Jaji Siyani ajitoa kesi ya Mbowe na wenzake, atoa maelekezo

October 20, 2021 8:39 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akishuka katika gari kwenda kusikiliza kesi inayomkabili na wenzake watatu ya mashtaka sita yakiwemo ya kula njama ya kutenda kosa na kufadhili fedha kwa ajili ya vitendo vya ugaidi. Picha| Mtandao.


  • Sababu kuu ni majukumu ya Jaji Kiongozi aliyonayo. 
  • Amejitoa muda mfupi baada ya kutoa uamuzi wa kesi ndogo katika kesi ya msingi inayowakabili washtakiwa hao.
  • Anakua Jaji wa pili kujitoa baada ya Jaji Elinaza Luvanda.

Dar es Salaam. Jaji Mustapha Siyani wa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa amejitoa kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu kutokana na majukumu ya Jaji Kiongozi aliyonayo.

Jaji Siyani aliyekuwa anaendelea kusikiliza kesi hiyo, aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 8 mwaka huu kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Tanzania na hivyo kumuongezea majukumu yake.

Jaji huyo akizungumza muda mfupi leo Oktoba 20 baada ya kutoa uamuzi wa kesi ndogo katika kesi ya msingi inayowakabili washtakiwa hao, amesema hawezi kusikiliza shauri hilo mfululizo kutokana na majukumu ya kuwa Jaji Kiongozi.

“Hivyo kwa majukumu niliyonayo nimeona nijitoe, aje Jaji mwingine haraka iwezekanavyo,” amesema Jaji Siyani ambaye ametupilia mbali pingamizi la upande la utetezi la kutaka maelezo ya mshtakiwa katika kesi hiyo Adamu Kasekwa yasipokelewe kwa madai yaliwasilishwa nje ya muda wa kisheria na mtuhumiwa alitishiwa kuteswa. 

Jaji Siyani anakuwa Jaji wa pili kujitoa katika kesi hiyo ya Mbowe na wenzake wanaokabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama ya kutenda kosa na kufadhili fedha kwa ajili ya vitendo vya ugaidi.

Awali kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 16/2021 ilikuwa inaendesha na Jaji Elinaza Luvanda ambaye alijitoa kutokana na mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, Freeman Mbowe kwa niaba ya wenzake kusema kuwa hawana imani na Jaji huyo katika kutenda haki dhidi ya kesi yao.

Mbowe alitoa madai hayo Septemba 6, 2021 muda mfupi baada ya Jaji Luvanda kutupilia mbali mapingamizi mawili kati ya matatu yaliyowasilishwa mahakamani hapo dhidi ya washtakiwa hao.

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan, wa pili ni Adamu Hassan Kasekwa, wa tatu Mohamed Abdillahi Ling’wenya na wa nne Freeman Aikael Mbowe.

Washtakiwa hao wanatetewa na jopo la mawakili 14, likiongozwa na Peter Kibatala, huku upande wa mashtaka ukiwa na mawakili watano wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW