Wawekezaji walia uhaba wa umeme, maji
- Wasema shughuli za uzalishaji zimepungua.
- Serikali yasema itafuta ufumbuzi wa kudumu.
Mwanza. Baadhi ya wawekezaji wa viwanda katika Mkoa wa Mwanza wamesema ukosefu wa maji na umeme wa uhakika wakati huu umewapunguzia kasi ya uzalishaji bidhaa, jambo linaloathiri mwenendo wa biashara zao.
Wawekezaji hao wametoa malalamiko hayo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Geofrey Mwambe alipotembelea baadhi ya viwanda mkoani hapa leo Novemba 26, 2021.
Meneja wa uhakiki wa ubora wa kiwanda cha kutengeneza madawa ya binadamu cha Prince Pharmaceutical Co Ltd, Fred Kilamlya amesema changamoto ya kukatika kwa umeme na maji inasababisha washindwe kufanya uzalishaji kwa kiwango walichojiwekea.
Kilamlya amesema wanahitaji lita za maji 350,000 kwa wiki, lakini wanapata kiasi kidogo, jambo ambalo linawafanya washindwe kuzalisha madawa kwa kiwango kinachohitajika.
Malalamiko hayo pia yametolewa na uongozi wa kiwanda cha Sandvik kinachotengeneza mitambo ya migodi ambapo ukosefu wa umeme wa uhakika umekuwa ukikwamisha shughuli zao.
Tatizo la upungufu wa maji linaelezwa linatokana na ukame na mabadiliko ya tabianchi.
Katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro na Arusha, shughuli nyingi za kiuchumi zinazotumia umeme zimetatizika, hasa saluni, wachomea vyuma (welding), wauza samaki, mashine za kusaga, hoteli na baa.
Serikali imeahidi kushughulikia tatizo la maji na umeme kwa wawekezaji katika sekta mbalimbali hapa nchini ili waweze kuzalisha kwa tija.
Waziri Mwambe amesema bwawa la Mwalimu Nyerere lililopo Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ambalo linatarajiwa kuzalisha umeme wa megawati 2,115 likianza uzalishaji litasaidia kupata nishari ya uhakika zaidi kwa wawekezaji.
Waziri huyo anasema Serikali inatambua umuhimu wa wawekezaji na kwamba inafanya juhudi mbalimbali kupata ufumbuzi wa kudumu wa nishati ya umeme na maji.
“Serikali inatambua malalamiko mliyotoa kuhusu umeme na maji na Serikali itafanya mawasiliano ya ndani kupata ufumbuzi,” amesema Mwambe.
Amesema Serikali ipo kwa ajili ya kulinda wawekezaji wote na kwamba suala la nishati ya umeme ni muhimu kwa ajili ya uzalishaji.
Latest
