Kodi, tozo za halmashauri pasua kichwa kwa wachimbaji wadogo

May 9, 2023 1:25 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Wachimbaji wadogo wa madini wakiwa kwenye Mkutano Mkuu Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA) uliofanyika jijini Mwanza. Picha | Mariam John.


  • Wazilaumu halmashauri kutoza kodi kubwa zisizo na uhalisia.
  • Majaliwa azitaka halmashauri kukutana nao kumaliz akero hizo.

Mwanza. Shirikisho la Wachimbaji wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) limeiomba Serikali kupitia upya kanuni za kodi na tozo kwenye halmashauri ili ziweze kufanana na zile zinazotungwa na Wizara ya Madini.

Akizungumza kwenye kongamano la Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo, Rais wa Femata, John Bina ameiomba Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa (Tamisemi) kutazama upya sheria hizo kwa kuwa zinawagandamiza wachimbaji.

Akitolea mfano kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita, Bina amesema madiwani wanatunga sheria ndogo za kodi ambazo ziko juu kuliko zile mama na zinatungwa bila kushirikisha wachimbaji jambo ambalo linasababisha kero kwa wachimbaji.

“Tunaomba Wizara ya Tamisemi pamoja na madiwani angalau kodi zifanane lakini hata yule anayetunga walau ashirikishe wizara ili asije na makodi makubwa mfano hapo Nyang’wale plant moja inatozwa Sh5 milioni na kuna wakati inakuwa haifanyi kazi lakini bado inatozwa makodi makubwa hivyo tunaomba suala hilo liangaliwe kwa kina,” amesema Bina.

Rais huyo wa wachimbaji pia ameeleza changamoto wanayokutana nayo ni uduni wa zana wanazotumia, ukosefu wa mitaji, kukosa sifa za kukopesheka katika mabenki, kutokuwa na taarifa sahihi za kijiolojia pamoja na kutokuwa na ufahamu wa sheria za madini.

Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa amesema wizara anatambua changamoto hizo na tayari wameendelea kubuni mbinu na mikakati mbalimbali katika kuzishughulikia.

Waziri Kiruswa amesema hadi kufikia Machi mwaka huu, jumla ya masoko 42 na vituo 93 za ununuzi wa madini vimeanzishwa kwenye maeneo mbalimbali ya uchimbaji wa madini ambayo yatawasaidia wachimbaji wadogo kupata masoko ya uhakika na  kutokuwa na sababu ya kutorosha madini.

Dk Kiruswa pia amesema kuhusu changamoto ya mitaji na vifaa bora wizara kupitia taasisi yake ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico) imeingia mkataba na taasisi za mabenki ambazo zimewezesha kuwakopesha wachimbaji wadogo zaidi ya Sh145 bilioni.

“Fedha hizi zimekopeshwa si kwa wachimbaji wadogo tu bali hata wakubwa nao wamekopeshwa, hivyo wizara inajitahidi kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuchochea uchumi wa Taifa,” amesema Dk Kiruswa.

Serikali yatoa tamko

Waziri Mkuu, Kassim Majalia amewaagiza mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya pale wanapotunga sheria ndogo wahakikishe wanashirikisha wadau wa sekta husika ili kupata mawazo yao.

“Msijifungie ndani kuweni kama wabunge, pale mnapotunga sheria hasa hizi ndogo zinazohusu kodi na tozo, washirikisheni wadau sio mnajifungia ndani na mnaiingiza mtaani mnaanza kukera watu, shirikisheni wadau na wao wazipitie waone na watoe mapendekezo yao,” amesema Majaliwa. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW