Mfahamu Paulina, mwanamke msomi anayetengeneza majiko banifu Dodoma
- Ni mhitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Biashara aliyeamua kufanya kazi ya kuchomelea vyuma.
- Majiko anayoyatengeneza yamesaidia kupunguza gharama za maisha na kutunza mazingira.
Dar es Salaam. Kwa miaka miwili sasa amekuwa akifanya kazi hii inayomfanya kuwa miongoni mwa wanawake wachache walioamua kuvunja miiko ya kijinsia iliyopo kwenye shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato.
Ni mke, mama, msomi na mpambanaji ambaye wakati wote anapofanya kazi hii haoni tofauti yoyote kati yake na wanaume kutokana na elimu, uzoefu na uwezo wa kufanya kazi hii ya kuchomelea vyuma.
Huyu ni Paulina Chuma msomi wa Shahada ya usimamizi wa biashara aliyeamua kufanya kazi ya kuchomelea vyuma mwaka 2021 na hatimaye kuanzisha kampuni iitwayo Pahiro akiwa na wenzake wawili.
Pamoja na mambo mengine kampuni hiyo imejikita zaidi katika uzalishaji wa majiko banifu, ambayo ni rafiki kwa mazingira kwa kuwa yanapunguza matumizi ya mkaa kwa kiasi kikubwa.
Ilikuwaje?
Changamoto ya kutopata ajira inayohusiana na taaluma yake ya usimamizi wa biashara aliyosomea ilimfanya ageukie fursa ya uuzaji wa majiko banifu.
Awali alikuwa akinunua majiko hayo kutoka kwa watu wengine kisha yeye kwenda kuuza, baadae akakata shauri ya kwenda kujifunza juu ya utengenezaji wa majiko hayo.
Safari yake haikuwa rahisi, mshangao wa wazi ulionekana kwa baadhi ya watu kutokana na yeye kuachana na kazi zinazohusiana na taaluma yake na kujikita kwenye fani inayodhaniwa kuwa ya wanaume pekee.
“Tulikuwa tunakutana na changamoto mwanzoni watu wanatuuliza kwanini ninyi wanawake mnafanya shughuli za welding (kuchomelea) baadae imekuja kuonekana ni kitu cha kawaida,” anasema Paulina.
Paulina Chuma (kulia) akielezea jambo kwa mteja aliyetembelea banda lake katika maonyesho ya 47 ya biashara maarufu kama sabasaba jijini Dar es Salaam.Picha |Daudi Mbapani/Nukta Africa.
Kwanini ‘majiko banifu’
Hamasa ya kutumia nishati safi kupikia inayoendelea kutolewa ili kupunguza kasi ya manadiliko ya tabia nchi yanayochangiwa na uharibifu wa mazingira ndio vilimshawishi yeye na wenzake kujikita zaidi kutengeneza majiko banifu.
Hata hivyo kwa kuwa si watu wote wangeweza kuhamia katika matumizi ya nishati ya gesi kwa mara moja, ujuzi wao ulikusudia kuleta suluhu ya kutunza mazingira kwa kuwa majiko hayo yanatumia mkaa kidogo na upatikanaji wake ni wa gharama nafuu.
“Tulivyokuja kusikia kwamba tunatakiwa kuhamia kwenye matumizi ya gesi tukawaza kwamba huwezi kumhamisha mtu anayetumia kuni moja kwa moja kuja kwenye gesi…
…Kama hatua za mtoto anakaa, anatambaa na kusimama tukasema labda tuanze na kupunguza matumizi ya mkaa ndipo watu wanaweza kuhamia kwenye gesi,” amebainisha Paulina.
Jiko hilo lililotengenezwa kwa bati nzito nyeusi, lina mishikio miwili inayomuzesha mtumiaji kulihamisha kwa haraka,lina sehemu ndogo ya kuwekea mkaa katikati ambayo kwa chini imezuiwa kwa wavu mgumu ili mkaa usitoke kirahisi.
Pembeni ya tundu hilo kuna bati zito lilinalokinga mkaa kukutana na bati la nje na kupoteza joto, kwa juu limewekewa chuma kizito na mafiga manne yanayoiwezesha sufuria kukaa vyema wakati wa kupika.
Kutokana na biashara yao kukua, hawatengenezi majiko madogo pekee kwa sasa wana uwezo wa kutengeneza majiko makubwa yanayoweza kutumiwa na taasisi yenye watu wengi.
“Tumeegemea zaidi katika utengenezaji wa majiko tunatengeneza majiko ya nyumbani kama hivi, majiko makubwa na sufuria kubwa zinazotumika katika taasisi,” amesema.
Tanzania imeazimia kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033 ikiwa ni utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) ya mwaka 2030
Wizara ya Nishati inatarajia kuzindua Dira ya taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia itakayoimarisha matumizi ya nishati hiyo ifikapo mwaka 2033, ambapo inatarajiwa angalau asilimia 80 ya wanachi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Waziri wa Nishati January Makamba aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24 aliwaambia wabunge kuwa wizara yake imetenga Sh4.5 bilioni kwa ajili ya kuhamasisha, kuelimisha wananchi, kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo inayohusu nishati safi ya kupikia.
Linapunguza gharama za maisha
Silvia Bernard ambaye ni miongoni mwa wateja wa majiko hayo ameiambia Nukta habari kuwa tangu ameanza kutumia majiko hayo mwezi April mwaka huu 2023, yamempunguzia matumizi ya mkaa kwa kiasi kikubwa.
“Majiko yake ni mazuri sana yanapunguza matumizi ya mkaa mfano mimi nilikuwa natumia Sh3,000 kununua mkaa ninaoutumia siku moja lakini sasa mkaa huo huo naweza kutumia kwa zaidi ya siku tano,”amesema Silvia ambaye ni mkazi wa Dodoma.
Soma zaidi
Ni safari yenye matumaini
Mwanzilishi Mwenza wa Kampuni hiyo Rogers Henry anasema ilimlazimu kufanya maamuzi magumu ya kuungana na wanawake hao kutokana na jamii iliyomzunguka kumshangaa na kutotegemea kama angeweza kuvumilia kufanya kazi na wanawake.
“Wengi waliniambia huwezi kukaa na wanawake muelewane, mbona wanaonekana kama hawataweza kazi ya shuruba…sasa hivi wanashangaa mpaka sasa hivi tupo wote na wanaweza kazi,” amesema Henry.
Rogers ameongeza kuwa kwa sasa, amejifunza kuwaamini wanawake na uwezo wao katika kazi kutokana na juhudi anazoziona kwa mke wake na binti yake ambao wamekuwa wakitamani kujifunza kazi anazozifanya.
Fundi huyo aliyewahi kufanya kazi na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) anasema wanamatumaini zaidi ya kuongeza ufanisi na uzalishaji katika kampuni hiyo kutokanana uhitaji wa bidhaa hizo ndani na nje ya mkoa huo.
Kazi hiyo haijabadilisha maisha ya Paulina na wamiliki wenza wa kampuni hiyo pekee bali imesaidia vijana wengine watatu ambao ni wahitimu kutoka sido na Chuo Cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).