Ifahamu kansa ya shingo ya kizazi na athari zake

January 10, 2023 6:38 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link

  • Husababishwa na maambukizi ya muda mrefu ya virusi vya  “human papilloma”
  • Virusi hivyo huenezwa kwa njia ya kujamiiana.
  • Upatikanaji duni wa kinga na matibabu huchangia asilimia 90 ya vifo duniani kote.

Dar es Salaam. Licha ya kuwepo nchini kwa miaka mingi kansa ya shingo  ya kizazi imeendelea kugharimu maisha ya wanawake wengi huku kukiwa na uelewa mdogo kuhusu chanzo cha ugonjwa huo na namna unavyoweza kuutibu.

Januari kila mwaka hutumika kutoa elimu na uelewa juu ya visababishi vya ugonjwa huo na jinsi ya kukabiliana nao kwa wasichana.

Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inasema kwa kiasi kikubwa saratani hii husababishwa na maambukizi ya mda mrefu (persistence infection) ya virusi viitwavyo “human papilloma”, ambavyo huenezwa kwa njia ya kujamiiana. 

“Kawaida mwili una uwezo wa hudhibiti maambukizi haya yaingiapo mwilini, lakini yasipodhibitiwa kikamilifu na kuwepo mwilini kwa muda mrefu husababisha ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi,” inasema taasisi hiyo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema matibabu ya mapema yanaweza kuokoa maisha ya wanawake takriban 342,000 waliopoteza maisha kwa ugonjwa huo mwaka 2020 na wagonjwa wapya 604,000 waliopata maambukizi hayo duniani kote kwa mwaka huo huo.

“Knsa ya shingo ya kizazi inazuilika  lakini upatikanaji duni wa kinga, uchunguzi na matibabu huchangia asilimia 90 ya vifo,” linasema Shirika hilo.

Hata hivyo, kabla ya mtu kupata madhara anaweza kugundua mapema dalili za ugonjwa huo kwa kujifanyia uchunguzi mwenyewe.

WHO inasema inachukua miaka 15 hadi 20 kwa saratani ya shingo ya kizazi kukua kwa wanawake walio na kinga ya kawaida na miaka 5 hadi 10 tu kwa wanawake walio na kinga dhaifu, kama vile walio na maambukizo ya VVU ambayo hayajatibiwa.

Enable Notifications OK No thanks