Fahamu dhana 5 potofu kuhusu Uviko-19

March 6, 2023 9:10 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na chanjo kutokuwa salama, na barakoa kutofanya kazi.
  • Baadhi huamini watoto hawawezi kueneza virusi vya Uviko-19.
  • Wataalam waonya chanjo ndiyo mkombozi sahihi katika vita dhidi ya Uviko-19.

Dar es Salaam. Wakati wanasayansi duniani wakiendelea kufanya tafiti za kina juu ya kirusi cha Uviko-19 kutokana na kujibadilisha mara kwa mara na kuibua milipuko mipya, dunia inakabiliwa na janga jingine la habari za uzushi ambalo limekuwa likiongeza athari za ugonjwa huo. 

Habari za uzushi kuhusu ugonjwa huo zimewafanya baadhi ya watu kupuuzia miongozo inayotolewa na wataalam wa afya na kusababisha ongezeko la vifo au kupata madhara ya kiafya ya muda mrefu.

Zifuatazo ni baadhi ya dhana potofu ambazo zimekuwa zikienezwa hasa kupitia mitandao ya kijamii au watu ambao hawana uelewa wa kutosha juu ya Uviko-19.

1.Chanjo si salama

Mwaka mmoja tu mara baada ya kuzuka kwa janga hilo wanasayansi na watafiti walikuja na chanjo ya Uviko-19 ambayo iliidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) baada ya kukidhi vigezo vya majaribio.

Chanjo ya Uviko-19 haikutoa suluhu iliyokusudiwa kwani ilikumbana na upinzani mkali kutoka kwa watu waliokuwa na imani potofu juu ya chanjo hizo kutokana na muda uliotumika ingawa mara kadhaa WHO imesisitiza hakuna chanjo iliyoidhinishwa ambayo si salama.

Kwa mujibu wa WHO mpaka sasa watu bilioni 5.1 wamepatiwa dozi kamili ya chanjo duniani kote, na hii inathibitisha kuwa chanjo hizi ni salama vinginevyo watu hao wangeshadhurika.

Rais Samia Suluhu Hassan akichapata chanjo ya Uviko-19 baada ya kuzindua rasmi utoaji wa Chanjo ya Uviko-19 Tanzania Julai 28, mwaka 2021. Pichal Ikulu mawasiliano

Mpaka sasa chanjo ndiyo njia iliyoonyesha ufanisi kwa zaidi ya asilimia 95 katika kukabiliana na maambukizi ya Uviko-19 ikiwa imeokoa zaidi ya vifo milioni 20 duniani kote.


2.Huhitaji chanjo kama umeshaugua Uviko-19

Baadhi ya watu huamini kuwa ikiwa umeshaugua Uviko-19 basi hauhitaji tena kupata chanjo. Jambo hili si kweli kwani kwa mujibu wa wataalam wa afya kinga ya mwili huanza kuimarika miezi mitatu baada ya mtu aliyeugua Uviko-19 kupona.

Kutokana na kirusi cha ugonjwa huo kujibadilisha mara kwa mara upo uwezekano wa mtu aliyeugua Uviko-19 kuugua tena mara ya pili wakati ambao bado afya yake haijaimarika na hivyo kuwa katika hatari ya kifo.


3. Barakoa hazifanyi kazi

Kuvaa barakoa kunasalia kuwa miongoni mwa njia bora ya kujikinga na maambukizi ya Uviko-19. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wataalam kutoka jarida la Heath Affairs ulionyesha barakoa zilisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kasi ya maambukizi mwaka 2020.

Wataalamu wa afya wanashauri mtu mwenye miaka miwili na kuendelea anaweza kuvaa barakoa  kuziba pua na mdomo anapokuwa sehemu za umma pamoja na kuweka umbali wa mita moja au hatua sita kati ya mtu na mtu.


Zinazohusiana


4. Watoto hawaenezi Uviko-19

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Havard cha nchini Marekani ulionesha kuwa hata watoto wana uwezo wa kupata na kusambaza maambukizi ya Uviko-19 kama watu wengine kutokana na kujibadilisha vinasaba kwa kirusi cha Omicron ambacho kinasambaa kwa urahisi zaidi.

Wataalam wa afya wanashauri ni muhimu kuwakinga watoto kwa kutumia barakoa na njia nyingine za kiafya kama kutoshiriki kwenye mikusanyiko pamoja na kunawa mikono kwa maji na sabuni.


5. Uviko-19 haina madhara ya muda mrefu

Kama nawe ni miongoni mwa watu waliokuwa na hizo fikra basi acha mara moja kwani wataalamu wa afya wanasema Uviko-19 inaweza kusababisha madhara ya kiafya ya muda mrefu kwa mtu yoyote.

Ukiona una dalili za uchovu, kukosa pumzi pamoja na kutosikia ladha ya chakula hata baada ya kupona Uviko-19 basi hizo ni dalili za madhara ya muda mrefu ambapo huwa ni pamoja na kuwa na hitilafu kwenye moyo, mapafu, ini, kibofu au ubongo.

Wakati huu ambao wanasayansi wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na kirusi kipya cha Kranken ni muhimu kwenda kupata chanjo ya Uviko-19 pamoja na kuzingatia tahadhari zote zinazopendekezwa.

Enable Notifications OK No thanks