Imani potofu zachangia watoto kupata saratani Kanda ya Ziwa

September 27, 2022 7:37 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baadhi ya watu kutoamini kuwa watoto wanaweza kuugua saratani.
  • Kuchelewa kwenda kupata matibabu kwachangia tatizo kuwa kubwa.
  • Serikali, wadau waingilia kati kumaliza saratani kwa watoto.

Mwanza. Mecktilida Saluja mkazi wa mtaa wa Mkolani jijini Mwanza alikuwa miongoni mwa watu ambao walikuwa hawaamini kuwa mtoto mdogo anaweza kupata saratani.

Hata ikitokea aliamini kuwa mtoto anakuwa amelogwa na si vinginevyo.

Bila kutarajia, Mecktilida, mama watoto watatu yalimfika kwenye nyumba yake baada ya mtoto wake kupata saratani.

Mtoto wake Cleopatra Fideli (3) akiwa na umri wa miaka miwili Julai mwaka jana, alipata  uvimbe vigumu sehemu ya tumbo lakini mama yake hakutilia maanani. 

Hali ya mtoto ilianza kubadilika akawa anapata homa za mara kwa mara na Agosti mwaka jana alipompeleka hospitali kumpima alionekana kuwa na uvimbe kwenye ini.

“Nilipewa rufaa ya kwenda Bugando kwa ajili ya matibabu na baada ya vipimo niliambiwa mtoto ana saratani ya ini, kitendo ambacho kilinishtua kwa kuwa huwa nasikia saratani huwapata watu wazima,” anasema Mecktilida.

Mecktilida anasema hakuweza kuamini moja kwa moja kama mtoto wake ana shida hiyo na kwamba aliamini huenda amerogwa lakini baada ya kuelimishwa na madaktari wanaoshughulika na ugonjwa huo ndipo alipokubali mtoto wake kuanzishiwa tiba.

Wanawake waliofika katika Kituo Cha Afya cha Kangunguli, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza kupata matibabu. Picha| Mariam John.

Anasema tiba ya kwanza aliyoanza kutibiwa ni ya kemikali kisha baadae aliandikiwa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufanyiwa upasuaji kuondoa sehemu iliyoathirika.

“Namshukuru Mungu toka mtoto afanyiwe upasuaji hali yake inaendelea vizuri na pia ninazingatia maelekezo niliyopewa na madkatari ambapo kwa sasa mtoto anaendelea vizuri,” anasema Mecktilida.Ni kweli saratani haiwapati watu wazima pekee. Hata watoto wanaweza kupata. Muhimu ni kuwa mzazi ukiona dalili zisizo za kawaida kwa mwili wa mtoto wako mpeleke hospitali akafanyiwe uchunguzi. 


Hali ilivyo katika hospitali ya rufaa Bugando

Kila mwezi Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza hupokea watoto 20 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wenye ugonjwa wa saratani na miongoni mwa saratani zinazoongoza kupokelewa kwenye hospitali hiyo ni pamoja macho, ini, matezi na saratani ya damu.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani na damu, Dk Heronima Kashaigili anasema saratani za watoto zinatibika iwapo mzazi atawahi kumpeleka hospitali ili kujua dalili za mapema.

“Changamoto iliyopo kwa sasa ni kwamba wazazi wanachelewa kuwapeleka watoto wao hospitali na wanapowafika wanakuwa kwenye hatua ya mwisho kitendo ambacho inakuwa gharama kubwa katika kuwatibu,” anasema Dk Kashaigili.

Anasema kwa sasa hospitali hiyo inafanya kazi karibu na Shirika la Kimataifa linalotoa Msaada wa Tafiti za Magonjwa ya Saratani (ICCARE) ambalo linatoa utafiti wa magonjwa ya saratani hasa kwa watoto.

Anasema kupitia shirika hilo, wazazi wanaelimishwa na wanapowawahisha watoto hospitali uwezekano wa watoto hao kupona ni mkubwa.

“Hata ugonjwa unapojirudia inakuwa ni mara chache na unapona kwa haraka, ingawa kinachoonekana katika mikoa hii kumekuwepo na Imani nyingi kuwa ugonjwa huo ni wa kurogwa kitendo kinachosababisha watoto kufikishwa hospitaali kwa kuchelewa na wengine kufariki,” anasema Dk Kashaigili.


Soma zaidi: 


Nini visababishi vya saratani kwa watoto?

“Hakuna sababu ya moja kwa moja hadi sasa ambayo inasababisha saratani kwa watoto ambapo zipo ambazo zinatokea tu na zingine zinachangiwa na mabadiliko ya vinasaba,” anasema Dk Kashaigili. 

Amesema dalili za za ugonjwa huo zinaweza kufanana kabisa na magonjwa ya kawaida ambayo yanawapata watoto.

Miongoni mwa dalili hizo kuwa ni upungufu wa damu, kuvimba kwa tezi, kuvimba tumbo, kupungua uzito, kupata makovu, kukosa hamu ya kula na kuvuja damu.

Zingine ni maumivu ya mwili, utando mweupe kwenye macho japo si kila utando ni dalili ya saratani na nyingine.

“Miaka ya nyuma wengi waliamini ugonjwa huo ni wa watu wazima lakini ukweli ni kwamba hata watoto wanaugua saratani hasa matezi, figo, jicho na saratani ya damu,” anasema Dk Kashaigili.


Tangazo:


Wadau wanaojihusisha na uelimishaji wa saratani

Hillary Sued ni mtafiti kutoka shirika la ICCARE nchini Tanzania anasema katika tafiti zao  ndogo zilizofanyika hivi karibuni zilibaini kuwa wagonjwa wengi waliokuwa wanakuja kutibiwa katika hospitali ya Bugando walikuwa wanaishia kenye dozi ya kwanza.

Anasema changamoto ni gharama za matibabu kuwa kubwa hivyo wengi kushindwa kumudu.

“Kutokana na changamoto hiyo, ICCARE ilianzisha program ya kuwasaidia watoto wenye saratani na waangalizi wao kumudu gharama za matibabu ya ugonjwa huo kwa kuwalipia hosteli, chakula na baadhi ya gharama zinazojitokeza wakati wa matibabu ya ugonjwa huo,” anasema Sued.

Kuhusu kufanya tafiti za ugonjwa huo anasema shirika linaendelea kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na zitakapokuwa tayari zitawekwa bayana.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV