Filamu za kimataifa zilizotumia Kiswahili
- Ni pamoja na Lion King pamoja na Tomb raider 2
- Nyingi zimetumia mandhari na lafudhi ya Kenya
- Uhaba wa mawakala wa filamu kimataifa na gharama za kurekodi vyatajwa kama sababu
Dar es Salaam, Kiswahili ni miongoni mwa Lugha zinazoendelea kukua kwa kasi ulimwenguni jambo linaloongeza fahari kwa Watanzania ambao ndio wazungumzaji wa lugha hiyo kwa kiasi kikubwa ambako vyanzo mbalimbali vinaitaja Tanzania kama ndio chimbuko lake.
Ukuaji wake unadhihirika kutokana na ongezeko la matumizi ambapo kwa sasa lugha ya Kiswahili inatumika kama somo katika mataifa mbalimbali, inatumika kama lugha ya taifa, lugha ya mawasiliano pamoja na katika shughuli za sanaa ikiwemo, muziki pamoja na filamu.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Kiswahili ni mojawapo ya lugha zenye asili ya Afrika ambazo zinatumiwa sana ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200 duniani.
Huenda ukuaji wa lugha hii ndio umefanya baadhi ya waandaji wa filamu za kimataifa kutumia baadhi ya maneno ya kiswahili katika filamu zao, ili kunogesha pamoja na kuvutia watazamaji wapya.
Hivi karibuni watu wengi walionekana wakinukuu sehemu ya maneno ya kiswahili yaliyotumika katika filamu ya Fubar iliyoigizwa na Arnold Schwarzenegger, hata hivyo filamu hiyo si ya kwanza bali zipo nyingine nyingi zilizowahi kutumia lugha hiyo.
Makala hii fupi inaangazia baadhi ya filamu za kimataifa ambazo zimetumia lugha ya Kiswahili katika mazungumzo.
1. The Lions King
Filamu hii ilizinduliwa mara ya kwanza mwaka 1994 na kampuni ya Walt Disney Pictures ya nchini Marekani, na kurudiwa tena mwaka 2019 ambapo inaelezea kisa cha mtoto wa mfalme Mophasa aitwaye Simba namna ambavyo alikutana na kuvishinda vipingamizi katika safari ya kuurithi ufalme wa baba yake.
Katika filamu hiyo, maneno yenye asili ya lugha ya Kiswahili kama hakuna matata, simba, pamoja na rafiki yametumika kwenye sehemu ya mazungumzo ya filamu hiyo pamoja na majina ya wahusika.
2. Tomb raider 2: (The Cradle of Life) 2003
Lara Croft (Angelina Jolie) anasafiri hadi Afrika kutafuta sanduku la Pandora, huko anazungumza na chifu wa kijiji akiomba ruhusa ya kuingia kwenye eneo linaloaminika kuwa ni chimbuko la maisha/uhai wa watu wa eneo hilo.
Chifu wa eneo hilo anakataa jambo hilo kwa kuwa anadhani ni hatari sana na hakuna mtu aliyewahi kwenda huko na akarejea.
Katika mazungumzo yao wanazungumza lugha ya Kiswahili huku ambapo baadhi ya maneno yanayosikika ni pamoja na “mnataka nini”, “acha hicho chuma na uende”, “ wewe kweli unaelewa unachofanya”, “haya mambo ni mazito”
3. The Crown Season 1
Filamu hii ya kihistoria ambayo ilianza kuoneshwa kupitia Kampuni ya filamu Netflix mwaka 2016 inaelezea msururu wa maisha ya Malkia Elizabeth II, kuanzia alipoutwaa ufalme kutoka kwa baba yake Mfalme George VI.
Lugha ya Kiswahili ilitumika wakati Elizabeth na mume wake Philip walipoenda mapumzikoni nchini Kenya mwaka 1952 ambapo wanaonekana wakikaribishwa kwa neno la kiswahili “Karibu”.
4. Queen Sono
Queen Sono hii ni filamu ya Afrika kusini inayoangazia masuala ya visa vya ugaidi iliyoandaliwa na Kagiso Lediga ambapo ilianza kuonyeshwa kwenye jukwaa la Netflix kuanzia Februari 28,2020.
Katika filamu hiyo pamoja na kutumia lugha mbalimbali zimetumika kama vile Kiingereza, Kiafrikaans, na Kixhosa baadhi ya maneno ya kiswahili yamesikika ambapo walitumia pia mandhari ya Afrika Mashariki kama vile Zanzibar na Nairobi wakati wa kurekodi.
5. The white Massai
The White Massai ni filamu ya mwaka 2005 iliyoongozwa na Hermine Huntgeburth. Filamu hiyo inamhusu Carola (Hoss), mwanamke wa Kijerumani anayeishi Uswisi anaye kwenda likizo na mpenzi wake nchini Kenya lakini ghafula anaangukia kwenze penzi jipya na mwanaume wa kimasai Lemalian (Ido) hatimaye wanaanza kuishi pamoja.
“Watoto kujeni niwatume” ni sentensi ambayo ilizungumzwa ndani ya filamu hiyo wakati Carola alikuwa akimtafuta Ido.
Mandhari na lafudhi ya Kenya inatumika zaidi kuliko Tanzania
Licha ya idadi kubwa ya wazungumzaji wa kiswahili kuwa nchini Tanzania, asilimia kubwa ya filamu zinazotumia lugha ya kiswahili, lafudhi yake huwa ni ya watu wa Kenya.
Mtayarishaji na mwandishi wa filamu nchini Tanzania Kefa Igilo ameeleza kuwa uchache wa mawakala wa filamu pamoja na kutofahamu lugha ya kiingereza ni miongoni mwa sababu zinazosababisha filamu hizo kutumia kiswahili chenye lafudhi pamoja na mandhari ya Kenya.
“Kwa upande wa Kenya mawakala wengi wa filamu kuliko hapa nchini, na sisi tulikuwa hatufahamu jambo hilo, kwa hiyo mtayarishaji inakuwa ni vigumu kuja tu kufanya kazi mahali ambapo hataweza kupata uaminifu katika kukamilisha kazi hiyo” amesema Igilo
Igilo ameongeza kuwa sababu nyingine ni kikwazo cha lugha kwa kuwa watayarishaji pamoja na waandishi wa filamu hupendelea kutumia lugha ya Kiingereza jambo linalowabeba Kenya kwa kuwa ni lugha ambayo wanaitumia katika shughuli zao za kila siku tofauti na Tanzania ambapo asilimia kubwa huzungumza kiswahili.
Sababu nyingine ni utunzi na utayarishaji wa filamu hiyo, huenda kulingana na kisa au stori mtayarishaji anahitaji mandhari ya Kenya pamoja na lafudhi kiswahili cha pwani lakini kinachotokea Kenya ili kukamilisha ujumbe ambao anahitaji kuutoa kupitia filamu hiyo.
Soma zaidi
- Monster Hunter: Filamu ya kuisindikiza wikiendi yako
- Unavyoweza kujikinga na magonjwa ya figo
- Jinsi ya kujinasua kwenye upweke, unyonge
Gharama na sheria za Tanzania ni kikwazo
Mwenyekiti wa Chama cha Wasanii wa Sanaa za Uoni Robert Mwampembwa ameiambia Nukta Habari gharama kubwa za kurekodi filamu Tanzania pamoja na sheria ambazo sio rafiki ndio sabahu inayowazuia watayarishaji na waandishi wa filamu kuja kufanya kazi Tanzania tofauti na Kenya ambapo gharama na sheria zao ni rafiki.
“Kibali ni Dola za Marekani 1000 (Sh 2.4 milioni) kwa raia wa nje na kwa mzawa ni Sh500,000 hii ni kubwa lakini wakenya hawana gharama kubwa, pia urasimu ni mkubwa katika bodi yetu ya filamu, na sheria zetu bado sio rafiki,” amesema Mwampembwa.
Mwampembwa amesema Serikali inapaswa kufanya mabadaiiko kwenye Sheria ya Filamu ya 1976 ambayo japo imefanyiwa marekebisho mara kadhaa mwaka 2013 na 2019 lakini bado s inapigiwa kelele.
Baadhi ya filamu za kimataifa ambazo zimewahi kurekodiwa Tanzania ni pamoja na Hatari mwaka 1962 pamoja na Queen Sono mwaka 2020.