Rushwa yaendelea kutikisa taasisi za elimu
- Ukosefu wa maadili watajwa kushamirisha rushwa hiyo.
- Suluhu ni kila mmoja kupinga rushwa katika eneo lake.
Dar es Salaam. Mikakati zaidi inahitajika iiwemo elimu ya kutokomeza rushwa katika shule na vyuo mbalimbali Tanzania baada ya kubainika kuwa rushwa bado inatikisa taasisi hizo za elimu.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza kupokea jumla ya malalamiko 139 katika kipindi cha Mwezi Octoba hadi Desemba, 2021 ambapo kati ya hayo, 70 yalihusisha na rushwa katika taasisi mbalimbali.
Kati ya malalamiko hayo 70 yaliyoripotiwa, 16 yalitoka katika taasisi za elimu yakiwemo yanayohusu rushwa ya ngono. Malamiko hayo 16 kutoka taasisi za elimu ni mengi kuliko taasisi zingine zilizokuwa na matukio ya rushwa.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Frank Mkilanya aliyekuwa akitoa taarifa ya hali ya rushwa katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2021 katika mkoa huo jana Januari 25 amesema kati ya malalamiko 70 yanayohusiana na rushwa, 62 uchunguzi wake unaendelea na sita uchunguzi wake imekamilika kwa watuhumiwa kufikishwa mahakamani.
Malalamiko mawili majadala yake yamepelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kupata kibali vya kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.
Aidha, katika malalamiko 69 yasiyohusu rushwa, taarifa 10 zimehamishiwa kwenye idara nyingine na malalamiko 59 elimu na ushauri umetolewa kwa wahusika.
“Takukuru tumekuwa na utaratibu wa kufuatilia mienendo ya utungwaji na usahihishaji wa mitihani kwenye vyuo vidogo, vya kati na vikuu kubaini kama vinaendana na matakwa ya kisheria, lakini bado kuna vimelea vya rushwa ambavyo vinaitafuna idara ya elimu, ” amesema Mkilanya.
Soma zaidi:
Hata hivyo, taasisi hiyo imeendelea kupanua wigo wa kupambana na rushwa ambapo tayari imezindua kampeni kwa vijana wa skauti kuwashirikisha kikamilifu katika mapambano hayo.
Kwa sasa, vijana hao wanapatiwa elimu ili wakawe mabalozi wazuri wa kupambana na rushwa.
Sababu za kukithiri rushwa ya ngono
Utafiti uliofanywa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika kipindi cha Januari na Februari mwaka 2020, ulibaini kuwa mmomonyoko wa maadili na matumizi mabaya ya madaraka, vimetajwa kuwa vyanzo vya kuwapo kwa rushwa ya ngono katika vyuo vikuu vikiwemo vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Sababu nyingine ni mfumo wa utoaji taarifa kutokuwa rafiki, mifumo dhaifu ya kushughulikia rushwa ya ngono na mamlaka ya kutoa alama za mitihani kuachiwa wahadhiri pekee.
Latest