na vifo vinavyotokana na ajali barabarani. Ajali hizo hutokea kwa sababu mbalimbali ikiwemo uvunjifu wa sheria, mwendo kasi na ulevi.
Wengine huenda mbali na kupakiza zaidi ya watoto wawili. Picha| Twitter.
Ripoti ya Takwimu Muhimu Tanzania ya mwaka 2020 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imeeleza kuwa kulikuwa na jumla ya ajali 1,933 za barabarani mwaka 2020 na watu 2,362 walijeruhiwa katika ajali hizo zilizohusisha magari, pikipiki na vyombo vingine vya usafiri wa barabarani. Kati ya ajali hizo, kulikuwa na vifo 1,384.
Kinachojulikana miongoni mwa wadau wa usafiri wa pikipiki
Huenda ukadhani dereva wa pikipiki hawajui kama kinachofanyika ni makosa lakini sheria zipo wazi kuwa mtoto yeyote hatakiwa kupakizwa juu ya pikipiki bila ya kuwa na mtu mzima wa kushikilia nyuma yake.
Dereva wa pikipiki mtaa wa Victoria jijini Dar es Salaam, Musa Omary ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, kisheria mtoto anatakiwa kukaa nyuma ya dereva na nyuma yake awepo mtu mzima wa kumshikilia.
“Hata kwenye bajaji, mtoto haruhusiwi kukaa nyuma peke yake. Sheria zipo ni vile tu hawajabahatika kukamatwa,” amesema Omary.
Dereva huyo amesema sheria iliyopo inamweleza dereva wa pikipiki kuendesha kwa mwendo usiozidi kilomita 45 hadi 50 kwa saa pale anapokuwa amempakiza mtoto.
“Ukikamatwa hapo ni faini kubwa tu au unaweza hata kuwekwa ndani ili ujifunze,” amesema Omary.
Sheria ya Usalama Barabarani (Road Traffic Act) ya mwaka 1973 imeeleza kuwa watoto wanaotumia usafiri wa pikipiki wanahitaji usimamizi wa watu wazima wakiwemo wazazi ili kuwaepusha na ajali.
Vitendo vyovyote vinavyohatarisha usalama wa watoto wanapotumia barabara vinaweza kumtia hatianni muhusika ikiwemo kupigwa faini au kufungwa jela.
Mkazi wa Shinyanga, Kassandra Hassan amesema swala la wazazi kuwapandisha watoto wadogo bodaboda peke yao ni tabia ambayo kwa sasa imeota mizizi.
Amesema asilimia kubwa ya wazazi au walezi huwapandisha watoto wadogo bodaboda peke yao hasa wakati wa kwenda shuleni kutokana na usafiri huo kuwa wa haraka na hauna muingiliano wa watu wengi ikilinganishwa na daladala.
Hata hivyo, kutokana na umri wa watoto usafiri huo unakuwa siyo salama pale wanapopandishwa bila uangalizi wa mtu mzima.
“Hili swala ni la hatari sana kwa watoto kwa sababu ajali zimekuwa ni nyingi kwasababu watoto wanalala wakiwa njiani na dereva mwenyewe (bodaboda) anakuwa hajui kama mtoto amelala hivyo wengi huanguka na kuumia,” amesema Hassan ambaye ni mzazi wa mtoto mmoja.
Inashauriwa mtoto akipandishwa pikipiki, mzazi akae nyuma ya mtoto kwa ajiliya kumshikilia. Picha| Pinterest.
Wadau wa usalama barabarani wanena
Usafiri wa pikipiki umetengenezwa kwa ajili ya kubeba watu wawili tu lakini kwa baadhi, bado wanalazimishwa usafiri huo kupandwa na watu zaidi. Wengine huenda mbai na kuakiza hadi watoto watatu kwenye pikipiki moja na dereva akiwa mtu wa nne.
Balozi wa Usalama Barabarani, Ramadhan Msangi ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, ni kosa kisheria kupakiza abiria zaidi ya mmoja kwenye pikipiki kwani inatakiwaa pikipiki ibebe watu wawili (dereva na abiria).
Hata hivyo, sheria inaruhusu mtoto wa umri chini ya umri wa miaka 9 kupanda pikipiki akiwa na msaidizi kwa maana mtu wa kumshikikilia.
“Ni jambo ambalo linahatarisha usalama wa hao watoto lakini na hata watumia barabara wengine pia maana sote tunajua ajali ikitokea, madhara yanaweza kuwapata hata watumia barabara wengine wanaokuwa eneo la ajali,” amesema Msangi.
Ili kuepukana na madhara mbalimbali, wadau wanashauri wazazi kuzingatia sheria ambayo ni kuhakikisha inapobidi mtoto apande pikipiki, basi aongozane na mtu mzima ambaye atakaa nyuma yake.
Lakini pia, kuangazia njia nyingine za usafiri ambao ni salama zaidi ikiwemo mabasi ya shule na hata daladala kwani mara nyingi huwa na sehemu ambazo wototo wanaweza kukaa.
“Nashauri wazazi au walezi waangalie njia nzuri na salama za kuwafikisha watoto wao shuleni ikiwezekana watoto wapandishwe bodaboda akiwepo na mtu mzima,” ameshauri Hassan.
Endapo Watanzania wakiamka na kulikemea hili, Taifa la kesho litalindwa na kuweza kutimiza ndoto zao.
Latest